"Kama unafikiri wewe ni mdogo kiasi cha kutoleta tofauti, haujawahi kukesha usiku kucha ukiwa na mbu." Ni methali ya Kiafrika.
Mbu ni viumbe wadogo sana lakini wakati wa usiku tukiwa tumelala wanafanya maajabu makubwa. Unaweza kuwa umelala na haujashusha chandarua ukaumwa na mbu mmoja ukiamka unajikuta umevimba usoni na unaweza kufikiri kulikuwa na jeshi la mbu chumbani kwako kumbe ni mbu mmoja tu. Mbu huyo huyo anaweza kukupatia ugonjwa hatari wa Malaria ambao ndiyo ugonjwa unaoua watu wengi duniani kila siku hasa watoto wadogo chini ya miaka 5.
Kama mbu mdudu mdogo sana anaweza kufanya mambo haya, kwanini wewe ushindwe kufanya kitu cha tofauti? Methali hii ya Kiafrika inatukumbusha kwamba kila mtu anaweza kufanya kitu cha tofauti na kikaleta mchango katika jamii. Usijidharau na kusema mimi ni mdogo au umri umekwenda. Umri wako kuwa mdogo au mkubwa hiyo ni fursa. Colonel Sanders alianzisha KFC akiwa na miaka 62, Je wewe unayesema umri umekwenda na haufanyi lolote umri wako unalingana na wa Colonel Sanders?
Ukisema wewe bado u mdogo kufanya kitu Fulani hivyo ni visingizio tu na havitakupeleka kokote. Kuanza mapema katika umri mdogo ni fursa kubwa kwani utajua mambo mengi mapema na hivyo kutanuka kifikra na kiutendaji, utaweza kufanya mambo kwa weledi mkubwa.
Kila mtu anakitu cha tofauti alichozaliwa nacho na anadaiwa kukileta duniani na kukifanyia kazi. Mimi na wewe tunalo jukumu hilo.
Kuna baadhi ya vitu ambavyo umezaliwa navyo ambavyo unavyowewe peke yako;
- Sauti yako ni ya kipekee, hakuna mtu mwenye sauti kama yako.
- Macho yako ni ya kipekee. Dunia nzima hakuna mtu mwenye macho kama yako.
- Alama za vidole vyako havifanani na vya mtu mwingine yeyote.
- Jambo la kushangaza zaidi katika mamilioni ya watu waliowahi kuishi duniani na wanaoendelea kuishi Leo hii hakuna mtu hata mmoja mwenye mapigo ya moyo kama yako.
- Kitabu ulichonacho kiandike.
- Nyimbo ulizonazo ziimbe.
- Jumbe za hamasa ulizonazo zitoe.
- Biashara uliyonayo ianzishe.
- Blogu uliyonayo ianzishe.
- App uliyonayo, ianzishe.
- Makala ulizonazo, ziandike.
- Wazo ulilonalo, anza kulifanyia kazi.
Wewe ni wa tofauti tunategemea utuletee kitu cha tofauti na cha kipekee. Na dunia siku zote inawapokea watu wanaofanya vitu vya tofauti na vya kipekee.
Uchunguzi unaonesha kwamba kila mwanadamu anazaliwa na uwezo,ujuzi na vipaji kuanzia 500-700. Je ni uwezo,ujuzi na kipaji gani umekionesha na kuleta tofauti?
*Mafanikio yako mikononi mwako.*
Edius Katamugora
Mwandishi na Mhasishaji
Mwandishi na Mhasishaji
0764145476
0625951842 (WhatsApp)
Email: ekatamugora@gmail.com
Instagram: ediuskatamugora
Www.bideism.blogspot.com
0625951842 (WhatsApp)
Email: ekatamugora@gmail.com
Instagram: ediuskatamugora
Www.bideism.blogspot.com
Share kwa marafiki zako kuwakumbusha jambo hili.
0 comments:
Post a Comment