Wednesday 28 March 2018

Mchango Wa Mzazi Kwa Mtoto Katika Kuutafuta Utaalamu II



#3: MCHUNGUZE MWANAO ANAPENDA NINI
   
Kila mzazi anao wajibu wa kuchunguza na kutizama mwanae anapenda kufanya nini. Mchunguze ni mambo gani anapendelea kuyafanya muda mwingi. Labda anapenda kulisha wanyama, huyu anaweza kuwa daktari wa wanyama, labda anapenda kufundisha wenzake, huyu anaweza kuwa mwalimu au profesa wa chuo kikuu, labda anapenda kuimba, huyu anaweza kuwa mwanamuziki, labda anapenda kushona, huyu anaweza kuwa fundi anayeshona mitindo mbalimbali, labda anapenda mambo ya ujenzi, huyu anaweza kuwa mhandisi wa ujenzi au msanifu majengo. Wahenga walisema, “Mahali moyo wako ulipolalia, ndipo miguu yako huamkia.” Kama mzazi una wajibu mkubwa wa kuchunguza mwanao anapenda kufanya mambo gani.
                            


#4: USIMLAZIMISHE MWANAO ASOME KITU ASICHOKIPENDA
    
Kuna wazazi wengi wameua watoto wao. Usishangae kusema hivyo lakini hapa namaanisha, kuna wazazi wengi wameua ndoto za watoto wao. Mtoto anataka kuwa mwalimu, mzazi anamlazimisha asome na kuwa mwanasheria. Hii ni hatari kubwa ambayo imesababisha dunia ikose wataalamu katika sekta mbalimbali. Ukimlazimisha mwanao asome kitu asichokipenda hata kidogo ni sawa na kumchukua samaki na kumleta nchi kavu, unategemea nini? Samaki huyo hawezi kuishi. “Mkono hata uwe mzuri namna gani kwako ni begani,” unatukumbusha msemo wa Kiswahili. Kuna watu wengi wanafanya kazi zisizo zao. Kadiri ya takwimu za mwaka 1987 Waamerika asilimia 24.3 hawana furaha kwa sababu walichagua kazi ambazo hazikupaswa kuwa kazi zao. Hii ni kutokana na kufanya kazi wasizozipenda. Kuishi maisha yasiyo na furaha ni msalaba mkubwa. Miaka ya hivi karibuni kiwango hicho kimeongezeka na kufikia asilimia 87. Wazazi wengi wamekuwa wakiwalazimisha watoto wao wasome kozi fulani kisa kozi hizo zina ajira kumbe wanafanya makosa makubwa. Nikukumbeshe wewe mzazi kuwa siku hizi kozi zote hazina ajira, karibu kila kozi kuna wahitimu wengi wapo mtaani ambao kila kukicha wamekuwa wakitafuta kazi ofisi hadi ofisi. Mwanao akisoma kozi anayoipenda ni rahisi hata kujiajiri. Kama hupendi kitu unachokisoma hata ile nguvu ya kusema nitajiajiri huwezi kuipata. Nchini Kenya kuna baba mmoja alimlazimisha mwanae asomee udaktari, kijana huyo hakutaka kukwazana na baba yake ingawa yeye hakupenda kuwa daktari alipenda kuwa muhasibu. Baada ya kusoma na kumaliza miaka mitano kijana huyo alitunukiwa shahada ya juu ya udaktari akiwa na daraja la kwanza (Upper Class). Yule kijana alipofika nyumbani kwao alimwambia baba yake maneno yafuatayo, “Baba, ulitaka nisome niwe daktari, vyeti vyako hivi hapa. Sasa narudi chuo kusoma kitu ninachokipenda.” Kijana huyo alirudi chuo kuanza kusomea uhasibu.
       
    Siku moja rafiki yangu Saada Mpandachalo aliwahi kuniambia maneno yafuatayo, “Kuna haja kubwa ya semina kwa wazazi wetu. Wengi tunatumbukia kwenye shimo la ndoto za familia kwasababu hatutaki kuonekana disobidients (wasio na adabu). Wakati mwingine dreamer (mwenye ndoto au muotaji) hapewi usingizi anaouhitaji, kila akitaka kuota anamwagiwa maji ya hofu ya laana. Tuangaze juu pia.”

Itaendelea...

Ndimi:
EDIUS KATAMUGORA
0764145476
ekatamugora@gmail.com

WEKA ODA KUPATA KITABU CHA NAMNA YA KUWA MTAALAMU UKIWA BADO UNASOMA KUPITIA 0764145476

Hii ni blogu rasmi ya Edius Katamugora, hapa utajifunza maendeleo binafsi, utapata makala mbalimbali zinazohusu biashara, elimu, hamasa na maisha kwa ujumla. Karibu sana katika blogu hii.

0 comments: