Tuesday 20 March 2018

Mchango Wa Mzazi Kwa Mtoto Katika Kuutafuta Utaalamu


Wazazi wanao mchango mkubwa katika kutengeneza njia ya mtoto au watoto wao kuwa wataalamu. Wazazi au wanauwezo wa kumfanya mtoto wao awe mtaalamu au kuharibu kabisa njia yake ya kuwa mtaalamu. Yote mawili yanawezekana.

     

Vitu ambavyo mzazi anatakiwa kuvifanya kwa watoto wake.
Kuna mambo ambayo wazazi wanatakiwa kuyafanya ili mtoto wao aweze kuwa mtaalamu katika Nyanja Fulani. Mambo hayo ni kama yafuatayo:


NYUMBANI NDIPO MAHALI SAHIHI NA SHULE NZURI KULIKO SHULE YENYEWE
Kuna wazazi wengi ambao wakimpeleka mtoto wao shule hufikiri kazi imekwisha kumbe hapana. Nyumbani ndipo kuna shule kubwa kuliko hata shule ambayo mwanao anakwenda. Heshima ya mwanao hataitoa shuleni bali katika familia anayotoka, tabia nzuri huanzia nyumbani na si shuleni. Haujawahi kusikia watu wakisema, “Upendo huanzia nyumbani?” Watu wengi ambao wamekuwa wataalamu katika sekta mbalimbali nyuma yao kuna mchango mkubwa wa familia zao. Ben Carson ambaye mwanzoni alikuwa anaonekana ni mtu wa kuwa wa mwisho darasani mama yake alimkataza kutizama televisheni na kumwanzishia program ya kusoma vitabu viwili kila wiki yeye pamoja na kaka yake Curtis. Baada ya kuanza kusoma vitabu maisha yake yalibadilika na alianza kushika nafasi za juu darasani. Mchango huu wa mama yake umemfanya kuwa daktari bingwa wa ubongo. Ameweza kufanya oparesheni kubwa za ajabu na za kutisha. Bila mama yake kuweka juu leo hii dunia isingemtambua Ben Carson.
Siku moja mtoto wa miaka minne ambaye uwezo wake wa kusikia ulikuwa mdogo alirudi kutoka shule akiwa na ujumbe ambao aliupeleka moja kwa moja hadi kwa mama yake. Ujumbe huo ulisomeka hivi, “Mtoto wako ni mpumbavu, hawezikujifunza, mwondoe shuleni.” Mama yake aliusoma ujumbe huo na kujibu, “Mtoto wangu ni mpumbavu, hawezi kujifunza, nitamfundisha mwenyewe.” Kilichofuata ni historia mtoto huyo baadaye alikuwa maarufu sana. Na si mwingine bali ni Thomas Edson, huyu ndiye aliyegundua kamera na pili ndiye aliyegundua balbu ya umeme. Anajulikana duniani leo kama baba wa umeme. Inawezekana asingekuwa mama yake, hadi leo hii tungelikuwa bado tunatumia vibatari, taa za chemli na mishumaa.


MJENGEE MWANAO TABIA YA KUSOMA VITABU.
Vitabu vimebadilisha sana maisha ya watu. Ukiniuliza siri ya mafanikio, siwezi kukosa kukwambia ni vitabu. Bila vitabu siishi. Kama mzazi una wajibu mkubwa wa kumjengea mwanao tabia ya kusoma vitabu, kutokana na vitabu atajifunza mengi. Waafrika wengi hatuna tabia ya kuwa na maktaba katika majumba yetu ndiyo maana kila siku tutaendelea kubaki nyuma na kupitwa na wenzetu. Kuna wazazi wengi ambao wananunua magazeti ya udaku na kuyarundika nyumbani kwao, hawa wanawaharibu watoto wao kwa spidi kubwa hata kuliko ile ya mwanga. Mzazi ukijenga tabia ya kusoma vitabu au hata magazeti yenye Makala za kufundisha wanao pia watavutiwa na kuanza kuiga tabia hiyo. Usipendelee kuwapa wanao zawadi kubwa ambazo hazitawasaidia miaka kumi ijayo. Kama kuna zawadi kubwa unaweza kumpa mwanao ni kumnunulia kitabu. Kama ukishindwa kumudu gharama za kununua vitabu mchukue mwanao na nenda kamwandikishe kwenye maktaba za mkoa ambazo zipo kila mkoa Tanzania nzima. Uzuri gharama ya kujiunga na maktaba ni bei rahisi sana ambayo kila mtanzania anaweza kuimudu. Gharama hiyo ni kuanzia shilingi 7000 kwa wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari na shilingi 9000 kwa wanafunzi wa vyuo na wananchi wote kwa mwaka. Hiyo ni pesa ambayo kila mtu anaweza kuipata. Mtoto wako hata kama anasoma shule za kulala, akija likizo hakikisha anakwenda makatba ili aweze kusoma vitabu na si kumwacha nyumbani akitizama televisheni siku nzima hilo alimsaidii lolote.

itaendelea.....

TANGAZO:
Bado napokea oda za kitabu cha NAMNA YA KUWA KUWA MTAALAMU UKIWA BADO UNASOMA (HOW TO BE AN EXPERT WHILE AT SCHOOL).
Watu 100 wa kwanza kuweka oda watapata kitabu hicho kwa bei ya shilingi 5000/= tu baada ya hapo bei itapanda. Wahi sasa nafasi zimebaki chache. Unaweza kuweka oda kupitia mawasiliano yangu hapa chini. Kitabu hicho kitakuwa kwa njia ya NAKALA TETE(soft copy) hivyo tutaweza kumfikia kila mtu. Kitabu hiki ni muhimu kwa kila mwanafunzi, mwalimu na mdau yeyote wa elimu. Karibu sana.


Ndimi:
EDIUS KATAMUGORA
0764145476
0625951842 (WhatsApp)
Email: ekatamugora@gmail.com

Hii ni blogu rasmi ya Edius Katamugora, hapa utajifunza maendeleo binafsi, utapata makala mbalimbali zinazohusu biashara, elimu, hamasa na maisha kwa ujumla. Karibu sana katika blogu hii.

0 comments: