Monday 31 May 2021

BARUA KWA MDOGO WANGU (2)

 


Jumapili 2:30

Mei, 30, 2021

Mpendwa Edgar,

Mambo kiddo, ni matumaini yangu kusikia kwamna hujambo make ni jana Jumamosi nilipoongea na wewe kwenye simu mama na kaka walipokuja kukuona shuleni, ingawa mazungumzo yetu yalikua ya muda mchache ndiyo maana nimesukumwa kukuandikia barua hiyo.

Kwanza jana, nilisahau kukuuliza kama tayari umenunua faili nililokwambia kwa ajili ya kuweka barua hizi ninazokutumia. Lakini kwa ninavyokufahamu tayari utakuwa umefanya hivyo.

Lakini pia nikuombe radhi Jumapili iliyopita sikuweza kukuandikia barua yangu ya pili kama nilivyoahidi kwenye barua yangu ya kwanza kwamba nitakuandikia barua kila Jumapili, sio kwamba nilikosa la kukuandikia, hapana, lakini nilitingwa na majukumu. Leo pia ratiba zangu zilikua zimekaza kidogo lakini imebidi nijiibe usiku huu niweza kukuandikia barua hii.

Natamani sana nikwambie mengi yaliyotokea kwenye ulimwengu wangu wiki hizi mbili zilizopita. Lakini kabla sijasahau, kwenye mazungumzo yetu ya jana ulinipa habari njema ambayo nilikupongeza sana lakini kuna kitu cha muhimu nilisahau kukwambia.

Nakumbuka uliniambia kwamba mwezi uliopita ulikuwa wa 13 darasani na mwezi huu umepanda na kuwa 7. Hizi ni Habari njema na za kufurahisha. Nataka nikwambie kitu kimoja mdogo wangu, kwenye mitihani yako mtu pekee unayepaswa kushindana naye ni wewe mwenyewe. Yaani shindana na wewe wa jana. Unajua huko shuleni walimu wanawaambia mshindane na wenzenu kitu ambacho kitakupa ugonjwa ambao unaua watu wengi ugonjwa huo unaitwa kujilinganisha. Kaka yako niliacha kushindana na watu darasani toka kidato cha pili na imenisaidia sana na sijawahi kufeli (labda niongezee).

Kuna jamaa mmoja nilisoma naye shule ya upili (kidato cha tano na sita) kila matokeo yalipotoka alizoea kujilinganisha na wengine, aliumia sana alipoona mtu fulani kamzidi wakati yeye alikua akitoa sana, nilikuja kukutana naye chuo bado ana tabia hiyo hiyo, utakuta analalamika ana G.P.A ya 4, kuna siku kidogo nimtwange kofi mimi nina G.P.A yangu ya 2.8 na nina furaha yeye na GPA ya 4 analalamika kafanya vibaya. Jitahidi sana kuepuka marafiki  wanaolalamika sana. Watu wa namna hii hata ufanyeje huwa wanaona hasi kila kitu.

Hakikisha unajipa changamoto ya wewe kuwa bora kuliko ulivyokuwa jana kila wakati hii itakusaidia utakapomaliza masomo yako na kuja huku mtaani. Huku maisha hayahitaji mashindano bali yanahitaji ushirikiano. Ni kama timu ya mpira, ili ushinde mechi lazima wachezaji wote washirikiane kuanzia golikipa, uje kwa mabeki, kwa mawinga hadi kwa wafungaji.

Jitahidi pia uwasaidie wenzako kwenye vipindi unavyoelewa kuliko wao, usiache kuwasaidia ukiogopa kwamba watakuja kukuzidi, ukiwa na roho ya hivyo nina wasiwasi na maisha yako ya baadae. Unajua nini mdogo wangu, huwa tunafanikiwa kwa kuwainua wengine.

Sikia Edgar, chochote unachokifanya ni uwekezaji ni kama kupanda mbegu, ukipanda mbegu nzuri utavuna mavuno safi. Kuwa mwema kila wakati na kwa kila mtu, bila kujali umri au kipato, itakusaidia sana. Usimkatie tamaa, mtu yeyote. Miujiza hutokea kila siku.

Nayapenda sana maneno haya ya Maya Angelou aliposema, “Watu watasahau ulichosema, watu watasahau ulichofanya, lakini watu hawatasahau jinsi ulivyowafanya wajisikie.”  

Kabla sijaanza kukuandikia barua hii nilikuwa nasoma Makala ya Tajiri toka Zimbabwe na mmiliki wa kampuni ya Econet ameandika hivi, “Usije ukafanya kosa hili. Kuna watu wengi wanaojiambia wenyewe ‘Nikipata pesa nyingi, nitakaa chini na kuanza kuwasaidia wengine’ ngoja nikwambie siri: Hawajawahi fanya hivyo! Na sehemu kubwa ya kujitoa sio pes ani muda. Na kila mtu ana muda kama mwingine, sisi wote ni mabilionea wa muda” Jitahidi utumie muda na nafasi uliyo nayo utafanikiwa sana.

Hivi Edgar, ulinunua kile kitabu cha Ben Carson cha THINK BIG nilichokwambia ununue? Jana jioni nilikuwa nasoma kitabu hicho na kama unakumbuka kwenye barua yangu ya kwanza nilikwambia umtegemee Mungu katika kila jambo, Carson anasema, “Mungu anajali kila eneo la maisha yetu na huwa anatutaka tumuombe msaada.” Ndipo nikarudi na kukumbuka maneno ya mfalme mwenye hekima sana aliyewahi kuishi aliposema, “Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, kabla hazijaja siku zilizo mbaya, wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo.” (Mhubiri 12:1)

Tena nimekuja kugundua, mimi na Ben Carson hatupishani sana. Aliandika kwenye kitabu chake akisema, “Naianza kila asubuhi na sala na kusoma Biblia, mara nyingi kitabu cha Mithali. Nasali na kusoma Mithali kila jioni.” Nafikiri unakumbuka mara ya mwisho nilikuambia usome mithali kila siku, leo nakuongezea vitabu vya Mhubiri na Joshua Bin Sira, visome upatapo muda.

Katika wiki iliyopita nilibahatika kukutana na Shlomo Sivan toka Israeli ambaye sasa tumekuwa marafiki. Kila siku huwa nakusisitiza ufahamiane na watu wengi, kutana na watu wakukutanishe na watu, ndipo utapata madili. Hakuna atakayekupa dili kama hakufahamu wala hakuamini, hakuna!

Sivan anamiliki kampuni ya kutengeneza programu za kompyuta wanazotumia wahandisi ujenzi, kampuni yake inaitwa Sivan Design ikiwa na makao yake makuu nchini Israeli lakini ana matawi katika nchi za Uganda, Zambia, na Nigeria, sasa anataka kuleta ofisi Tanzania na Ethiopia. Rafiki yangu huyu alinionesha kitu kinachoitwa GIS nilipenda sana hicho kitu kwa maana nilikuwa nasikia kina Spezos wakieleza ila niliona jinsi GIS inavyofanya kazi kwenye miradi kama ya umeme na maji. Ama kweli “Kuna mambo mengi bado ya kujifunza” hayo yalikuwa maneno aliyonambia mzungu huyu. Ndiyo maana huwa nakwambia usiende kulala bila kujua umejifunza nini kwa siku husika, hata kama ni jambo dogo wewe jifunze tu. Elimu ni bahari, wahenga walisema.

Rafiki yangu huyu hakuishia hapo aliniambia Habari za binti yake wa miaka 15 ambaye hadi leo hii amejifunza vitu vingi na ameweza kuvimudu. Anasema binti yake alijifunza kutengeneza Cocktail (Hiki kinywaji najua hujawahi kunywa lakini kwasababu ya umri wako siku moja nitakuonjesha Mocktail walau utapatapata kujua jinsi cocktail ilivyo) kupitia Youtube na sasa anatengeneza Cocktail za viwango vya juu. Si hilo tu binti huyo alitaka kujifunza kucheza muziki ndani ya miezi 2 alikuwa akitumia saa 2 kila siku jioni kujifunza, leo hii ni mnenguaji mzuri.

Unajua Sivan aliniambia nini? Mwanae anaweza kujifunza vitu vingi kwa sababu ya kuwa na nia, kudhamiria na kufokasi. Ukiweza pia kuwa na hivyo vitu vitatu nilivyotaja hapo juu mdogo wangu hakuna kitu kitakachokutatiza kujifunza chochote.

Natamani siku moja ukija mjini nikukutanishe na marafiki zangu ambao waliamua kujifunza mambo peke yao na sasa hivi wanaishi huku mjini kwa hayo mambo waliyojifunza.

Nilimuuliza pia Sivan amewezaje kuwa na kampuni kubwa kiasi kile inayotoa huduma dunia nzima, majibu yake yalikuwa haya; tengeneza bidhaa nzuri na watu watakuja kununua na pili tatua matatizo magumu na watu watakuwa tayari kuingia mifukoni mwao na kukupa pesa zao.

Mdogo wangu, leo nimekuandikia mengi, natamani niendelee lakini nikupe mwanya na wewe kuyatafakati maneno haya na kuyafanyia kazi.

Usisahau kuitunza barua hii kwenye faili lako, umalizapo kuisoma.

Nakutakia masomo mema. Kwa kheri!

 

Nakupenda sana mdogo wangu,

Kaka Yako,

Edius Katamugora. 

Hii ni blogu rasmi ya Edius Katamugora, hapa utajifunza maendeleo binafsi, utapata makala mbalimbali zinazohusu biashara, elimu, hamasa na maisha kwa ujumla. Karibu sana katika blogu hii.

0 comments: