“Ni majaliwa yake Mungu eeh kuuona
mwaka”, waliimba kundi fulani la bendi. Ama kweli ni jambo la heri na la
kumshukuru Mungu kuuona mwaka mpaya wa 2021, kushukuru ni kuomba tena, pia
shukrani ni jambo la busara.
Mwaka uliopita wa 2020 ulikuwa na
mambo mengi ambayo yalitutia hofu ya kuuona mwaka huu mpya wa 2021, wengine
wameishia kusema sijui umeishaje lakini ndio hivyo umekwisha na sasa tupo
katika mwaka mpya.
Nimeona ni kosa kubwa nisipokuandikia
mpendwa msomaji wangu katika siku hii mpya naya kwanza katika mwaka,
nisingeandika chochote nitakuwa sijatenda haki.
Kama ilivyo miaka mingine natumaini
umejipanga kufanya makubwa kama ambavyo huwa unafanya kila mwaka. Binafsi
nimejipanga pia kukupa mambo mazuri wewe msomaji wangu, yatakayo kukuza
kifikra, kiimani, kiutendaji na kiuchumi.
Wakati mwaka 2020 unakaribia ukingoni
niliwaaga rafiki zangu na wasomaji wangu kwamba sitokuwepo katika mitandao ya
kijamii hadi ifikapo Aprili mosi, ni kweli nimeanza kufanya jambo hilo hata
kabla ya wakati niliopanga haujafika yaani leo Januari Mosi.
Nimefanya hivyo hili kujipa muda wa kufanya uchunguzi wa “KUNA NINI NJE YA MITANDAO YA KIJAMII” lakini pia kuwasaidia watu kupunguza uraibu (additictions) katika mitandao ya kijamii. Naamini katika kipindi hiki cha miezi mitatu nitakuja na majibu sahihi yenye utafiti na mashiko.
Nisiende mbali basi nirudi katika mada
yangu iliyonisukuma kuandika makala hii.
Ninajua unayo mambo mengi ambayo
umepanga kuyafanya katika mwaka huu mpya
wa 2021, nimeamua nami kukuongezea baadhi ya mambo ambayo yatakusaidia kuufanya
mwaka huu mpya wa 2021 kuwa mwaka bora kwako.
Fanya yafuatayo hili kuufanya mwaka
2021 kuwa mwaka bora kwako.
1. 1. Sali sana
Kuna aliyewahi kusema, “Usiifanye sala kama spea tairi kwamba unapolihitaji ndipo unalikumbuka,” Mungu hachezi mchezo wa kubahatisha, alisema mwanasayansi nguli Albert Einstein. Jitahidi kutanguliza sala katika yale ufanyayo, mtangulize Mungu mbele katika kila jambo. Usikumbuke sala wakati mambo yako yamekwama. Usikumbuke kuvuta shuka wakati kumekucha, inakumbusha methali ya Kiswahili.
Tunakumbushwa katika biblia “Mkumbuke Mungu siku za ujana wako…”” (Mhubiri 12:1)
2. 2. Weka malengo ya miaka kumi
“Hatupangi kushindwa, tunashindwa kupanga,” ni msemo tunaousikia mara kwa mara, bila mipango ni kana kwamba unatembea na unakwenda kusikojulikana, utapotea.
Jipe changamoto unataka kuwa umefanya nini ndani ya miaka kumi ijayo yaani hadi mwaka 2030 uwe umefanya mambo gani, kisha orodhesha katika hayo mambo mwaka huu unatakatiwa kufanya nini. Ni katika kupiga hatua ndogo tunafikia pakubwa, ngazi moja hukupanisha kwenye nyingine.
Nimetumiwa ujumbe siku hii ya leo na rafiki yangu uliosema, "Mungu abariki mipango yenu 2021. Fanya tathimini ya 2020, weka malengo, yapimike na uyape muda wa utekelezaji. Yaandike ukutani, kila litakalofanikiwa, weka alama ya vema. Yapange kwa uzito wake."
Kuna aliyewahi kusema, “Maisha hayana lifti za umeme bali maisha yana ngazi lazima upande ngazi moja baada ya nyingine.”
3 3. Jifunze vitu
vingi
Mchungaji Sunday Adelaja anasema waafrika wengi tumekubwa na kitu kinachoitwa MLIMA WA UJINGA. Naye baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere mojawapo ya vitu alivyovipiga sana vita ni ujinga. Hata kwenye maandiko tunasoma, “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa” (Hosea 4:6a).
Mwaka 2021 jiwekee ratiba ya kujifunza kitu kabla hujakwenda kulala. Ukipanda kitandani kila siku usiku jiulize swali hili, “Leo nimejifunza nini?”
4. 4. Kuwa mtu wa
watu
Wahaya wa Tanzania wana msemo husemao, “Watu ni Mali.” Kila kubwa unalotaka lifanikiwe linahitaji watu. Jichanganye na watu, wasaidie watu maana ni katika kutoa tunapokea, asiyetoa hapokei, hasiyepoteza haokoti.
Kuwa tayari kuwa daraja la wengine kuvuka ili wapate kile wanachotaka na usiwe kikwazo. Wakina “fulani yule ana roho mbaya” huwa hawafiki popote na awaendelei. Tafadhali usiwe mtu aliyewekewa chata hiyo mbaya.
Kadri unavyofahamiana na watu wengi ndivyo fursa zinazidi kufungukia upande wako.
Mwandishi wa kitabu cha It’s not how good you are, it’s how good you want to be Paul Arden anasema, fikiria wewe ni msanifu majengo (Archtect) na watu wanaokufahamu ni wale tu wa kampuni unayoifanyaia kazi, je unafikiri ni hilo ni jambo jema? Anamalizia kwa kusema, “Sio kile unachokifahamu bali ni watu wangapi unaowafahamu,”
Mzunguko wa watu unaowafahamu ndiyo thamani yako. Mwisho wa yote usimdharau yeyote unayekutana naye maana ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
5. 5. Kuwa na matumizi bora ya fedha
Ili ukuwe kiuchumi ni wazi kuwa lazima uwe na matumizi bora ya fedha. Kuwa mtu wa bajeti, usiitumie pesa kabla haijangizwa katika bajeti. Shida ya pesa ni kwamba ukiwa nayo matumizi huongezeka. Kumbuka pesa ina macho na inaona, pesa ina miguu, inatembea, pesa ina pua, inanusa, pesa ina masikio inasikia.
“Pesa ni kama mgeni; inakuja leo na kuondoka kesho,” ni methali ya Malawi. “Kutengeneza pesa ni kama kuchimba kwa sindano, kuitumia ni kama kumwaga maji mchangani,” inatukumbusha methali ya Japan.
“Kuitafuta pesa ni mtihani, Okoa pesa na pesa itakuokoa (Methali ya Jamaica)” ameandika Padre Faustin Kamugisha (Phd) katika kitabu chake kiitwacho Maisha ni Mtihani.
6. 6. Jua mambo mengi
Hii inaendana na hile ya tatu ya kujifunza mambo mengi. Tunaishi katika dunia ambayo watu wanaojua vitu vingi ndio wanaokumbatiwa kuliko watu waliojifungia katika kitu kimoja. Ukiwa shuleni au kazini usiwe mtu wa “Hii sio kazi yetu ni ya watu fulani,” jifunze, hauwezi kujua itakupeleka wapi.
Mimi niliamua kujifunza uandishi bila kwenda chuoni hiyo ikanipelekea kuandika kwenye gazeti na huko nimekutana na watu walionipa fursa katika kazi za ujenzi ambazo nimesomea, je ningejiweka katika chumba cha “Mimi ni mtu wa ujenzi” ningekuwa wapi?
Hakuna hasara katika kujua vitu, hakuna kitu kama uharibifu wa maarifa, unaweza kujifunza kitu leo usione umuhimu wake lakini kikaja kukufaa siku za usoni. Ni heri ujue vitu vingi kuliko kutojua vitu.
Yote yakishasemwa, Nikutakie MWAKA MPYA 2021 wenye mafanikio, afya njema na furaha tele!
Wenu,
Edius
Katamugora
0764145476
ekatamugora@gmail.com
0 comments:
Post a Comment