Thursday 7 May 2020

ELIMIKA NA EDIUS (6)

ELIMIKA NA EDIUS (6)

Mfahamu John Stephen Akhwari Mwanariadha Maarufu Toka Tanzania
__________________________________________________

Ukiambiwa utaje wanamichezo waliowahi kuipaisha Tanzania duniani sina shaka utawataja kina Samatta, Hasheem Thabit na Mwakinyo. Sasa ngoja nikwambie kuna mtu na maarufu kuwashinda hawa, yaani kwa umaarufu Samatta akasome.

Anaitwa John Stephen Akhwari.

Mgunduzi wa mtandao wa Facebook Bwana Mark Zuckerburg anasema, "Dunia inabadilishwa na watu wenye nia." Watu wenye kiu na msukumo wa ndani ndio waliofanya mambo yanayoiacha dunia mdomo wazi.

Jumapili ya tarehe 20, mwezi Oktoba mwaka 1968 nchini Mexico yalikuwa yakifanyika mashindano ya Olympic. Tanzania iliwakilishwa na mwanariadha John Stephen Akhwari. Mbio za mile 26 (Km 42) zilianza kukimbiwa mnamo saa 9 mchana hivi, siku hiyo ilikuwa siku ya jua Kali.

Katikati ya mbio Akhwari alianguka na aliumia mguu hasa maeneo ya goti na bega (hiyo ilitokana na jografia ya nchi ya Mexico ambayo imejaa milima Akhwari hakuwahi kukimbia katika maeneo ya milimani) Hivyo hakuweza kuendelea na mbio. Alipelekwa pembeni na kufungwa bandeji mguuni, sehemu ya goti.

 Saa limoja baada ya mtu wa kwanza kupita katika mstari wa ushindi (Huyu alikuwa raia wa Ethiopia Moma Wolde) huku baadhi ya watazamaji wakiwa wamekwisha ondoka uwanjani lilitokea tukio moja la ajabu sana.

John Stephen Akhwari alionekana akirudi uwanjani kuendelea na mbio. Hapo ulikuwa muda wa saa moja jioni. Hatimaye John Stephen Akhwari aliweza kumaliza mwendo wake wa maili 26 (Km 42) ingawa alikuwa mtu wa mwisho. Siku hiyo wakimbiaji walikuwa 79, 17 kati yao hawakuweza kumaliza mbio akiwemo Bikila mkimbiaji toka Ethiopia aliyekuwa amechukua tuzo Olympic iliyopita. Baada ya kufanya tukio hilo la kushangaza, waandishi wa habari walimzunguka na kumuuliza kwanini aliendelea na mbio ili hali mtu wa kwanza alikwisha pita kwenye mstari wa ushindi saa moja lililopita. Stephen Akhwari aliwajibu waandishi,

"Sikutumwa na nchi yangu maili 5000 kutoka hapa, kuanza mbio, nilitumwa kumaliza mbio."

Leo hii kauli hiyo Imempa jina kubwa John Stephen Akhwari pamoja na maumivu makali aliyoyapitia lakini alionekana mshindi. Wanamichezo wengi duniani wamekuwa wakifundishwa kutokana na kauli ya Akhwari.

Funzo: Maliza Mbio zako.
#ElimikaNaEdius
💎Mwisho✍🏽
Sponsored by Jgraphics.

Edius Katamugora
Content Creator
Creative Writer
0764145476
ekatamugora@gmail.com

Hii ni blogu rasmi ya Edius Katamugora, hapa utajifunza maendeleo binafsi, utapata makala mbalimbali zinazohusu biashara, elimu, hamasa na maisha kwa ujumla. Karibu sana katika blogu hii.

0 comments: