Thursday, 29 March 2018

MCHANGO WA MZAZI KWA MTOTO KATIKA KUUTAFUTA UTAALAMU III

Inaendelea sehemu ya III



#5: MKUTANISHE NA WATAALAMU.
Baada ya kugundua mwanao anapenda nini jitahidi sana kumkutanisha mwanao na wale watu wanaofanya vitu anavyopenda kuvifanaya siku za mbeleni. Hawa watampa hamasa ya kufanya zaidi na mbinu gani anaweza kufanya ili naye aweze kuwa mtaalamu. “Nimefika hapa nilipo kwa kusimama kwenye mabega ya wengine,” alisema Albert Eistein. Mwanao pia anahitaji mabega ya kusimamia ili afike mahali anakotaka kufika. Ili awe mtaalamu katika uwanja wa ndoto yake. Baada ya kukutana na waandishi wengi na kufahamiana nao nimepata kujifunza mambo mengi kuhusu uandishi na wamekuwa watu wanaoniambia kila kukicha, “Usichoke kuandika.” Mwanao pia anahitaji kukutanishwa na watu wa namna hiyo.
 
   
 Image result for AFRICAN MOTHER TEACHING HER SON

#6: HAKIKISHA MWANAO ANAJUA SOMO LA HESABU
  Strive Masiyiwa aliwahi kuandika kwenye ukurasa wake wa Facebook kwamba, kama mwanao hajui hesabu mzazi unafanya makosa makubwa. Dunia ya sasa hivi inabadilika ni dunia inayoendeshwa kwa hesabu sana kuliko ilivyokuwa hapo nyuma, hivyo ni wajibu wa kila mzazi kuhakikisha kuwa mwanae yuko vizuri katika somo la hesabu. Mzazi unahitaji kujua kama mwanao shuleni anaye mwalimu mzuri wa somo la hesabu. Ukiona mwanao hafanyi vizuri kwenye somo la hesabu hakikisha unafanya jitihada zote awe vizuri katika somo hilo. Ukweli ni kwamba somo la hesabu sio somo gumu kama wengi wanavyolichukulia lakini inatokana na watu wengi kuliogopa tu hata kabla hawajajifunza kitu chochote. Mwanao akiweza kujua somo la hesabu vizuri ni rahisi sana kujua masomo mengine. Hata kama mwanao ana ndoto za kufanyia kazi masomo ya sanaa mwambie dunia imebadilika inaenda katika sehemu ambayo hesabu aikwepeki. Mtafutie mwanao masomo ya ziada. Kama mzazi usiruhusu mwanao afanye vibaya katika masomo ya hesabu. Hii itaaharibu kesho yake.



#7: MFUNDISHE MWANAO ELIMU YA PESA
  Familia nyingi za kiafrika hazina utamaduni wa kuwafundisha watoto wao elimu kuhusu pesa. Hakuna shule itakayo mfundisha mwano kuweka akiba, hivyo ni jukumu lako wewe mzazi kumfundisha mwanao elimu kuhusu pesa. Mfundishe mwanao namna na jinsi ya kuweka akiba. Mwambie kila pesa anayoipata ajifunze kutoitumia yote bali achukue kiasi na kuweka akiba. Mwambie mwanao anapokuwa bado yu kijana ajifunze kuwekeza katika maeneo mbalimbali na awe na matumizi mazuri ya pesa. Hata maandiko yanatuuliza, “Katika ujana wako hukukusanya, utapata wapi upatapo kuwa mzee?” (Yoshua Bin Sira 25:3) Ukifanikiwa kupata pesa hakikisha unawafundisha wanao somo hilo gumu la pesa ambalo duniani hakuna shule yoyote inayotoa elimu kuhusu pesa. Wafundishe wanao namna ya kudhibiti mzunguko wao wa pesa na pia njia mbalimbali za kutafuta pesa. Kama mwanao leo hawezi kujua matumizi mazuri ya elfu tano hata apewe milioni mia mbili hawezi kamwe kuzimudu. Ndio maana baada ya wazazi matajiri kuwarithisha watoto wao mara nyingi familia za hivi hurudi katika lindi la umaskini. Tatizo liko wapi? Uliwafundisha wanao kula samaki badala ya kuwafundisha namna ya kuvua samaki. Mwanao akiwa na matumizi mabaya ya elfu kumi Mungu hawezi kumpa milioni moja maana anajua atateseka tu. Mfundishe mwanao kuwa na matumizi mazuri katika pesa kidogo anayoipata au aliyonayo ili baada akipata zaidi aweze kumudu hata hiyo pesa kubwa.



Hii ni blogu rasmi ya Edius Katamugora, hapa utajifunza maendeleo binafsi, utapata makala mbalimbali zinazohusu biashara, elimu, hamasa na maisha kwa ujumla. Karibu sana katika blogu hii.

0 comments: