Wednesday 10 February 2021

SABABU 4 MUHIMU KWANINI UANZE KUTUMIA EMAIL (BARUA PEPE) MARA MOJA KUANZIA SASA

 Uchunguzi wangu mkubwa nilioufanya siku za hivi karibuni nimegundua kwamba watanzania wengi hawana kabisa utaratibu wa kutumia email mara kwa mara. Wengi wa watu niliowafanyia uchunguzi hawana kabisa email na hata wale wenye nazo hawajui namna ya kuzitumia.

                             

Ni siku si nyingi zimepita nimekutana na mwanafunzi wa chuo kikuu hajui kabisa kutumia email, inasikitisha.

Ukimwambia mtu akutumie kitu fulani kwenye email ni kana kwamba umemtukana. Sasa katika zama hizi za mapinduzi ya nne ya viwanda na nyakati hizi za zama za taarifa ni muhimu sana kutumia email ili mambo yako yaende sawasawa.

Inawezekana sasa hivi usinielewe na uanze kusema jamaa anaongea upuuzi gani huyu, lakini siku yakikukuta yatakayokukuta utakuja kunikumbuka.

sikutishi ila huo ndio ukweli. Sasa kabla sijaenda mbali hebu nikupe faida 4 za kutumia email (nafikiri ukizijua hizi faida 4 utaanza kutumia email yako mara moja kuanzia sasa);

1. Email hutunza kumbukumbu

Watu wengi wamezoea kutumiana taarifa mbalimbali na wengine mafaili muhimu kupitia mitandao ya kijamii kama vile WhatsApp na Telegram na mingnineyo lakini mitandao hii huweza kufuta mafaili hayo ama si rahisi kuyapata unapopoteza simu yako au simu yako kupoteza mafaili.

                                     

Unapokuwa na email hakuna kinachopotea. Mtu akikutumia ujumbe fulani unaweza kupata hata baada ya miaka kumi. Sasa kwanini bado unaendekeza mambo ya WhatsApp wakati unatuma vitu muhimu kwa marafiki zako na hata mambo mengine ya kikazi na biashara?

2. Email ina faragha zaidi ya mitandao ya kijamii

Kudukuliwa limekuwa jambo la kawaida sana kwa Tanzania na Afrika kiujumla. Chunguzi zinasema hadi sasa Afrika kiujumla ina ukosefu wa wataalamu wa udukuzi zaidi ya 100,000. Taarifa zaidi zinasema dukuzi zaidi ya 96% hufanyika Afrika na haziripotiwi.

                          

Dukuzi nyingi sikuhizi hufanyika katika mitandao ya kijamii. Email ni njia salama ambayo faragha yake ni kubwa sana kuliko ya mitandao ya kijamii.

Kama una mambo yako ya muhimu na ya siri nakushauri utumie zaidi email kuliko kutumia mitandao ya kijamii kuyafanya.

3. Email ni njia salama na nzuri ya kuhifadhi mawasiliano yako

Unakumbuka kipindi umepoteza simu ulipitia changamoto gani? Unakumbuka siku ulipompigia  mtu fulani simu akakwambia alipoteza simu na hivyo hakuwa na namba yako? Haya yote hufanyika kwasababu watu wengi si watumiaji wa email.


Ukiwa na email unaweza kuhifadhi mawasilianao yako yote. Mpaka leo hii email yangu ina mawasiliano zaidi ya 1000 ambayo hata ningekuwa na line ngapi nisingeweza kuyatunza.

Siku nyingine ukipoteza simu na ukakosa kuwa na namba za watu jua tu ni uzembe wako sio uzembe tu bali uzembe uliopindukia.

4. Ni njia rasmi ya mawasiliano ya kikazi

Siku hizi mawasiliano mengi ya kikazi yanafanyika kwa njia ya email. Usishangae siku moja bosi wako anakwambia niandikie email. Ni muhimu pia kujifunza namna nzuri na bora ya kuandika email sasa. Nimeona siku hizi Gmail wameweka hadi sehemu ya kufanyia vikao kwa njia ya video kama ilivyo kwa mtandao wa Zoom mambo yanazidi kuwa makubwa kila uchao.

5. Email Haipunguzi ubora wa kitu

Nafikiri si mara ya kwanza kusikia kwamba ukimtumia mtu picha kupitia Whatsapp ubora (quality) wake huwa unapungua. Unfanyaje kuepuka shida hii? Email ni jibu tosha. Ukitumia email hauwezi kupunguza ubora wa picha au kitu kingine, picha yako inapokelewa kwa ubora ule ule.

 

Imeandaliwa Na

Edius Katamugora (Kijana wa Maarifa)

0764145476

ekatamugora@gmail.com

Hii ni blogu rasmi ya Edius Katamugora, hapa utajifunza maendeleo binafsi, utapata makala mbalimbali zinazohusu biashara, elimu, hamasa na maisha kwa ujumla. Karibu sana katika blogu hii.

0 comments: