Wednesday, 19 July 2017

Huwezi Kuchagua Wazazi Na Ndugu, Unaweza Kuchagua Marafiki

Hata kama umezaliwa na wazazi maskini au wabaya kiasi gani huwezi kuchagua nani awe baba yako au mama yako. Huwezi kuchagua nani awe ndugu yako. Baba yako hata kama ni mlevi kiasi gani analewa tilalila, huwezi kuchagua baba mwingine ndiye hiyo Mungu amemuumba awe baba yako.

Ndugu yako hata wawe wakorofi vipi, huwezi kuchagua na kusema wewe sio ndugu yangu ndo imekwisha tokea hakuna namna. Dunia ipo hivyo toka vizazi hata vizazi. Yusufu katika Biblia alikataliwa na ndugu zake na hatimaye kuuzwa kama mtumwa huko nchi ya Misri, lakini baadaye ndiye aliyekujq kuikomboa familia yake isije kufa na njaa huku akiwaambia nduguze, "Mimi ndiye Yusufu ndugu yenu mliyemuuza."

Kanuni hii ya chaguzi inageuka pale linapokuja suala la kuchagua marafiki. Rafiki hata awe mzuri namna gani au mbaya namna gani ni uchaguzi wako pekee ambao utaruhusu nani ujenge naye urafiki na nani usijenge naye urafiki.

Marafiki wana mchango mkubwa katika Maisha yeti. Marafiki wanaweza kukufanya uendelee au wanaweza kukufanya urudi nyuma. Wanaweza kukujenga au kukubomoa. Marafiki wanaathiri sana tabia zetu na hata utendaji kazi wa Maisha yetu ya kila siku.

Uchunguzi unaonesha kwamba, tabia zq marafiki zako watano unaokaa nao muda mwingi ndizo tabia zako wewe mwenyewe. Tony Robbins mwandishi maarufu wa Vitabu toka Marekani anasisitiza, "Wewe ni wale unaoambatana nao muda mwingi."

Ndio maana kwenye kitabu changu cha Barabara Ya Mafanikio niliandika sura niliyoipa jina la "Niambie rafiki yako, nikwambie tabia zako." Waliokisoma wananielewa zaidi.

Chagua Leo kuwa na marafiki kwenye malengo, tafuta marafiki wanaowaza mambo chanya, jichanganye na marafiki wanaowaza na wanaopambana kufanikiwa, tafuta marafiki wanaowaza maendeleo.

Achana na marafiki wanaowaza starehe, watakuchelewesha, achana na marafiki wanaopoteza muda wao mwingi kujadili Maisha ya wengine, hawa utawakuta wanajadili "mtu fulani analipwa shilingi ngapi au anamiliki pesa kiasi gani." Tena wanabisha kwa hoja Kali wakati pesa anayolipwa au kumiliki mtu huyo wao hawapati faida hata ya seti tano.

Achana na Marafiki ambao kila kukicha wao ni kujadili mipira ya Simba na Yanga. Ni mashabiki tu ambao mara nyingi hata. Kadi za timu hizo hawana. Hawa Watakuchelewesha.

Bill Gates ambaye ni tajiri namba moja duniani na Warren Buffet ambaye ni tajiri namba tatu duniani na mwekezaji namba moja wa karne ya ishirini na moja walikutana tarehe 5 mwezi Julai mwaka 1991 na kuanzisha urafiki. Tarehe kama hiyi mwezi Julai mwaka 2016 walifanya sherehe ya kuazimisha miaka 25 ya urafiki wao. Hapo ndipo msemo naamini msemo wa Wahenga unaosema "Ndege wenye mabawa yanayofanana, huruka pamoja."

Kumbuka: Huwezi kuchagua wazazi wala ndugu, lakini unaweza kuchagua marafiki. Chagua Leo marafiki sahihi. Ambatana na marafiki sahihi.

"Mafanikio Yapo Mikononi Mwako."

Ndimi
EDIUS KATAMUGORA
AUTHOR AND MOTIVATIONAL SPEAKER
0764145476
0625951842
Email: ekatamugora@gmail.com

Karibu ujipatie kitabu changu cha BARABARA YA MAFANIKIO, Kwa shilingi 6000/= mikoani tunatuma pia.

Imani yangu ni kwamba mafanikio ni kitu cha kushirikishana, washirikishe na wenzio kile ulichojifunza.  

Hii ni blogu rasmi ya Edius Katamugora, hapa utajifunza maendeleo binafsi, utapata makala mbalimbali zinazohusu biashara, elimu, hamasa na maisha kwa ujumla. Karibu sana katika blogu hii.

0 comments: