Thursday, 3 August 2017

Kama Umetegwa Na Ulichosema Umenaswa Na Maneno Ya Kinywa Chako

KUTOKA KITABU CHA BARABARA YA MAFANIKIO



Unapoamka asubuhi jinenea maneno mazuri juu yako, mimi nimebarikiwa, mimi ni jasiri, mimi ni mzuri, mimi ni mkarimu, mimi ni mwenye busara na hekima, mimi ni mchapakazi, mimi ni mwenye uwezo na akil, mimi ni mwenye vipaji rukuki kutaja machache. Ukianza kujinenea maneno mazuri kama hayo unavutia akili zako kama unavyojinenea. Wahenga wanasema ‘’ Maneno huumba,’’.

Wewe ni mtu wa pekee sana katika uumbaji wa Mungu ndio maana katika mamilioni ya watu duniani umepewa alama za vidole tofauti yaani unazo wewe peke yako. Ndio maana nasema wewe ni wa pekee. Sauti uliyonayo wewe hakuna mtu mwingine mwenye nayo ingawa kuna wakati utasikia watu wanakwambia sauti yako inafanana na ya mtu mwingine lakini kiuhalisia sio kweli. Kabla ya wewe kuzaliwa na wazazi wako, Mungu alikwisha kuumba wewE kichwani mwake na kukufanya kiumbe chake kizuri haswa.

Je kwanini tunajinenea maneno mabaya?. Unakuta mtu anasema; ‘’ Mimi ni mbaya, mimi ni muoga, mimi sina akili, mimi sina kipaji, mimi ni mzee,’’. Unavyonena juu yako ndivyo unavyojivutia kuwa. James Allen mwandishi wa vitabu aliwahi kusema ‘’ As a man thinketh, so he is,’’ akimaanisha ‘’ Jinsi mtu anavyofikiri ndivyo anavyokuwa,’’. Kuna nguvu Fulani inayokusukuma kuelekea kule unakonena.
 Ukisema mimi sina akili, hutawahi hata siku moja kufanya vizuri darasani, ukisema mimi sina akili, hutowahi kuwa jasiri hata siku moja, ukisema mimi sina kipaji hutowahi kuona vifurushi vya vipaji vilivyo ndani yako. Uchunguzi uliofanyika unaonesha kwamba kila mtu anazaliwa na uwezo na vipaji kuanzia 500-700, lakini wewe ukikazania kusema mimi sina kipaji huwezi kuona hata kimoja kati ya vipaji 500-700. Ukisema mimi ni maskini wa kutupwa kweli utabaki kuwa maskini wa kutupwa, ukisema mimi ni mzee, hata kama una miaka 35, utaona tu mvi zinajileta kichwani mwako na uso unakunjamana.

Jifunze kujinenea maneno mazuri kila mara hasa unapoianza siku mpya. Maneno unayoongea au kunenena juu yako, hayaongelei wakati wa sasa yanaongelea wakati ujao. Ndio maana huwa napenda kusema ‘’ Usitazame tu pale chini ulipo, tazama na juu unapoweza kuwa,’’.

Maneno ni kama umeme ambao ukiutumia vizuri utakusaidia kufanikisha mambo yako lakini ukiutumia vibaya na bila tahadhari utakulipukia. Hii ndiyo maana halisi ya maneno. Ukijinenea vitu vizuri mambo mazuri yatafuata njia yako na ukijinene mambo mabaya mambo mabaya yatakujia.
Kuna watu wengine hadi leo hii wanafikiri na kuyabeba vichwani yale waliyoambiwa na wazazi, ndugu, marafiki, wafanyakazi wenzao, walimu na watu wengine ya kwamba wao hawawezi, hawana adabu, hawana akili, ni waoga, ni wasumbufu. Na bado wanayabeba vichwani mambo ambayo hadi leo yanawaathiri. 

Kuna mtu mmoja akiwa madarasa ya chini mwalimu wake alimfukuza shuleni na kumuandikia ujumbe uliosomeka ‘’ Mwanao hana akili na hawezi lolote hivyo tumemwondoa shuleni,’’. Mama yake baada ya kuupokea ujumbe hule na kuusoma alijibu ‘’ Nitamfundisha mwenyewe,’’. Leo hii mtu huyu ndiye Edison Thomas ambaye ndiye aliyegundua taa ya umeme inayowaka. Wengi wanamuita baba wa umeme duniani. Watu wakibeba maneno mabaya juu yako maneno hayo yapite sikio moja na kutokea sikio la pili, usikubali kuyaweka kichwani  kwako. Jibariki leo na neno zuri mbele ya maneno haya ‘’ Mimi ni………,’’.

"We are snared by the words of our mouth." (Proverbs 6:2) "Kama umetegwa kwa ulichokisema, umenaswa kwa maneno ya kinywa chako." (Mithali 6:2)

Kupata nakala ya kitabu hiki unaweza kuwasiliana nami, kupitia 0764145476 ili uweze kujifunza zaidi.
"Mafanikio yapo mikononi mwako."

Ndimi
EDIUS KATAMUGORA
AUTHOR AND MOTIVATIONAL SPEAKER
0764145476
0625951842 (WHATSAPP)

Imani yangu ni kwamba mafanikio ni kitu cha kushirikishana, mshirikishe na rafiki yako kile ulichojifunza.

Usisahau kijipatia nakala ya kitabu changu kizuri cha BARABARA YA MAFANIKIO.

Hii ni blogu rasmi ya Edius Katamugora, hapa utajifunza maendeleo binafsi, utapata makala mbalimbali zinazohusu biashara, elimu, hamasa na maisha kwa ujumla. Karibu sana katika blogu hii.

0 comments: