Friday 12 March 2021

WATU WAMECHOKA KUSUBIRI. OKOA MUDA WAO


Unasubiri mpenzi wako akutumie SMS baada ya neno “Nikwambie kitu,” anachelewa. Unasubiri maji uliyoweka jikoni yachemke upate chai. Unasubiri gari kituoni, yote yanafika yamejaa. Unasubiri mzigo wako ulioagiza mtandaoni, siku unaona kama zimeganda. Unasubiri siku uliyoambiwa kutolewa ‘out’ haifiki. Ukiwa mtoto unasubiri Krismasi au Pasaka ifike ili uvae nguo mpya, nayo unaona haifiki. Siku mshahara ukitoka kwenye ATM kunakuwa na msululu wa watu, unaona kama haufiki, bado unasubiri. Matokeo ya kidato cha nne yanatoka na unasubiri uone umepangiwa shule gani, kila uchao unaona jamaa wamekaa kimya. Unasubiri matokeo ya usaili wa kazi uliyoomba, bado nayo hayatoki.

Matokeo ya haya yote yanasababisha watu kupoteza uvumilivu. Watu wanataka mambo yanayookoa muda. Tazama kote utaona wazi, Taxify ilikuja ili kuokoa muda, rice cooker inaokoa muda, gesi zinaokoa muda wa kupika, sehemu zenye nembo ya FAST FOOD wote hawa wanataka upate chakula fasta, ulipe usepe chao. Kuna ambao wakienda kwenye duka la simu kununua chaja utasikia wakisema, “Nahitaji fast chaja,” kuna watu ni wavivu hadi kutafuna miwa sasa wanatengenezewa juisi ya miwa. Kuna ambao wanasafiri na ndege wanavaa track suit na sendo ili tu wasipoteze muda kuvua mkanda na viatu wakati wa CHECK IN. wale wanaopiga picha za passport size utasikia wakitangaza, “Pata passport size ndani ya dakika 3”

  Haya yote ni kukufanya uonekane haupotezi muda. Ukipatia kuokoa muda wa watu umetoka kimaisha. Jiulize leo, je hiki ninachokifanya au ninachotaka kufanya kinaokoa muda wa watu?

Hii ni blogu rasmi ya Edius Katamugora, hapa utajifunza maendeleo binafsi, utapata makala mbalimbali zinazohusu biashara, elimu, hamasa na maisha kwa ujumla. Karibu sana katika blogu hii.

0 comments: