Saturday 21 November 2020

MAMBO 7 YA KUFANYA UNAPOPITIA KATIKA NYAKATI NGUMU

Kila unayekutana naye anapambana mapambano usiyoyajua wala kuyafahamu, karibia Kila mtu anayo mitihani au magumu anayoyapitia maishani. Ndiyo maana Mwandishi wa kitabu Cha "The Road less Travelled" M.Scott Peck, M.D alianza kwa kuandika katika kitabu chake maneno haya, "Maisha Ni magumu."


Naye Robert Schuller Mwandishi na mchungaji mashuhuri anasema, "Nyakati ngumu hazidumu, lakini watu wagumu hudumu,"


Je Kama Kila mtu anapitia katika nyakati ngumu, wengine wanawezaje kustahimili magumu ya nyakati ngumu au mikikimiki na mimi nishindwe? 


Inawezekana hilo ndilo swalo linalopita kichwani kwako.


Nyakati ngumu zimewafanya watu wachukue maamuzi magumu ambayo huwaacha watu midomo wazi. Kuna watu wamejiua kisa kupitia katika nyakati ngumu. Kuna wengine wameua ndoa au mahusiano yao kisa wanapitia katika nyakati ngumu.


Kuna wengine wameharibu biashara zao kisa wanapitia katika nyakati ngumu.


Niliwahi kuandika katika kitabu changu Cha Pumba za Edius kwamba, "Usione watu wanafurahia maisha kila uchao ukafikiri kwamba kila kitu kwenye maisha kipo sawa, hapana, kila mtu anao usiku wake wa giza."


Je nifanye nini ninapopitia katika kipindi kigumu?


Zifuatazo ni njia zinazoweza kukusaidia kuvuka katika kipindi kigumu;


1. Chunga mawazo yako.

Mara nyingi tumesikia ikisemwa, "Akili/ubongo wako ni kila kitu." Huu ni ukweli usiopingika. 


Sisi ni matokeo ya kile tunachofikiri. Hivyo unapopitia katika magumu chunga mawazo yako, acha Kusikiliza vitu vitakavyomaliza nguvu ndani yako.


Acha kuwa na mawazo hasi. Ikumbukwe kuwa mawazo ndiyo huzaa maneno, na maneno ndiyo huzaa matendo na kisha matendo ndiyo huzaa jinsi ulivyo.


Unaweza kuona sasa mawazo yanavyobadilika na kuleta matokeo ya tofauti.


2. Sali/Omba Mungu

Naupenda sana msemo wa Dkt. Benjamin Carson katika kitabu chake cha Think Big ambapo neno G katika BIG lilisimama katika maana ya Mungu yaani God, anasema, "Usiwe mkubwa zaidi ya Mungu."


Kufahamu kwamba kuna mtu mkubwa aliyekuumba na anayekufahamu toka ungali tumboni mwa mama yako ni jambo zuri sana kama ukimrudia yeye akurudie katika kipindi kigumu.


Ni muhimu sana pia kuwa mtu wa sala kila mara sio katika nyakati zile unazopitia magumu, sala zako unazoomba wakati hauna shida au magumu zinaweza kujibiwa wakati ukiwa na shida. Ndiyo maana Albert Eistein aliwahi kusema, "Mungu hachezi mchezo wa kubahatisha."


Sali kila wakati na kila Mara, usiifanye sala Kama spea ya tairi kwamba itaitajika tu pale gari linapopata pancha.


3. Omba ushauri kwa watu unaowaamini.


Tunaishi katika dunia ambayo kila gumu unalopitia Kuna watu wamelipitia na kuomba ushauri.


Baada ya kupitia magumu na kuomba ushauri kwa baadhi ya watu niliowaamini nilikuja kugundua kumbe na wao wana mifano ya watu waliopitia magumu zaidi ya yangu na wakaweza kuivuka bahari yao ya matatizo.


Hapo ndipo nilipowaza na kujisemea, "Kama wao wameweza kwanini mimi nisiweze." Mungu aliweka nguvu ndani yetu ya kufanya makubwa ndiyo maana toka tukiwa wadogo tukianguka tunasimama tena na hatubaki chini.


4. Tembelea maeneo tulivu.


Wanasayansi wanasema kutembelea maeneo tulivu na yaliyo na ukijani mwingi hupunguza msongo wa mawazo. 


Ukipitia katika magumu toka nje usijifungie ndani, upweke huongeza mawazo zaidi na unaweza kukufanya uchukue maamuzi magumu.


Unapotembelea maeneo yenye ukijani na hewa safi unaufanya ubongo wako uingize hewa safi inayoleta utulivu wa nafsi.


5. Sikiliza Podcast za Hamasa.


Hakuna muda mzuri wa Kusikiliza podcast za Hamasa Kama muda unapopitia katika magumu.


Kwenye podcast hizo huwa mara nyingi unakutana na watu waliokwisha pata magumu hata zaidi ya yako.


Lakini pia podcast hizo hukusaidia kuprogramu akili yako. Nakubaliana na mhamasishaji Les Brown aliyesema, "Usipopragramu akili yako, akili yako itaprogramiwa."


6. Soma Vitabu


Mojawapo ya faida ya Kusoma Vitabu ni kuondoa msongo wa mawazo. Wote wanaope da Kusoma Vitabu wanalifahamu ili.


Mfano Ukiwa katika nyakati ngumu na ukasoma kitabu Kama Hekaya za Abunuasi unajikuta baada ya kuwa na huzuni unacheka tu.


Watu walioishi na mimi wanajua vizuri tu. Kuna wakati huwa natoa tabasamu Kali huku nikiwa nasoma kitabu. Muda huo huwa nimekutana na jambo la kunifurahisha.


7. Usilalamike wakati wa magumu ni wakati wa kuona fursa.


Juzi tu nilikutana na maneno haya kwenye mtandao wa Twitter, "Malalamiko yako ni wazo zuri la biashara la mtu mwingine."


Waswahili husema, baada ya dhiki faraja. Matatizo ni fursa. Henry Ford baada ya kuunguliwa na kiwanda chake kilichokua na ukubwa wa zaidi ya viwanja 3 vya mpira alisema, "Makosa yetu yote yamechomwa." Baada ya wiki mbili aligundua kamera.


Unaweza kupitia nyakati ngumu na wewe ndiwe ukawa mtatuzi wa shida uliyokumbana nayo.


Aliyepitia katika ndoa yenye mikikimiki na hatimaye utulivu anaweza kuwa mshauri mzuri wa wale wanaopitia magumu katika ndoa.


Mwanafunzi anayefeli darasani na baadaye kuanza kufaulu anaweza kuwa mshauri mzuri wa wanafunzi wanaofelu darasani.


Hivi ndivyo alivyofanya Dkt. Ben Carson aliandika kitabu kiitwacho mikono itendayo maajabu, humo anaelezea maisha yake akionesha jinsi alivyokua mbovu darasani lakini baadae alifanikiwa kuwa nambari Moja na kuwa daktari mkubwa wa masuala ya ubongo.


Mwisho nimalize kwa kusema, nyakati ngumu ni za muda tu na si za kila siku wala saa. Bill Ocean aliwahi kuimba, "Pale mwendo unapokua mgumu, watu wagumu huendelea kusongambele." Utafute wimbo huo unaitwa, "When the going gets tough."


Ndimi:


Edius Katamugora

ekatamugora@gmail.com

0764145476

Hii ni blogu rasmi ya Edius Katamugora, hapa utajifunza maendeleo binafsi, utapata makala mbalimbali zinazohusu biashara, elimu, hamasa na maisha kwa ujumla. Karibu sana katika blogu hii.

0 comments: