Siku moja wakati nimeandika makala katika gazeti la Jamhuri linalotoka kila siku za Jumanne kila wiki mtu mmoja alinitumia ujumbe ufuatao, "Habari Edius naomba unishauri nifanye biashara gani, nina mtaji wa shilingi milioni mbili, nimewaza hapa hadi kichwa kinaumwa sijui nifanye nini."
Kwanza kabisa ni wazi kuwa watu wengi wana nia na wanatamani kuwa wafanyabiashara na wajasiriamali wakubwa lakini bado hawajajua wafanye nini. Kama wewe ni mmojawapo makala hii imeandikwa makusudi kwako.
Kuna njia nyingi za kupata wazo la biashara hapa nimeamua kukuandikia njia chache.
Njia za kupata wazo la Biashara:
1. Tatua matatizo yaliyo katika jamii zako
Biashara yoyote kubwa huwa imelenga kutatua tatizo. Wanaoendesha bajaji na bodaboda wamelenga kutatua kero ya usafiri mtaani kwenu, anayeuza chakula amelenga kutatua tatizo la njaa, hauwezi kukwepa kula.
Bahati nzuri au mbaya Afrika ni bara lililojaa matatizo, watu wengi wa nje wanakimbilika kuwekeza kwenye bara hili kwasababu wanaona matatizo lukuki. Je umewahi kufikiria ni matatizo gani yanayoikabili jamii yako ambayo unaweza kuyatatua.
Andrew Mupuya pichani ni kijana toka nchini Uganda ambaye hutengeneza bahasha mbalimbali kwa ajili ya kubebea mizigo mbalimbali ambazo hutumika sokoni, kwenye supermarkets na kwenye maduka ya madawa (famasi).
Baada ya serikali ya Uganda kukataza matumizi ya mifuko ya plastiki Andrew aliona fursa kubwa katika kutengeneza bahasha za karatasi ili kutatua tatizo lililokuwepo. Narudia tena, Afrika imejaa matatizo na inahitaji wajasiriamali watakaoweza kujitokeza na kutatua matatizo hayo.
Wiki iliyopita rafiki yangu Charles Anyomi toka nchini Ghana alinipa habari jinsi alivyoanzisha biashara ya mgahawa. Anasema siku moja alikwenda hospitali, alipofika hapo hospitali alihitaji kula kitu chochote lakini cha kushangaza mahali pale hapakuwa na huduma yoyote ya chakula. Hiyo akaona anaweza kuanzisha mgahawa katika hospitali ile. Aliona tatizo na kuona ni kwa namna gani anaweza kulitatua na akapata pesa. Alikwenda na kuuona uongozi wa juu wa mahali pale na kisha wakampa eneo la kufanya biashara yake. Anasema hadi sasa biashara hiyo inamlipa sana.
2. Kutokana na vitu unavyopenda kuvifanya.
Umewahi kujiuliza kwamba mambo unayopenda kuyafanya unaweza kuyageuza na kuwa wazo la biashara.
Mfano unapenda sana kupika, unaweza kuanzisha hoteli kubwa yenye kutoa huduma nzuri na vyakula vya hadhi. Mimi napenda kuandika, hivyo nimeamua kuyabadili maandishi yangu kuwa biashara, ninaandika vitabu, makala katika magazeti, natoa semina, hivyo vyote vinaniingizia pesa.
Kaa chini na tafakari ni mambo gani unapenda kuyafanya ambayo unaweza kuyabadili kuwa biashara yenye mafanikio, Je unapenda kushona? Au unapenda kuimba, au unapenda kupamba, badili leo mambo unayoyapenda yawe biashara yako.
Marie Mukagahima ni binti aliyekulia katika jamii ya wakulima. Katika kukua kwake alipenda sana kilimo. Leo hii inamiliki kampuni yake inayotengeneza mikate ya unga wa maboga, anatengeneza mafuta kutokana na mbegu za maboga na vitu vingi vinavyotokana na maboga.
Itaendelea...
Edius Katamugora
(Kijana wa Maarifa)
0764145476
ekatamugora@gmail.com
Monday, 11 March 2019
Edius Katamugora
Hii ni blogu rasmi ya Edius Katamugora, hapa utajifunza maendeleo binafsi, utapata makala mbalimbali zinazohusu biashara, elimu, hamasa na maisha kwa ujumla. Karibu sana katika blogu hii.
1 comments:
Brother umenifumbua ubongo vizur sana mm napenda sana kunywa kahawa kwa siku naweza kunywa hata vikombe 15au zaid.... sasa nimepata wazo zuri ambapo nikilifanyia kazi Mungu ataweka wepes mie ni mfanya kazi katk sheli fulni hapa nchini hua naona madereva wa maroli wanavyohangaila kutafuta kahawa na sigara nitafany mpngo hvi karibuni kufungua kijiwe cha kahawa hp maeneo ya sheli naamin nifanikiwa kwa uwezo wa Mungu ahsant sana kwa funzo lako zuri Mungu atakulipa kaka
Post a Comment