Tuesday, 12 May 2020

ELIMIKA NA EDIUS (8)

ELIMIKA NA EDIUS (8)

Mfahamu Tina Turner Staa wa Muziki Aliyepitia Manyanyaso Katika Ndoa, Leo anaishi Maisha Safi akiwa na Miaka 80.
____________________________________________________

#ElimikaNaEdius
Nyuma ya mteremko kuna mlima, na nyuma ya tabasamu kuna sononeko, taabu, misukosuko,sikitiko, huzuni,maisha magumu kutaja machache.

Hayo ni maneno ambayo yanafaa kutoa picha ya maisha halisi ya bidada Staa wa muziki wa Roll & Rock -Tina Tunner.

Huwa tunapenda kuona maisha ya wasanii wengi na Kuwaita marolimodo lakini huwa hatupendi kujua nyuma yao ya pazia.

Twende pamoja..

"Watu duniani wanauliza mara nyingi, ni lini utapunguza kasi, lakini ndio kama naanza," ni maneno ya Anna Mae Bullock ambaye jina lake maarufu ni Tina Turner.

Tina Turner alizaliwa 26 November 1939 huko Nut Bush, Tennessee.

Baba yake alimiliki shamba kubwa hivo msosi kwao haukuwa ishu. Akiwa mdogo alikuwa na sauti nzuri, lakini pia na ndoto.

Alikuwa na dada yake aitwaye Alline ambaye walizidiana miaka mitatu. Baba yake na mama walikuwa na ugomvi usiokwisha, akiwa na miaka 10 mama aliacha familia na kuondoka. Dunia yao ikabadilika.

Mbaya zaidi baba yao akaoa mke mwingine, siku ya siku akapaki mizigo akasepa, akawaacha home alone.

Wakati huo Tina alikuwa na miaka 13, ndugu yao mmoja akawachukua akaanza kuishi nao. Baadae dada yake akaenda kuishi na mama yao aitwaye Zelma huko St. Louis. Akiwa na miaka 16 Tina naye akaenda kuishi na mama yake.

Huko akahitimu shule ya upili (high school) akaanza kutoka auti ni dadaye Alline. Hapo ndipo alipogundua Klabu moja maarufu iitwayo Club Manhattan, klabu maarufu zaidi huko St. Louis (Kama ilivyokuwa Billcannas enzi za kina Zilla)

Kuna muda dada yake akaacha kumpeleka klabu, alipofikisha miaka 17 ndipo alimpeleka tena. 

Kuna siku wakawa wameketi kwenye meza wakisikiliza muziki bomba toka kwa bendi ya Kings of Rhythm.

Dakika chache stejini akatimba kiongozi wa bendi hiyo. Unajua alikuwa nani?

Huyu ni Ike Turner.

Mara ya kwanza kumuona Ike, Tina alikuwa na miaka 16 na Ike 24. Alikuwa bado anasoma. Ike alikuwa ni mtu aliyeunda bendi ya watu 18, iliyoitwa Tophatters baadaye ilivunjika katika makundi 2 mojawapo likiwa Kings of Rhythm lililoongozwa na Ike Turner.

Basi binti Tina akazoea ile klabu pamoja na dada ake. Wakawazoea waimbaji wa ile bendi. Siku moja wakawa nao wakamwambia dada yake Tina, Alline aimbe, kuruti akagomesha, Tina akaanza kuimba.

Watu "woyooo," utafikiri wamemsikia Maua Sama anaimba This Love. Baada ya hapo Anna akawa mmojawapo wa waimbaji wa The Kings of Rhythm. Ike akaanza kumwita "Little Ann" na akaanza kumnunulia nguo pamoja na vito vya thamani.

Akamnunulia mpaka jino la dhahabu. Binti akafikiri yuko mbinguni anaimba mapambio na kina Petro na Yakobo.

Lakini kulikuwa na tatizo, binti alikuwa Highschool na hakuwahi mwambia mama yake kazi yake mpya kwenye bendi ya The Kings of Rhythm.

Familia ikagundua anaimba, ikamkatalia kuimba.

Baadaye Ike akaamwomba mama yake na kumwambia atamtreat kama mdogo wake (yaani wawe kaka na dada😋) na kumwaidi binti yake atakuwa staa.

Akiwa na miaka 18 Tina akapata mtoto wa kwanza, baba yake alikuwa mmojawapo wa vijana wa ile bendi. Akiwa na miaka 20 akawa ndo mwimbaji mkuu wa bendi.

Miezi 6 baadae wakatoa ngoma iitwayo A Fool In Love ambayo ilikuwa hit song Amerika nzima. Sio kwenye chati za watu weusi mpaka chati za watu weupe kwenye topu 40. Miaka 10 ya kusubiri Ike akaona ametoboa. 

Akataka kwenda California na kuiacha bendi yake. Huko anakwenda na little Ann kuanzisha bendi mpya. Binti anakwenda kuwa staa na kuwa na jina jipya "Tina Turner."

Basi wakaenda huko na kuanzisha bendi iitwayo Ike and Tina Turner Revue. 

Ike akaweka madansa na waimbaji waitwao Ikettes walioimba na kucheza nyuma ya Tina. 

Ikettes walipewa sheria moja hakuna kuwa mrefu au mrembo zaidi ya Tina. Na kwenye shoo kumzidi Tina ni marufuku.

Mwisho mwa 1960 A Fool In Love ikiwa singo ya pili kwenye charti za Rhythm na Blues. Wakaanza kufanya tour iitwayo "The Ike and Tina Revue"

Wakanza kusafiri kwenye mahoteli na maklabu makubwa wanapiga pesa ndefu. Tina alifurahi sana. Lakini mambo yakaanza kubadilika. Kuanzia stejini hadi nje ya steji.

Ike Turner akaanza kukontroo kila kitu kwenye Revue, alichagua nyimbo, wanamuziki, klabu walizopaswa kwenda kupafomu, juu ya yote akaanza kumkontroo na Tina.

Kuna wakati Tina alipanda stejini akiwa na macho mekundu au mdomo umepasuka. Ikimuuliza afanye nini anasema, "Simjui mtu mwingine yoyote, nahitaji kuimba." Akaanza kuimba kale ka wimbo ka "Dunia duara mama eeeh, eeeh, dunia duara mama e, ntalia na nani?"

Kipindi hicho Tina alikuwa mama wa watoto wawili. Mtoto wa pili baba yake alikuwa ni Ike. Ilikuwa ni familia tayari huku Tina akiwalea pia watoto wawili wa Ike aliomkuta nao.


Muda kidogo baada ya kutoka St. Louis na kwenda California mwaka 1992 Ike alimuomba Tina awe mkewe. Akakubali kisa aliogopa.

Katikati ya miaka ya 1960 bendi yao ikaendelea kupaa juu. Lakini Ike akendelea kuwa na tabia mbovu.

Nyumbani Tina alikuwa kama paka aliyekosa maziwa kwenye steji alikuwa "Queen of the Jungle."

Mapenzi yakawa kizunguzungu, Nyimbo za kina Zuchu sijui Raha kwake ni ubatili mtupu, ni ubatili mtupu. Akawa anajisomea kitabu cha Fr. Kamugisha "Ndoa yataka moyo" anajifariji ili siku ziende.

Mpaka mwaka 1968 Tina alikuwa mgonjwa wa kudumu akienda hospitali kila mara kutokana na kichapo alichokuwa akipewa na mmewe Ike.

Kuna siku akataka kujiua, jaribio likashindikana. Akapelekwa Hospitali hajitambui, kushtuka uso kwa uso na mmewe Ike. Ike akamwambia...

"Unataka kufa? Kufa sasa." (Kama wewe ni mwanaume ulishawahi mwambia mtoto wa mtu haya maneno makali kama haya simama jipige kifua mara 3 sema Bwana nisamehe mimi mkosefu).

Hiyo ilikuwa siku ambayo Tina hatokuja kuisahau maishani.

Mwaka 1969 wakabadili aina ya muziki wakaanza kuimba rock na roll. Mmojawapo wa wimbo walioimba ni Proud Mary.

Miaka ya 70 Ike akafungua studio mpya iliyoitwa Bolic Sound Office. Akaanza kushinda huko hata siku 5 bila kulala akitumia dawa za kupoteza usingizi. 

Muda wote akitafuta hit song ya kutoa. Huku msanii wa kutegemewa akawa Tina.

Tina akaandika wimbo unaitwa Nutbush City Limits (ambao ulizungumzia maisha yake ya awali) ukabamba sana, huku ukishika namba 22 kwenye charti za U.S na 2 huko UK. Wakaanza kuwika kimataifa.

Ike akamwajiri mwanamke aitwaye Valerie Bishop mwaka 1974 alikuwa ni mbudha. Akamfundisha Tina kuhusu dini ya Kibudha.

Tarehe 2/7/1976 Tina akasema Liwalo na liwe. Wakawa wanakwenda Shoo wakitokea California. Wakiwa wanaelekea Airport Ike akataka kumpa Tina Chokoleti Tina akakataa, Ike akaanza kumgombeza. 

Zamu hii binti akauwa mkimya kama miaka 16 iliyopita akaanza kurudisha ngumi. Msekemseke ukaanza.
Hadi kwenye ndege bado wakawa wanazozana. Wakafika hotelini wamejaa damu wakasingizia wamepata ajali. Wakapewa chumba kimoja.

Wakaingia chumbani, Ike akalala kitandani(alikuwa hajalala siku 5) Tina akasubiri alale. Akajitazama kwenye kioo. Akaona amejaa damu usoni. Fasta akaenda kuosha uso wake, akavaa koti jeusi akaweka na miwani usoni. Huku akaiwa na senti 36 mfukoni. Akafungua mlango akasepa.

Ndoa ikaishia hapo akaanza kujificha hataki kabisa Ike amuone. Binti anatembea na mguu wa kuku.

Ike akamshitaki mahakamani kwamba anamdai dola 500,000. Kesi ikaenda mahakamani, Tina alisema jambo moja, "Chukua kila kitu tulichovuna wote miaka 16. Nitachukua fyucha yangu."

Tina akaendelea kusota peke yake. Miaka ya 80 akatoa ngoma Kama Private Dancer na What Love Got to do zilihiti sana utafikiri ni Tina wa mwaka 1960. Akaanza kupiga tua na kina Lionel Richie.

Private dancer ikatengenezewa mpaka muvi akatoa wimbo mwingine uitwao We don't need another hero.

Januari 28,1985 alipewa tuzo ya mwimbaji bora wa kike na msanii bora wa video. Baadae ndani ya aliungana na mastaa wengine kibao duniani ndani ya masaa 10 waliandika wimbo wa We are the World ili kupata pesa ya kuisaidia Ethiopia.

Hadi Leo hii Tina Turner ana miaka 80 na aliolewa tena na mjerumani Erwin Bach mwaka 2013.

Huyo ndiye Tina Turner mtunzi wa kibao cha I Don't Wanna Lose You ambacho binafsi ni kibao bora kwangu ukifatisha na kibao cha Private Dancer.

Funzo: Toka kwenye eneo lako la faraja(Get out of your comfort zone)
💎Mwisho✍🏽

#ElimikaNaEdius



✍🏽Imeandaliwa na

Edius Katamugora 👷🏾
Content Creator
Creative Writer
0764145476
ekatamugora@gmail.com

Hii ni blogu rasmi ya Edius Katamugora, hapa utajifunza maendeleo binafsi, utapata makala mbalimbali zinazohusu biashara, elimu, hamasa na maisha kwa ujumla. Karibu sana katika blogu hii.

0 comments: