Monday, 15 February 2021

MAMBO 3 MUHIMU YA KUZINGATIA KWA KILA KIJANA

     


Wiki si nyingi zilizopita nilikutana na Tajiri mmoja anayemiliki mabasi ya kwenda mikoani, kampuni ya ujenzi na kiwanda cha maji lakini pia amewekeza katika kilimo. Tajiri huyu aliniambia maneno haya, “Hawa vijana wa siku hizi nawaogopa sana,” Nikamuuliza kwanini? Akasema, “Hiki nahisi ni kizazi ambacho Mungu alikiumba na kukipa akili kubwa sana,” Akaendelea kusema, “Yaani mimi mkinipa vichwa vyenu napambana kwa miaka 3 tu kisha naanza kukesha kanisani.”

Hapo sasa nikaja kukumbuka maneno ya Mark Zuckerberg aliyewahi kusema, “Vijana wadogo wanaakili.”

Sijasema haya kuwasifia vijana lakini nimesema haya kuwapa motisha kwani wazee wetu wanatuangalia kwa jicho la kipekee na wanatuona kama ni kizazi teule. Yule Tajiri lakini hakuishia hapo alimalizia akisema, “Tatizo lenu kubwa ninyi vijana ni kwamba hamfikirii siku za mbeleni mnafikiria mambo ya karibuni, mnataka kila kitu kitokee hapo hapo, ukimwambia kijana awekeze kwenye biashara itakayoanza kulipa baada ya miaka 3 au mitano au kumi anaona kama unaongea blah blah.”

Hapo niseme kwamba, “Akili za kuambiwa, changanya na zako,” kama alivyopenda kusema mzee Jakaya Kikwete.

Je kama kijana unayeanza maisha unatakiwa kufanya nini?

Kama kijana unayeanza maisha unatakiwa kuchukua muda wako mwingi ukifanya chaguzi. Kumbuka leo hii wewe ni matokeo ya chaguzi ulizowahi kuzifanya, na kesho yako itategemea na chaguzi unazozifanya leo. “Maisha ni maamuzi,” aliwahi kuimba mfalme wa Salasala Godizillah.

Kuna chaguzi tatu muhimu unazotakiwa kufanya kama kijana; wapi unaishi, upo na nani na nini unachokifanya.

                                                     Wapi unapoishi


Sisi ni matokeo ya mazingira yanayotuzunguka. “Ukienda sehemu wanapokula konokono na wewe unakula konokono,” inasema methali ya Kihaya. Jiulize je, mazingira uliyonayo yanaweza kukufanya utimize ndoto zako na mipango yako, kama jibu ni hapana basi unatakiwa kutafuta mazingira sahihi. “Kama haupendi mahali ulipo, ondoka, wewe sio mti,” anasema muhamaishaji Jim Rohn.

                                Upo na Nani?

                                

Kila mtu anahitaji watu ili afanikiwe lakini sio kila mtu ni wa kuambatana naye. Watu wanaokuzunguka wana mchango wa kukupeleka mbele au kukurudisha nyuma. Chagua vizuri watu wa kuwa marafiki zako. Marafiki ni kama ngazi, wanaweza kukushusha na kukupandisha. “Watu huchukua tabia n ahata mawazo ya wale wanaokaa nao,” aliandika Napoleon Hill miaka 83 iliyopita baada ya kuwafanyia uchuguzi matajiri 500. Naye milionea na mwandishi Steve Siebold anasema, “Kipato chako kinakaribiana na kile cha marafiki zako wa karibu.” Leo hii fanya tathimini ya wale wanaokuzunguka. Je wanakusaidia kufikia malengo na maoni yako?

                                                     Nini Unachokifanya?


                                  

Ni mambo gani unafanya, je ni kazi inayokuingizia kipato, ama umejiajiri na unaingiza kipato kupitia biashara au huduma unayoitoa au kuna ujuzi fulali unajifunza? Kila muda kaa chini na tafakari juu ya yale mambo unayoyafanya kila siku. Jali sana muda wako, muda wako ndicho kitu cha thamani sana hapa duniani. Mwisho wa yote kumbuka, Maisha hayana gia ya kurudi nyuma.

Tafadhali share ujumbe huu kwa rafiki zako wa karibu. Sharing is caring.

Imeandaliwa Na

Edius Katamugora

0764145476

ekatamugora@gmail.com

 

Hii ni blogu rasmi ya Edius Katamugora, hapa utajifunza maendeleo binafsi, utapata makala mbalimbali zinazohusu biashara, elimu, hamasa na maisha kwa ujumla. Karibu sana katika blogu hii.

0 comments: