Tuesday 10 April 2018

KANUNI YA MASAA ELFU KUMI (10000)




Wataalamu wa mambo ya Neva na ubongo wanasema ili mtu awe mtaalamu anahitaji masaa 10000 ili aweze kubobea katika fani fulani.

                               



Kama ni mwandishi, mwanamuziki, mwanamitindo, mchezaji, mwanafikia, mshereheshaji, mwanamahesabu, mkemia hata jambazi sugu unahitaji masaa 10000 ili uwe umebobea katika kitu unachokifanya.

Ukichukua masaa matatu kila siku kufanya kitu unachotaka uwe mtaalamu wacho tuseme uchoraji utahitaji jumla ya miaka tisa ili kuwa mtaalamu katika fani ya uchoraji. Hivyo kadri unavyotumia muda mwingi kujifunza kitu ambacho siku za mbeleni unahitaji kutumia muda mwingi kukifanyia mazoezi.

Daktari na mtaalamu wa mambo ya neva na ubongo (Neorologist) bwana Daniel Levitin anasema, “Picha inayojitokeza ya uchunguzi inaonesha kwamba masaa elfu kumi yanahitajika ili mtu awe mtaalamu. Baada ya kufanya chunguzi mbalimbali kwa watunzi, wacheza mpira wa kikapu, waandishi, wanamuziki, wacheza vinanda majukwaani, wacheza bao, majambazi na hata unachokifanya wewe, namba hii hujirudia mara nyingi. Hii haimaanishi kwamba wengine wanafanya mazoezi na kufanikiwa zaidi ya wengine. Lakini tumekuta kwamba hakuna aliyewahi kuwa mtaalamu chini ya masaa tajwa hapo juu. Inaonekana kwamba inachukua ubongo kwa muda mrefu kuifanya yote ambayo inahitajika kufikia ujuzi wa kweli.”

Mwaka 1971 kwa muda wa miezi saba Bill Gates pamoja na marafiki zake  walitumia masaa karibia 1,575 kwenye kujifunza kompyuta ambayo inakadiriwa kuwa masaa nane kila siku ndani ya siku saba (wiki moja). Muda mwingine walitumia hadi masaa ishirini au thelathini siku za wikiendi. Kuna wakati rafiki yake Paul Allen aliyezaliwa Januari 21, 1953, ambaye ni mshirika wake katika kuanzisha kampuni ya Microsoft alipata nafasi ya kutumia kompyuta za chuo cha Washington, ingawa kompyuta hizo zilitumika muda mwingi masaa ishirini na nne. Waligundua kwamba kompyuta hizo zilikuwa zipo wazi kuanzia saa tisa usiku hadi saa kumi na mbili asubuhi. Hivyo Bill Gates anasema ilimpasa kuamka saa tisa usiku kwenda kwa mguu au kwa basi ili akajifunze mambo ya kompyuta. Kutoka akiwa darasa la nane hadi anaacha chuo cha Havard kwa miaka saba mfululizo Bill Gates alikuwa akijifunza kompyuta. Ambayo miaka saba ni tayari Zaidi ya masaa 10000.
Wewe pia kama kweli una nia ya kuwa mtaalamu wa kitengo au fani Fulani unahitaji kutumia muda wako mwingi kujifunza kitu ambacho unawiwa kuwa mtaalamu.

Lengo la kuandika kitabu cha Namna ya Kuwa Mtaalamu Ukiwa Bado Unasoma ni kukutaka wewe uanze mapema kufanyia kazi kitu ambacho siku za mbele natamani kuona ukiitwa mtaalamu wa kitu hicho. Siri pekee ni kuweka jitihada na kutumia muda mwingi kujifunza. Kama ukiamua unaweza. Anza leo sasa kutumia kila muda unaopata kujifunza. Kadri unavyotumia muda kidogo ndivyo utakavyotumia muda mwingi kuufikia utaalamu.

Ukitaka kuwa 1% lazima ufanye kile ambacho 99% hawakifanyi. “Ni muhimu sana kufanya kazi kwa bidii na juhudi. Usiwahi kutazama njia za mkato. Kuna masaa 24 ndani ya siku moja. Kama ukilala masaa 6 kwa  siku, una masaa  18 yaliyosalia. Watu wengi hufanya kazi masaa 8 au kumi. Hivyo sasa una bado masaa 8 yaliyosalia, tunafanya nini na  hayo masaa 8 ndilo swali lenyewe,” anasema Arnold Schwarzenegger.

Yale maneno ya “Dah, jamaa nimesoma nae tena tulikuwa tunakaa dawati moja lakini leo sio size yetu.” “Alianza kama mzaa, lakini leo yuko mbali mno.”
“Dah alikuwa mshikaji wangu mimi nilikua namchukulia poa tu.” Kutaja machache. Hayaji hivi hivi bila wewe kuendelea kupambana na kuhakikisha unatimiza ndoto zako. Usichoke mtu wangu wa nguvu.

Usisahau kupakua APP yetu kupitia sehemu iliyoandikwa DOWNLOAD OUR APP FOR FREE chini kabisa ya ukurasa huu.

"Mafanikio yako mikononi mwako."

Ndimi:
EDIUS KATAMUGORA
Mwandishi na mhamasishaji
0758594893
ekatamugora@gmail.com

Usisahau kuwashirikisha wengine makala hii.  

Hii ni blogu rasmi ya Edius Katamugora, hapa utajifunza maendeleo binafsi, utapata makala mbalimbali zinazohusu biashara, elimu, hamasa na maisha kwa ujumla. Karibu sana katika blogu hii.

0 comments: