Saturday, 1 April 2023

๐— ๐—•๐—œ๐—ก๐—จ ๐Ÿฐ ๐—ญ๐—” ๐—ž๐—จ๐—ช๐—”๐—™๐—”๐—ก๐—ฌ๐—” ๐—ช๐—”๐—ง๐—จ ๐—ช๐—”๐—ฉ๐—จ๐—ง๐—œ๐—ช๐—˜ ๐—ก๐—” ๐—ช๐—˜๐—ช๐—˜.

Kuna watu ukikutana nao siku ya kwanza tu kuna vitu unaviona kwao na wanakuvutia ndani ya muda mchache wa kukutana nao. Watu hawa si kwamba walishuka toka mbinguni kama Mungu alivyokuwa akiwashushia wana wa Israeli Manna, La hasha. 

Watu hawa kuna mbinu wamejifunza zinazowafanya watu wavutiwe nao. 

Zifuatazo ni mbinu zitakazokufanya uwe na ushawishi mkubwa kwa watu tofauti tofauti; 

1. Kumbuka majina ya watu.

Majina ya watu  yana maajabu mengi. "Sauti tamu kuliko zote duniani kwa watu si mziki mkubwa, bali ni majina yao." Alisema Les Giblin naye Dale Carnegie alikoleza akisema, "Majina ni sauti tamu na muhimu katika lugha yoyote duniani." 

Jaribu kukumbuka siku ulipokutana na mtu ambaye hukujua kama anakufahamu na ghafla akakuita kwa majina yako. Nafikiri ulifurahi sana na ulitaka kuwa na mazungumzo zaidi na huyo mtu. Huo ni mfano kidogo wa kuonesha majina yako yalivyo muhimu. 

Rafiki yangu mmoja aitwaye Iddi Amani Mwamwindi amekwenda mbali na kuweka kichwani majina matatu ya watu wote anaowafahau. Yaani akikutana na mimi ataniita Edius Jacob Katamugora. Huwa namshangaa sana lakini nami naendelea kujifunza. Binafsi nimejifunza kusevu jina zaidi ya moja kwenye simu yangu. Kuna aliyeona jina lefu nililosevu kwa simu yangu akashangaa nawezaje vile kuandika majina yote ya mtu. Ni kitu nimejifunza na napenda sana lakini pia kinabisaidia sana.

Majina ya watu ni muhimu ndiyo maana wengine wamejitengenezea majina yao(Brand) na wanatamani wajulikane kwa majina hayo na wanayalinda kwa nguvu kubwa. Msanii Bruno Mars aliwahi kusema, "Kila mtu huniita Bruno, hawaniiti Peter- hilo ni jina langu la serikali." 

Majina ya mtu ni kitambulisho, yanamtofautisha yeye na mwingine.  Hivyo kujua jina la mtu unamfanya ajisikie wa pekee. Ndiyo maana makapuni utengeneza baji zenye majina ya wafanyakazi wao. Tuzo hutolewa zikiwa na majina ya anayepewa tuzo hiyo. Hapo utaona majina yalivyo na umuhimu. 

Jitahidi kujua majina ya mtu na namna yanavyotamkwa. Hii itakuongezea sifa kubwa sana ukutanapo na mtu. Inaonesha upo makini kiasi gani. "Mwanzo wa hekima ni kuviita vitu kwa majina yake sahihi." Alisema Mwanafalsafa Confucius maelfu ya miaka iliyopita. 

Jitahidi sana kukumbuka majina ya watu. Hata kwenye mawasiliano ya simu waite watu kwa majina yao. Kuna tofauti kubwa kuandika au kutamka maneno haya, "Habari za asubuhi." Na "Habari za asubuhi Bw. Edius / Bi. Anna" tofauti ni kubwa kuliko unavyofikiri. 

Miaka ya nyuma Coca cola walikuwa na kampeni ya kutengeneza chupa zilizokuwa na majina ya watu, kampeni hii ilifanya vyema sana. Hata wewe unaweza kuona namna ya kuitumia kwenye biashara yako. Naamini utanipenda. 

2. Sikiliza kwa umakini

Kuwa msikilizaji mkubwa ni kipaji na ni ujuzi. Unaweza kunolewa. Watu wengi ni wazungumzaji na si wasikilizaji. Ajabu kubwa Mungu wakati wa uumbaji alipiga hesabu kali, akatupa mdomo mmoja na masikio mawili ili tuweze kuwa wasikilizaji sana na si wazungumzaji sana. 


Kuwa msikilizaji ni chanzo cha heshima. Mtu huona kwamba umempa heshima kubwa hivyo anatakiwa kurejesha heshima hiyo. 

Kuwa msikilizaji kuna faida kubwa. Kwanza unajifunza mengi. Kuwa mzungumzaji unatoa yale yote unayoyajua. Jikumbushe kila asubuhi kwamba hakuna chochote utakachosema leo kitakachokufunza lolote bali ukitaka kujifunza lazima usikilize. 

"Kama ukifanya kusikiliza na kuchunguza(kudadisi) kazi yako utapata faida kubwa kuliko utakavyoongea," alisema Robert Baden-Powell. Sikiliza ufanikiwe, sikiliza uendelee. "Watu wengi waliofanikiwa ninaowafahamu ni wale wanaosikiliza zaidi ya kuongea." 

Saikolojia inasema huwa tunapenda watu wanaotupenda. Kuwasikiliza watu ni kuwaonesha upendo juu ya maoni yao. Kukubali kupokea yale tu wanayosema lazima na wao wakukubali wewe. 

Leo jipe jukumu la kuwa msikilizaji sana kuliko kuongea. 

Nelson Mandela alipoulizwa ni kitu gani kikubwa alichojifunza kwenye uongozi alisema, "Kuwa mtu wa mwisho kuzungumza." Ujuzi huu alijifunza toka kwa babu yake. Ukiwa mtu wa mwisho kuzungumza maana yake umewapa watu wote nafasi ya kuzungumza na umewasikiliza vema. 

3. Weka pozi kidogo kabla ya kuwajibu watu.

Hata kama unajua majibu weka pozi kidogo katika kutoa majibu yako. Kitaalamu wanasema hesabu tatu (yaani moja, mbili, tatu) kisha toa majibu. 

Ukijipa pozi katika kutoa majibu unawaonesha watu kwamba maswali au kile walichokisema umekichakata kichwani na unatoa majibu mazuri. 

Ukitoa majibu fasta fasta inaonesha kwamba wewe unataka pointi zako zionekane zina mashiko zaidi kuliko zao. Ukifanya hivyo utakuwa umetoka relini na watu hawawezi kuuona umuhimu wako. 

4. Ongelea kuhusu wao

Bahati mbaya huwa tukikutana na watu tunapenda kujisemea ya kwetu, hii ni mbaya sana. Ni kama kujisifia. Hakuna mtu anaweza kushawishika na mtu anayependa sifa zaidi zaidi watakudharau. 

Unapokutana na watu pendelea kuwazungumzia wao kuliko kujizungumzia. 80% iwe kuhusu wao na 20% asilimia iwe kuhusu wewe. Tumia zaidi maneno "wewe" na "yako" na wala si "mimi" au "yangu." 

Ukifuata mbinu hizi nne ulizojifunza leo utakuwa mtu bomba saaaana linapokuja suala la kufahamiana na watu. Nakutakia yote yaliyo mema mpendwa. 

Wenu mtiifu, 

Edius Katamugora 

Kijana wa Maarifa

Hii ni blogu rasmi ya Edius Katamugora, hapa utajifunza maendeleo binafsi, utapata makala mbalimbali zinazohusu biashara, elimu, hamasa na maisha kwa ujumla. Karibu sana katika blogu hii.

0 comments: