Linapokuja suala zima la malezi, methali za Kiswahili zinatuweka wazi; mtoto umleavyo, ndivyo akuavyo, samaki mkunje anagali mbichi na asiyefunzwa na asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu.
“Inachukua Kijiji kumkuza mtoto” inasema methali ya kiafrika. Naye Vladimir Ilych Lenin kuhusu malezi alikuwa na haya ya kusema, “Nipe miaka minne niwafundishe Watoto na mbegu nitakayoipanda haiwezi kung’olewa kamwe.””
Malezi tunaweza kusema ni namna mtu anavyoelekezwa kuishi katika maisha yenye mpangilio na utaratibu na kuishi katika kanuni za jamii husika.
Kama mzazi ni muhimu mno kujenga tabia za mwanao tangu anagali mtoto, inawezekana wazazi wengine wanawaacha walimu shuleni nafasi hiyo ya kujenga tabia za wanao, wanafikiri kwamba mtoto wao atafundishwa tabia njema shuleni lakini wanasahau jambo moja muhimu ya kwamba familia ndiyo shule ya kwanza.
Kama wazazi ni muhimu kujua kwamba jukumu la kwanza kwa Watoto wetu ni kuwapa malezi bora na kuwapa msingi sahihi wa maisha. Nimesema msingi ili nieleweke vizuri, jengo lolote refu unaloliona limesimama katika msingi imara. Kadri jingo linavyozidi kwenda juu zaidi na chini yaani kwenye msingi ndivyo linavyokwenda chini zaidi.
Watoto mara nyingi hufanya matendo yale ambayo wanaanza kuyaona kwa wazazi wo. Unaweza kusikia mtoto akitoa matusi hadharani, kumbe ni yale matusi aliyoyasikia kwa wazazi wake jana usiku. “Kile mtoto akisemacho, amesikia nyumbani”, inasema yote methali ya Nigeria, Nao watu wa Uhispania wanasema, “Kile Watoto wanachosikia kutoka kwa wazazi wakati wa kuota moto, ndicho wanachorudia barabarani. ”
Katika kitabu chake cha MAISHA NI MTIHANI Padre Dk. Faustin Kamugisha anasema “Malezi ni mtihani.” Kama malezi ni mtihani na mtihani lazima mtu aufanye na kuushinda hivyi ni jukumu la mzazi kuhakikisha mwanae anapata malezi bora na si bora malezi.
Mtoto anahitaji malezi bora toka kwa pande zote mbili yaani baba na mama na si kwa mama tu. Wanaume wengi wamekua wakikosea hapa, wanawaachia jukumu zima la kulea wake zao.
Hii imekuwa wazi pale mtoto anapofanya makosa mwanamke ndiye anayenyooshewa kidole, utasikia mwanaume akisema, “Hivi ndivyo unavyowafundisha Watoto wako”. Makosa makubwa.
Kumbuka unapomnyooshea mtu kidole vitatu vinaelekea upande wako na kimoja kinaelekea juu kuonesha wazi kuwa na wewe unaohusika kwa namna moja ama nyingine.
Hivi karibuni kumezuka kitu ambacho ninaona kinakua kwa kasi sana, ningekuwa mtu wa mitandao ningesema kasi ya 4G. Unakuta binti anatafuta kijana anampa mimba kisha kwasababu binti huyo anakua na uwezo kiuchumi basi anaamua kwenda kumlea mtoto wake peke yake. Ni hawa tunaowaita single mother siku hizi.
Kuwa single mother inaweza kutokea kama ajali lakini usitengeneze mazingira kama wanawake wengi wanavyofanya siku hizi.
Kuna athari kubwa za mtoto kukosa malezi ya baba. Inawezekana usiyaone leo lakini madhara ukaja kuyaona huko baadae.
Tunatengeneza kizazi ambacho kwanza wanaona kuishi bila baba au mategemezi ya mwanaume ni kitu cha kawaida. Anaweza kuwa binti aliyekuzwa na mama yake, huyu akiolewa anaweza kuona kama mwanaume si lolote maana ameambiwa mengi na mama yake kuhusu wanaume toka anakua. Ndiyo maana Charles Swindoll aliwahi kusema, “Kila siku ya maisha yetu tunawekeza kwenye benki za kumbukumbu za Watoto wetu”
lakini pia anaweza kuwa mtoto wa kiume aliyelelewa na mama peke yake kwasababu hajawahi kuona majukumu ya baba katika familia asifanye chochote kwenye familia au akaoa mke na kuanza kumnyanyasa. Aya mambo ninayosema si hadithi za kusadikika za Alifulela Ulela, hasha! Yapo kwenye jamii zetu na tunayona kila uchao.
Takwimu zinasema kwamba karibia 85% ya vijana wadogo walioko gerezani walikualia katika nyumba zisizi na baba na karibia wafungwa wote wamekulia katika familia ambazo hazikuzingatia malezi bora.
Kila matokeo yana chanzo, wazazi tusiwe chanzo cha kuwanyima Watoto wetu malezi bora na hatimaye wakaja kuishia gerezani.
Suleimani mwandishi wa kitabu cha Mithali akijua umuhimu wa malezi anasema, “Mlee mtoto kaika njia impasayo naye ahataiacha, hata atakapokuwa mzee” (Mithali 22:6)
Wafundishe wanao kujituma ka kufanya kazi kwa bidi. Wote waliofanikiwa neno “bidii” huwa halikosi kinywani mwao wanapoulizwa kuhusu mafanikio yao. Inawezekana umewahi kusikia kuhusu Serene na Venus Williams. Hawa ni wadada waliotikisa katika ulimwengu wa mchezo wa tenesi. Wakiwa wadogo iliwapaswa kila asubuhi saa 12 alfajiri kuamkia uwanjani kufanya mazoezi na kisha ndipo walipokwenda shule, leo hii wamekuwa hapo walipo. Hakuna kinachokuja kwa urahisi.
Mwandishi wa kitabu cha The road less travelled alianza kitabu chake kwa kuandika maneno haya. “Maisha ni magumu.” Usimpe mwanano kila kitu vingine mfundishe kutafuta mwenyewe. Usimpe samaki kila siku bali mfundishe kuvua samaki ili siku samaki wakikosa akavue mwenyewe. Kwa msingi huo naunga mkono hoja maneno ya Lazarus Long aliyesema, “Usiwafanye wanao vileme kwa kuyafanya maisha yao kuwa mepesi.”
Ndimi,
Edius Katamugora
ekatamugora@gmail.com
0764145476
0 comments:
Post a Comment