Friday, 8 December 2017

Wakati nikiwa nasoma kidato cha pili nilipewa kitengo cha somo la Jografia ambapo nilikua nafanya kazi pia katika kituo cha utabiri wa hali ya hewa.

Kupewa kitengo hiki ilikua faraja kubwa sana kwangu kwani niliweza kujifunza mambo mengi. Nikiwa nafanyakazi katika kitengo hicho nilipata kazi ya kufanya kazi kwa ukaribu sana na Idara ya utabiri wa hali ya hewa ya taifa.

                                            
                         

Katika kituo hicho cha hali ya hewa nilikua nikichukua vipimo vya jotoridi na mvua kazi ambayo niliifanya kila siku bila kukosa kwa upimaji wa mambo ya hali ya hewa. Pili nilikua nikitunza kumbuka zote zinazohusiana na mambo ya hali ya hewa katika kituo changu ambazo baadae zilitumwa kwenye Idara inayohusika na utabiri wa hali ya hewa ya taifa.

Mojawapo ya changamoto kubwa niliyokumbana nayo katika kazi hiyo, ilikua ni lazima ufanye kazi kila siku, haijalishi umebanwa kivipi au unafanya shughuli gani. Kazi yangu hii pia ilikua ngumu kipindi cha mvua, maana muda wa kupima ulikua saa 3.15 asubuhi hivyo hata kama mvua inanyesha utakwenda kupima mvua na kisha itakayoendelea kunyesha itahesabika kama mvua ya kesho.

Kitu kikubwa nilichojifunza katika kazi hii ni kwamba data za hali ya hewa zinazokusanywa hutumika katika kukadiria hali ya hewa ya siku zijazo. Mfano unaweza kuambiwa kwamba mwakani kutakuwa na mvua chache hivyo wakulima jiandaeni kutunza mazao na vitu kama hivyo. Au nafikiri umewahi kuona kwenye televisheni wakielezea kuhusu utabiri wa hali ya hewa ambapo kwa mfano utaambiwa kesho mvua itanyesha, au kutakuwa na wingu kiasi.

Kunasomo kubwa ambalo mimi binafsi nililipata hapa na ningependa wewe pia ujifunze pia. Somo lenyewe ni "Kesho ni Leo."

Kwenye utabiri wa hali ya hewa utaambiwa mambo yanayohusu kesho, mwezi ujao, mwaka ujao au hata miaka mitano ijayo. Hiki ni kitu cha kushangaza lakini hayo yote hutokea.

Wewe pia unahitaji kuitabiri kesho yako. Ukitaka kuwa mtu Mwenye mafanikio unahitaji kuwa mtabiri wa kesho yako unahitaji kuwa mtu anayeona kesho kama Leo. Sifa moja wapo ya watu waliofanikiwa ni kuwa na maono makubwa, yaani kujiona tayari wapo katika hali Fulani ambayo wanaitegemea.

Wewe pia unahitaji kufikiria baada ya miaka mitano au kumi utakuwa mtu wa namna gani. Hii itakupa motisha kila siku kufanya jambo Fulani ili usogee kule unakotaka kufika. Helen Keller pamoja na kuwa kipofu akiwa na umri wa miaka miwili ambaye pia ni mwandishi gwiji wa karne ya ishirini aliishia kusema "Ni bora kukosa kuona kuliko kukosa kuwa na maono." Unahitaji pia kuwa mtu ambaye anaiona kesho Leo hii. Unahitaji kuwa mtu anayepiga picha ya maisha yako ya baadae. Kama utabiri wa hali ya hewa ya kesho unavyofanyika Leo wewe pia unahitaji kutabiri maisha yako ya kesho Leo hii.

Jione kama mtu ambaye tayari amekwisha fanikiwa kufanya jambo Fulani, hii itaifanya akili yako kupambana na kuhakikisha jambo hilo linafanyika.

 Godius Rweyongeza katika kitabu chake cha Tatizo Sio Rasirimali Zilizopotea anasema "Huwezi kufika kimwili kule unakokwenda kabla haujafika kiakili." Peleka mawazo yako kule unakotaka kwenda, weka akili yako kule unakofikiria kufika lazima utafika. "Chochote akili inachokiamini na kukiwazia muda mwingi lazima kitokee." Aliwahi kusema Napoleon Hill

Je unaiwazia kesho yako au kila siku upo tu unaifikiria Leo na Jana? Kuanzia Leo kuwa mtu mwenye maono makubwa, kuwa mtu anayepiga picha za kesho zako. Wewe ni kile kitu ambacho unakiwazia muda mwingi.

Mojawapo ya watu wanaofanya vizuri katika kuitabiri kesho ni wasanifu majengo. Hawa kwanza uliweka jengo wanalotaka lijengwe katika mfumo wa karatasi ngumu zilizounganishwa(ambazo hufanana na jengo litakalo jengwa). Baadaye karatasi hizo ngumu huletwa katika uhalisia na kuwa jengo kamili lililosimama ardhini. Hawa wanatengeneza picha na baadaye wanaileta picha yao katika jambo linaloonekana. 
Tengeneza picha ya kesho yako.

"Nilimwambia baba yangu kwamba siku moja tutakuwa matajiri na tutakuwa na nyumba kubwa lakini hakuaniamini. Nilifanya kweli!" Anasema Christian Ronaldo mchezaji maarufu wa mpira wa miguu toka Ureno, mchezaji wa Real Madrid na mshindi wa tuzo ya UEFA 2017.Jifunze kuiona kesho yako. Jifunze kuitabiri kesho yako.

Mafanikio yakomikononi mwako.

Ndimi:
Edius Katamugora
Mwandishi na Mhamasishaji
0764145476
0625951842 (WhatsApp)
Email: ekatamugora@gmail.com
Instagram: ediuskatamugora

Jipatie kitabu cha Barabara Ya Mafanikio kwa shilingi 6000 tu. Piga 0764145476
Imani yangu ni kwamba mafanikio ni kitu cha kushirikishana. Mshirikishe na mwenzako kile ulichojifunza.

Hii ni blogu rasmi ya Edius Katamugora, hapa utajifunza maendeleo binafsi, utapata makala mbalimbali zinazohusu biashara, elimu, hamasa na maisha kwa ujumla. Karibu sana katika blogu hii.

0 comments: