#3:
MCHUNGUZE MWANAO ANAPENDA NINI
Kila mzazi anao wajibu wa kuchunguza
na kutizama mwanae anapenda kufanya nini. Mchunguze ni mambo gani anapendelea
kuyafanya muda mwingi. Labda anapenda kulisha wanyama, huyu anaweza kuwa
daktari wa wanyama, labda anapenda kufundisha wenzake, huyu anaweza kuwa mwalimu
au profesa wa chuo kikuu, labda anapenda kuimba, huyu anaweza kuwa mwanamuziki,
labda anapenda kushona, huyu anaweza kuwa fundi anayeshona mitindo mbalimbali,
labda anapenda mambo ya ujenzi, huyu anaweza kuwa mhandisi wa ujenzi au msanifu
majengo. Wahenga walisema, “Mahali moyo
wako ulipolalia, ndipo miguu yako huamkia.” Kama mzazi una wajibu mkubwa wa
kuchunguza mwanao anapenda kufanya mambo gani.
#4:
USIMLAZIMISHE MWANAO ASOME KITU ASICHOKIPENDA
Kuna wazazi wengi wameua watoto wao.
Usishangae kusema hivyo lakini hapa namaanisha, kuna wazazi wengi wameua ndoto
za watoto wao. Mtoto anataka kuwa mwalimu, mzazi anamlazimisha asome na kuwa
mwanasheria. Hii ni hatari kubwa ambayo imesababisha dunia ikose wataalamu
katika sekta mbalimbali. Ukimlazimisha mwanao asome kitu asichokipenda hata
kidogo ni sawa na kumchukua samaki na kumleta nchi kavu, unategemea nini?
Samaki huyo hawezi kuishi. “Mkono hata
uwe mzuri namna gani kwako ni begani,” unatukumbusha msemo wa Kiswahili. Kuna
watu wengi wanafanya kazi zisizo zao. Kadiri ya takwimu za mwaka 1987 Waamerika
asilimia 24.3 hawana furaha kwa sababu walichagua kazi ambazo hazikupaswa kuwa
kazi zao. Hii ni kutokana na kufanya kazi wasizozipenda. Kuishi maisha yasiyo
na furaha ni msalaba mkubwa. Miaka ya hivi karibuni kiwango hicho kimeongezeka
na kufikia asilimia 87. Wazazi wengi wamekuwa wakiwalazimisha watoto wao wasome
kozi fulani kisa kozi hizo zina ajira kumbe wanafanya makosa makubwa.
Nikukumbeshe wewe mzazi kuwa siku hizi kozi zote hazina ajira, karibu kila kozi
kuna wahitimu wengi wapo mtaani ambao kila kukicha wamekuwa wakitafuta kazi
ofisi hadi ofisi. Mwanao akisoma kozi anayoipenda ni rahisi hata kujiajiri.
Kama hupendi kitu unachokisoma hata ile nguvu ya kusema nitajiajiri huwezi
kuipata. Nchini Kenya kuna baba mmoja alimlazimisha mwanae asomee udaktari, kijana
huyo hakutaka kukwazana na baba yake ingawa yeye hakupenda kuwa daktari
alipenda kuwa muhasibu. Baada ya kusoma na kumaliza miaka mitano kijana huyo
alitunukiwa shahada ya juu ya udaktari akiwa na daraja la kwanza (Upper Class).
Yule kijana alipofika nyumbani kwao alimwambia baba yake maneno yafuatayo,
“Baba, ulitaka nisome niwe daktari, vyeti vyako hivi hapa. Sasa narudi chuo
kusoma kitu ninachokipenda.” Kijana huyo alirudi chuo kuanza kusomea uhasibu.
Siku moja rafiki yangu Saada Mpandachalo aliwahi kuniambia maneno
yafuatayo, “Kuna haja kubwa ya semina
kwa wazazi wetu. Wengi tunatumbukia kwenye shimo la ndoto za familia kwasababu
hatutaki kuonekana disobidients (wasio na adabu). Wakati mwingine dreamer (mwenye
ndoto au muotaji) hapewi usingizi anaouhitaji, kila akitaka kuota anamwagiwa
maji ya hofu ya laana. Tuangaze juu pia.”
Itaendelea...
Ndimi:
EDIUS KATAMUGORA
0764145476
ekatamugora@gmail.com
WEKA ODA KUPATA KITABU CHA NAMNA YA KUWA MTAALAMU UKIWA BADO UNASOMA KUPITIA 0764145476
0 comments:
Post a Comment