Saturday 20 February 2021

FANYA HAYA KUWA MAARUFU/MTU WA WATU

                                       

Umewahi kujiuliza kwanini mtu fulani anapendwa sana na watu, au mtu fulani anajulikana sana kwa watu na wewe hujulikani? Au umewahi kujiuliza kwanini mtu fulani unayemjua kuna marafiki zako wengine ambao hutegemei hata kama wanamjua lakini unakuta wanamjua.

 

Je jambo kama hili hutokeaje? Je watu hao ni watu wa namna gani?

Kuna siku nilikuwa nikitembea mjini na rafiki yangu tukaingia kwenye ofisi moja, katika angaza angaza macho nikaona kibao cha ofisi fulani, katika ofisi hiyo kuna mtu anafanya kazi hapo ni rafiki yangu sana wa muda mrefu, lakini sikujua kama wanayo ofisi katika sehemu hile tuliyokwenda.

Yule mtu niliyekuwa naye nikasikia anasema, “Hapa kuna rafiki yangu fulani anafanya kazi katika ofisi hii,” chap kwa haraka nikamuuliza anaitwa nani? Akataja jina, nikashtuka, alitaja jina la yule mtu ninayemfahamu.

Basi bwana nikamuuliza ulimfahamu vipi huyu mtu, akanijibu, “Yule jamaa ni mtu,” Hapo ndipo nikatambua kumbe kuna tofauti kubwa kati ya binadamu na mtu.

Ndipo nikaanza kufanya uchunguzi watu ambao wana tabia za yule mtu rafiki yetu huwa wanaishi vipi na watu na wanafanyaje mambo yao.

Kama unataka kuwa kama mtu niliyemzungumzia fanya mambo haya kuwa maarufu au mtu wa watu;

1.Wajali watu bila kujali wana nini 

                      

Jali kila mtu bila kuangalia ni mkubwa au mdogo ana cheo au ana cheo. Waheshimu watu wote, usiwabague. Kosa kubwa ambalo watu hufanya ni kuwanyenyekea wale tu ambao ni wakubwa wao au wale ambalo wanaweza kuwasaidia. Mtu akija ofisini kwako msaidie huwezi jua kesho na kesho kutwa atakuwa nani. Kuna watu ambao wanajuta kama wangejua Rais Magufuli atakuja kuwa Rais basi wangemtendea mema ili baadae awakumbuke lakini hawakuitumia fursa hiyo vizuri. Wasaidie watu kadri uwezavyo. Jijengee utaratibu wa kwamba kila mtu unayekutana naye ana fursa ya kukusaidia au wewe kumsaidia. Nyenyekea ule vya watu. 

2. Kuwa msikilizaji mzuri, wahase wengine waongee kuhusu wao 

                      

Watu wengi wanapenda kuongea na hawapendi kusikiliza. Tumepewa ndomo mmoja na masikio mawili vitumike vyote kwa uwiano sawa, yaani ongea kidogo na sikiliza sana. Unapoongea unatoa kile unachokijua tu lakini unaposikiliza kuna vitu vingi unajifunza. Nelson Mandela aliwahi kuulizwa ni nini siri ya kuwa kiongozi bora, alijibu, “Ili uwe kiongozi bora jifunze kuwa wa mwisho kuongea,” anasema alipokuwa mdogo baba yake alipokuwa akienda kwenye vikao alikuwa akiwasikiliza watu wote kisha anakuwa wa mwisho kuongea.

Wasikilize watu wanaposema shida zao, sikiliza kuelewa na usisikilize ili uwahi kujibu. Wahase watu waongee zaidi kuhusu wao. Dale Carnegie alikuwa akiendesha darasa la NAMNA YA KUONGEA HADHARANI (PUBLIC SPEAKING COURSE) kuna siku akaishiwa kabisa maneno au mambo ya kufundisha. Ndipo alipoanza kuwaruhusu wanafunzi wake kila mmoja anyanyuke na aanze kuongea kuhusu yeye. Alishtuka kuona watu wengi wanafunguka mambo mengi na wanapenda hasa kufanya hivyo. Aligundua jambo kubwa kwamba watu wanapenda kuongea kuhusu wao. Hayo yakampelekea aandike kitabu kiitwacho HOW TO WIN FRIENDS AND INFLUENCE PEOPLE. Watu maarufu pia waliweza kuingia kwenye darasa lake mmoja wapo akiwa Tajiri na mwekezaji mkubwa Warren Buffet.

Unaambiwa ukiingia ofisini kwa Warren Buffet cheti pekee alichotundika ukutani kwake ni kile alichopewa baada ya kuhitimu kozi ya Dale Carnegie.

    Jifunze kwa kila mtu uanyekutana naye, nakubaliana na Ralph Wardo Emerson aliyewahi kusema, “Kila mtu ninanyekutana naye ni mkubwa kwa njia moja ama nyingine. Kwa kulitambua hilo najifunza kutoka kwake.” 

      3. Tabasamu

              
                       

Tabasamu hubeba ujumbe mzito kwenye uso wa anayelitoa. Tabasamu linasema,, mimi ni mwenye furaha, mimi naufurahia wakati uliopo, mimi nayafurahi maisha, mimi hata iweje sinuni, tabasamu linasema kama nimeshindwa leo kesho nitafaulu. Wachina wana msemo usemao, “Kama huwezi kutabasamu, usifungue duka.” Tabasamu ni ishara ya kuwakaribisha watu wawe karibu yako. Unapokutana na mtu mpya mtazame machoni na kisha tabasamu. Mtu huyo anaondoka na furaha kwamba ulimpokea vyema. Usiwe mtu wa kununa nuna watu watakukimbia.

4. Ongea katika namna ya yale wanayoyapenda watu wengine  

U   Unapokutana na watu ongelea vitu wanavyopenda wao na si unavyopenda wewe, utawaboa. Ongelea matatizo yao na uyape suluhu. Watu watakukimbilia kama wewe ni mtatua matatizo na si mleta matatizo. Kuwa mmoja wa watatua matatizo ya watu, wenye matatizo ni wengi duniani na wale wanaotatua matatizo ni wachache mno kuliko kawaida. “Kama hutatui tatizo wewe ni tatizo,” anasema Mchungaji Sunday Adelaja.

       5.Wapongeze watu bila unafiki

     Mtu fulani anapofanya kitu kizuri kuwa tayari tena mstari wa mbele kumpongeza, mtie faraja na mtie moyo kuwa aendelee kusonga mbele. Usiwe mtu anayechukia mafanikio ya mwenzako. Wanaofanikiwa wanaendelea kufanikiwa kwasababu wanafurahia kuona wenzao wanafanikiwa. Mafanikio hayahitaji wivu, wivu ni kidonda, ukishiriki utakonda. Toa pongezi kila inapohitajika, usisubiri wengine waanze, hata mtu akifanya jambo dogo namna gani kama limefanikiwa mpongeze, ataona unajali. Na watu wanaanza kujali baada ya kuona na wewe unajali.

Imendaliwa Na,

Edius Katamugora

ekatamugora@gmail.com

0764145476 

Tafadhali sambaza (share) ujumbe huu kwa rafiki zako. Sharing is caring.

Hii ni blogu rasmi ya Edius Katamugora, hapa utajifunza maendeleo binafsi, utapata makala mbalimbali zinazohusu biashara, elimu, hamasa na maisha kwa ujumla. Karibu sana katika blogu hii.

0 comments: