Wednesday, 29 November 2017

Ukitaka Kuacha Kumbuka Kwanini Ulianza

Wakati kampuni ya Coca Cola inaanza iliuza chupa 3 tu za soda ndani mwaka mzima!

Najua umeshangaa maneno niliyoanza nayo hapo juu lakini hiyo ni historia ya kweli.

Leo hii Coca Cola ipo kila mahali. Ni kampuni ambayo imeweza kudumu kwa muda mrefu ukilinganisha na kampuni nyingine duniani tangu kuanzishwa kwake katika karne ya 19, Leo hii tupo karne ya Ishirini na moja.

Leo hii Coca Cola inakadiliwa kuuza chupa za vinywaji zaidi ya bilioni 1.7. Na imefika katika nchi zaidi ya 200 duniani. Kila mtu anaifahamu Coca Cola, karibia kila kona ukipita utakutana na bango la Coca Cola, kwenye Televisheni, kutaja machache. Inawezakana hata wewe Leo hii imejiwekea lengo la kupata mlo wako wa mchana ukishushia na Coke baridiii.

Bofya hapa kujipakulia Application ya blog yetu bure: BIDEISMBLOG

Tujifunze nini kutoka kwa Coca Cola?

Kitu cha kwanza na cha msingi ambacho inatupasa kujifunza hapa ni Ukitaka Kuacha Kumbuka Kwanini Ulianza.
Watu wengi wanakuwa na ndoto kubwa wanapoanza kufanya kitu Fulani, mfano biashara, kazi flani, anasomea kitu fulani lakini baadaye ndoto zao huyeyuka kama mshumaa. Malengo yao yamepotea.

              

Ulipokuwa unaanza ulikuwa na sababu milioni za kufanikiwa lakini Leo hii unaona milima tu. Hebu rudi nyuma tizama zile sababu zilizokusukuma kuanza kufanya kile unachokifanya. Ingawa huoni kama umepiga hatua inakupasa ukomae na usikate tamaa. Safari ya kuanza na chupa 3 ndani ya mwaka mzima kwa Coca Cola hadi kufikia chupa bilioni 1.7 kwa siku iwe fundisho kubwa kwako.

Inawezekana mwaka 2017 uliona mwaka wa neema kwako lakini hadi Leo hii unaona balaa tupu. Ngoja nikwambie rafiki yangu mwezi uliobaki unaweza kuwa mwezi wenye maajabu makubwa sana kwako kama hautaamua kukata tamaa. Kama utaweka nguvu na jitihada.

Nakubaliana na King Martin Luther Jr, aliyewahi kusema "Ukishindwa kukimbia, tembea. Ukishindwa kutembea, tambaa. Katika kila unachokifanya hakikisha unapiga hatua fulani."

Pili: Jifunze kutokana na kushindwa.
Kuna somo kubwa katika kushindwa. Lakini somo hili wanalielewa wale tu wenye mtizamo chanya. Ukishindwa rudi nyuma angalia ulikosea wapi na urekebishe makosa. Watu waliofanikiwa wanasifa moja ya kuwa vigan'ganizi hawajawahi kukubali kushindwa, Thomas Edson alishindwa kutengeneza balbu ya umeme zaidi ya Mara 1000 lakini hatimaye alifanikiwa na Leo hii anaitwa Baba wa Umeme duniani. Je wewe umeshindwa mara ngapi na kujiona hufai na umekata tamaa, inawezekana mara moja.

Tatu: Wakati mambo yanapokuwa magumu ndio wakati inakupasa wewe kusimama imara. Robert Schuller, mchungaji na mwandishi mashuhuri wa vitabu aliwahi kusema, "Nyakati ngumu hazidumu, lakini watu wagumu hudumu." Hivyo unahitaji kupiga moyo konde na kuendelea na kile unachokifanya.

Wakati kama huu ndipo utakapokutana na maneno mengi ya kukurudisha nyuma. Watu watakutukana na kukwambia "Tulikwambia jambo hilo haliwezekani." Lakini mimi nakwambia "Jambo hilo linawezekana."

Kumbuka Nuhu alijenga safina ndani ya miaka 120 bila kuona hata tone la mvua. Watu waliokaa naye karibu walimcheka na kumkebehi wakimwona mpumbavu wa kutupwa. Kipindi hicho mvua hata zilikua hazinyeshi kwani Mungu alikuwa akimwagilia mimea na maji yaliyotoka chini ya ardhi yakipanda juu. Nuhu aliishi mamia ya maili kutoka bahari ilipokuwa (Inawezekana hakuwahi kuiona bahari) lakini akukata tamaa alikuwa mtu mwenye msimamo na hatimaye aliweza kuimaliza safina. Watoto wake pia walimshangaa wakiona baba yao kama anapiga ngoma kwenye maji wakisema "Baba anatengeneza kitu gani miaka 120 hata tone la mvua hatujawahi kuliona!."

Coca Cola iwe fundisho kubwa kwetu.

Ukitaka Kuacha, Kumbuka Kwanini Ulianza.

Mafanikio yako mikononi mwako.

Ndimi:
Edius Katamugora
Mwandishi na Mhamasishaji.
0764145476
0625951842 (WhatsApp)
Email: ekatamugora@gmail.com

Jipatie kitabu cha Barabara Ya Mafanikio kwa shilingi 6000/= tu.

TANGAZO:
Unaweza kupata application ya blog hii toka play store kwa kuipakua bure kabisa. Ingia Play Store na tafuta Bideismblog

Hii ni blogu rasmi ya Edius Katamugora, hapa utajifunza maendeleo binafsi, utapata makala mbalimbali zinazohusu biashara, elimu, hamasa na maisha kwa ujumla. Karibu sana katika blogu hii.

0 comments: