Lengo kubwa la biashara yoyote au ujasiriamali wowote unaofanyika ni kupata faida ya kipato hasa hela.
Hata kama ni kampuni inayotoa huduma Fulani lengo lake kubwa ni kujiingizia pesa kama faida ya uendeshaji wa huduma inayotoa kampuni husika.
Kama mkulima anavyoanza kuliandaa shamba lake kabla ya kuanza kilimo au mchezaji anavyoanza kufanya mazoezi kabla ya siku ya mechi. Mfanyabiashara au mjasiriamali Kuna vitu ambavyo anavihitaji kabla ya kuingia kwenye biashara yoyote.
Vitu hivyo viwili ni kama vifuatavyo.
1. Mawasiliano (uwezo wa kuwasiliana/ability to communicate).
Mawasiliano ni kitu muhimu sana kwa mtu anayetaka kuanza kufanya biashara au ujasiriamali. Uwezo wa mtu kuwasiliana ndio humfanya aweze kuuza bidhaa yake na ikubalike kwa watu.
Katika dunia ya Leo kama uwezo wako wa kuwasiliana au kuongea na watu ni mdogo ni wazi bidhaa yako itashindwa kuuzika.
Jinsi unavyoweza kuwasiliana na watu ndivyo unavyoweza kujiingizia kipato. Ukitaka kujipima uwezo wako wa kuwasiliana ni wa kiasi gani ingia kwenye chumba ambacho hujuani na mtu yeyote na ukiweza kuuza kitu chako hapo utakuwa una uwezo wa kuuza chochote.
Katika karne ya ishirini na moja mawasiliano ni kitu muhimu sana ndiyo maana hata katika kuomba kazi yoyote kigezo kimojawapo siku hizi ni ujuzi wa kuwasiliana (communication skills).
Mhamasishaji wa Kimarekani Les Brown aliwahi kusema "Unavyofumbua kinywa chako, unaiambia dunia wewe ni nani." Kumbe jinsi unavyowasiliana na watu katika mazingira ya kawaida itakusaidia utakapo anza biashara au ujasiriamali.
Mojawapo ya vitu ambavyo watu wengi huomba niawasaidie ni namna ya kuondoa hofu ya jinsi ya kuongea na watu. Watu wengi huofia kuongea mbele za watu, hili ni tatizo kubwa kwa mtu yeyote mwenye ndoto ya kufanya biashara au ujasiriamali.
Utawezaje kuondoa hofu ya kuongea mbele ya watu?
Uwezo wa kuongea na watu ni kitu ambacho mtu yeyote anaweza kujifunza. Hivyo usiwe na hofu kwamba uoga wako hauwezi kuisha.
1. Anza kuongea mbele ya vikundi vidogo vidogo. Sio rahisi mtu kuongea kwenye kundi kubwa kama huwezi kuongea kwenye kundi dogo la hata watu watano. Wachina wanasema "Safari ya maili elfu moja huanza na hatua moja."
Popote unapokuwa na kundi dogo kama la marafiki zako wakichangia hoja Fulani hakikisha na wewe unachangia hoja hiyo tena ukiwaangalia machoni. Marafiki ni watu ambao umewazoea hivyo kwako hofu itakuwa ndogo. Tabia mpya hujengwa ndani ya siku 30, hivyo ukiweza kujijengea uwezo wa kuongea mbele ya rafiki zako utakuwa kwenye hatua nzuri.
2. Ongea na kioo.
Kila siku unapoamka asubuhi au muda wowote nenda mbele ya kioo na ongea maneno yoyote huku ukijitazama kwenye kioo. Hii ni njia ya ajabu yenye matokeo chanya kwa watu wenye hofu za kuongea mbele ya watu.
3. Tafuta nafasi ya kuongea popote.
Inapotokea nafasi ya kuongea kwenye kikundi chochote hakikisha unashiriki. Kama ni mwanafunzi hakikisha kwenye presentation unakuwa nambari moja. Kama ni mtu wa kawaida kwenye shughuli za mtaani hakikisha unashiriki ipasavyo. Unaweza hata kushirikisha watu kusoma neno la Mungu kwenye nyumba za ibada. Hii itakuondolea hofu ya kuongea mbele za watu.
2. Ujuzi wa kuuza (Selling Skill)
Lengo kubwa la ujasiriamali au biashara yoyote ni kuuza kama nilivyotangulia kusema. Uwezo wa kuuza vitu ndiyo utakufanya uingize kipato na biashara yako ikue.
Kuuza pia ni ujuzi unaofundishika na watu wengi waliofanikiwa kwenye biashara yoyote ni watu waliojifunza mauzo huko nyuma. Unaweza kuona mtu Fulani anauza kitu Fulani ukumchukulia Poa lakini siku ukikuta anamiliki biashara kubwa usishangae.
Tunapoanza mapema kujifunza kuuza tunajenga kitu kinachoitwa hofu ya kukataliwa (fear of rejection). Yaani uende kuuza bidhaa yako watu waikatae hapo utajifunza vitu vingi. Ndiyo maana nimeanza na kusema mawasiliano ni kitu cha kwanza muhimu.
Leo hii kama una ndoto za kufanya biashara yoyote kubwa tafuta kitu chochote cha kuuza na uanze kufanya hivyo Mara moja. Hii itakusaidia kuondoa hofu ya kukataliwa na watu (fear of rejection). Kama hauna chochote cha kuuza msaidie hata mwenzako anayefanya biashara kutangaza na kuuza biashara yake. Nakwambia ukifanya hivyo mapema siku utakapo anza biashara yako kwako utakuwa rahisi na naamini utanipenda.
Aliko Dangote tajiri namba moja Afrika yeye akiwa bado mdogo alikuwa akinunua mfuko wa pipi na kwenda kuuza mojamoja akiwa shule ya msingi. Leo hii ni mfanyabiashara mkubwa.
Warren Buffet tajiri namba tatu duniani na mwekezaji namba moja duniani yeye akiwa darasa la pili alizoea kwenda kuuza pipi mlango hadi mlango. Huku pipi iliyokuwa ikipendwa sana ndiyo akiifanyia biashara zaidi.
Salim Bakhresa yeye akiwa na umri wa miaka 16 alianza kuuza kwenye mgahawa huko Zanzibar. Leo hii anaviwanda vinavyouza bidhaa zake Afrika Mashariki na Kati. Huyu ndiye mmiliki wa bidhaa za Azam.
Jifunze kuuza itakusaidia. Anza mapema kujifunza kuuza. Hakikisha pia uwezo wako wa kuwasiliana ni wa hali ya juu.
Imani yangu mafanikio ni kitu cha kushirikishana. Washirikishe na wenzako kitu ulichojifunza.
Ndimi
Edius Katamugora
Mwandishi na Mhamasishaji.
0764145476
0625951842 (WhatsApp)
ekatamugora@gmail.com
Karibu kujipatia kitabu cha Barabara Ya Mafanikio, bei ni shilingi 6000/=.
0 comments:
Post a Comment