Habari mpendwa msomaji wa Bideism blog. Ni matumaini yangu kwamba umefanikiwa kuuona mwezi mpya mwezi wa Novemba.
Leo hii ningependa nikushirikishe mambo 31 niliyojifunza mwezi ulioisha jana mwezi wa Oktoba.
Karibu tujifunze pamoja mtu wangu wa nguvu.
Mambo 31 Niliyojifunza Mwezi Oktoba:
1. Mvivu siku zote hakosi la kusema.
Lazima awe na sababu za kujitetea kwanini hajafanya kitu fulani au kwanini hawezi kufanya kitu fulani.
Lazima awe na sababu za kujitetea kwanini hajafanya kitu fulani au kwanini hawezi kufanya kitu fulani.
2. Jitahidi kutumia gharama zozote ujikutanishe na watu unaotamani kuwa kama wao watakwambia na utajifunza mambo mengi.
3. Mimea na wadudu ni vitu vinavyoweza kutoa mafunzo makubwa kwenye maisha yetu ya kila siku. Tunaweza kujifunza kwa wadudu kama sisimizi katika suala la kuweka akiba. Sisimizi ni chungu mweusi kama siafu. "Sisimizi hana kiongozi, ofsa, wala mtawala; lakini hujiwekea chakula wakati wa kiangazi, hujikusanyia akiba wakati wa mavuno" (Methali 6: 7-8).
4. Kila mtu anauwezo wa kuona kitu tofauti na mtu mwingine. Kila mtu anaweza kuona fursa kivyake.
"Fundi Seremala akiona mti anaona mbao nzuri ya kutengenezea samani nzuri sana za kuuza pale Keko Furnitures.
Ndege wao huona sehemu ya kutengeneza viota vya makazi na kutua.
Mwajuma anaona sehemu ya kupigia picha.
Mimi naona kivuli cha kupumzika kubadilisha mawazo na wenzangu.
Majuhudi, mganga wa mitishamba anaona dawa ya kutibu presha, sukari na magonjwa yasiyopungua saba.
Savai mwalimu wa Hisabati anaona fimbo nzuri zilizonyooka za kuwachapia wanafunzi wanaofanya vibaya kwenye somo lake.
Kaka yangu Godius anaona kurasa zisizopungua mbili za kwenye kitabu chake cha Kutoka Sifuri Hadi Kileleni akisema "Ukitaka kufanikiwa jifanye kama mti, refuka usiangalie miti mingine."
Raymond Mgeni naye anaona utenzi mzuri wa kuusifia mti."
5. Kila mtu anayekutana naye ni fursa. Jitahidi kuishi vizuri na watu na pia kutenda mema kwa kila mtu bila kubagua.
6. Mlango mmoja wa fursa ukifungwa mwingine unafunguliwa. Tatizo watu wengi hubaki kuyaweka macho yao kwenye mlango uliofungwa.
7. Kisichokuua kinakukomaza. Saikolojia inasema "kufanya kazi ambazo unaziona ngumu kunakufanya ukue."
8. Ukipata muda wa kufanya kitu fulani hakikisha unakifanya kwa ufanisi wa ari ya juu kwani muda haurudi nyuma.
9. Kufanya kazi kwa bidii na juhudi kunalipa. Juhudi haijawahi kumuangusha mtu.
10. Tembea na kalamu na notibuku muda wote ili uandike yale unayojifunza na matumizi yako ya pesa na kadhalika, kwani kichwa chako hakiwezi kukumbuka kila kitu. Kocha akitoa kadi ya njano au nyekundu kwa mchezaji anaandika kwenye kadi zake, ingawa mpira huchezwa ndani ya dakika 90.
11. Kuna furaha katika kutoa. Kutoa ni moyo vidole huachia.
12. Jifunze kusamehe kila siku kabla ya kulala. Chuki humchoma anayeitunza na sio anayechukiwa.
13. Kabla haujamhukumu mtu jifanye wewe ni yeye. Vaa viatu vyake. Hii itakusaidia kutoa hukumu sahihi.
14. Kila mtu amezaliwa kuwa kiongozi na kila kiongozi lazima awe msomaji. Mwalimu Julius K Nyerere aliacha maktaba yenye vitabu zaidi ya elfu nane (8000).
15. Uoga wa kuongea mbele za watu ni kitu kinachowasumbua watu wengi, lakini kuongea mbele za watu ni ujuzi unaoweza kufundishika. Ukweli ni kwamba unaweza kujifunza kila kitu kama ukiamua na kujitoa. Kama wengine wameweza kwanini wewe usiweze?
16. Kuwa mjasiriamali sio kitu rahisi. Kama kingelikuwa kitu rahisi kila mtu anageweza kuwa mjasiriamali.
17. Watu wengi hupenda kusikia wanayotaka kuyasikia lakini hawasikilizi. Jifunze kusikiliza.
18. Kama una kipaji flani hakikisha kila siku haipiti bila kufanyia kazi kipaji chako.
Kipaji chako kinahitaji mazoezi ya kutosha kwani kinamahusiano makubwa na utendaji wa ubongo wako. Jinsi unavyofanya kila siku ndivyo unavyoweza kuendeleza kipaji chako.
Kipaji chako kinahitaji mazoezi ya kutosha kwani kinamahusiano makubwa na utendaji wa ubongo wako. Jinsi unavyofanya kila siku ndivyo unavyoweza kuendeleza kipaji chako.
19. Maisha yakikupa limau. Tengeneza juisi uuze. Somo: usibaki kuwa mlalamikaji bali kuwa mtatuzi. Dunia inawatatuzi wachache, itakulipa endapo utakubali kuwa mtatuzi.
20. Mazoezi ya mwili uufanya mwili kuwa na afya nje na pia akili kufanya kazi kwa uwezo wa hali ya juu. Wataalamu ushauri mtu kufanya mazoezi ya mwili kwa muda usiopungua dakika 200 kila wiki ambazo ni sawa na nusu saa kila siku iitwayo Leo.
21. Mungu akikupa mzigo anakupa mabega ya kuubebea. Tatizo maana yake ni suluhisho.
22. Kama rafiki yako anamiliki biashara mpe muunge mkono kwa kununua bidhaa zake na sio kuomba akupe bure kila mara.
23. Ukisema "Siwezi kufanya kitu fulani."
Akili yako huacha kufanya kazi.
Akili yako huacha kufanya kazi.
Ukisema "Nitawezaje kufanya kitu fulani?"
Akili yako huanza kufanya kazi.
Akili yako huanza kufanya kazi.
24. Ukitambua yakwamba watu huwasahau marehemu mapema, utaacha kuishi maisha ya kuigiza na kumfurahisha kila mtu. Kuwa wewe na Fanya mambo yanayokupa furaha.
25. Usiache kufanya kile unachokifanya hata kama watu hawakuungi mkono kwa kile unachokifanya. Kila mtu aliyefanikiwa alipita katika hali hii.
26. Wateja ambao hawana furaha ni sehemu kubwa na nzuri ya kujifunza.
27. Jitahidi kubadilika kutoka na na mabadiliko ya teknolojia. Dunia ya Leo inabadilika kwa kasi ya ajabu sana.
28. Huduma nzuri unayoitoa kwenye biashara yako ni tangazo tosha kuliko hata matangazo ya kwenye magazeti, redio na televisheni.
"Kanuni ya Girard ya 250"
Watu wengi hupenda kuwaambia wenzao kuhusu biashara au malengo yao. Kumbe unapomuuzia mtu kitu unawauzia marafiki zake pia, ndugu na jamaa.
Jeo Girard anaamini kwamba "Kila mtu anao marafiki 250 anaowafahamu ambao anaweza kuwaakaribisha kwenye sherehe au msiba." Kumbe unapomuuzia mtu mmoja kitu kibaya anaweza kuwaambia marafiki zake 250 kuhusu bidhaa yako mbaya au huduma yako mbovu.
Kwa mwaka mzima watu 13000 wanakuwa wameambiwa kuhusu biashara yako hivyo kuharibu biashara yako.
Kumbuka watu 250 ni kadrio la chini kabisa ukilinganisha na watu wanaotumia mitandao ya kijamii kama Facebook, Instagram na WhatsApp.
Funzo
Unapofanya biashara yako hakikisha kila mteja unamtendea haki kwa kumpa huduma bora.
Unapofanya biashara yako hakikisha kila mteja unamtendea haki kwa kumpa huduma bora.
Unapofanya biashara yako unafanya biashara na watu wengine 250 ambao huwaoni. Kumbuka ni rahisi watu kutangaza ubovu wa biashara au huduma yako kuliko kutangaza uzuri wa biashara unayoifanya.
Ukimpoteza mteja mmoja umewapoteza wateja 13000 kwa mwaka.
29. Andika malengo yako na hakikisha kila siku unayasoma Mara 3 na zaidi kila siku. Hii itakupa motisha ya kufanya kazi kwa juhudi ili kuhakikisha unayatimiza.
30. Usiudharau umri wako hata siku moja, kuwa na umri mdogo ni fursa tosha na kuwa na umri mkubwa sio kigezo cha kutofanikiwa. Colonel Sanders mwanzilishi wa Kentucky Fried Chicken (KFC) alianza akiwa na miaka 65 .
31. Ukipata muda wa kuwafundisha na kutoa maelezo kwa wengine Fanya hivyo. Hiyo ni mbegu bora unapanda.
Asante kwa kuwa nami mwanzo hadi mwisho wa nakala hii. Ni matumaini yangu umejifunza mengi na litakuwa jambo jema ukiwashirikisha marafiki zako.
"Mafanikio yako, mikononi mwako."
Ndimi
Edius Katamugora
Mwandishi na Mhamasishaji.
0764145476
0625951842 (WhatsApp)
Email: ekatamugora@gmail.com
Instagram: ediuskatamugora
Edius Katamugora
Mwandishi na Mhamasishaji.
0764145476
0625951842 (WhatsApp)
Email: ekatamugora@gmail.com
Instagram: ediuskatamugora
1 comments:
Nzuri kaka! nimekusoma. Thanks
Post a Comment