Thursday, 9 November 2017

"Chuo Bata." Msemo Unaowapoteza Wanavyuo Wengi

Nilipokuwa nasoma kidato cha tano ndipo ilipokuwa mara yangu ya kwanza kusikia msemo uliokuwa ukivuma ambapo watu walikuwa wakisema "Chuo Bata."
 
Akili yangu ikakubaliana na neno hilo nikajua kweli hasa kwamba chuo ni sehemu ya kula bata. Ni sehemu ya kustarehe na kula kuku kwa mrija.

Muda ulifika wa Mimi kuwa mwanafunzi wa chuo. Jambo la kushangaza niliona picha tofauti ya kile nilichokitegemea. Niliona tofauti ya kile ambacho wengi walikiita "Chuo Bata." Ukweli ni kwamba chuo sio bata. Ukiendekeza bata chuoni maisha lazima yakupige picha. Rafiki yangu JJ sikuzote huniambia "Namtafuta huyu mtu aliyeanzisha msemo wa chuo Bata." 

Sasa hivi wakati vyuo vingi vimefunguliwa tena wengine wakianza mwaka wa kwanza. Kama kuna mtu alikudanganya kwamba chuo ni bata, futa hayo mawazo.  Maana ipo siku yatakuja kukukwamisha.

                                    
                              
Kama wenzako wakiendeleza kula bata wewe achana nao Fanya mambo yafuatayo ipo siku mtaongea kwa lugha tofauti. Ndiyo maana wakati naandika kitabu cha Barabara Ya Mafanikio nilikipa jina la "Mafanikio yako mikononi mwako.":

1. Weka nidhamu  mstari wa mbele:
 
Hapa namaanisha nidhamu binafsi kwako mwenyewe maana wahenga walisema "Jiheshimu, utaheshimiwa." Na pia nidhamu kwa watu.

==> Nidhamu juu ya matumizi ya muda: acha kutumia muda wako vibaya kwenye mitandao ya kijamii, kuangalia series na kubet. "Ukitaka kujua thamani na umuhimu wa mwaka mmoja muulize mwanafunzi aliyerudia darasa." Anasema Dr. Fr. Faustin Kamugisha

==> Nidhamu juu ya matumizi ya pesa: kama ndio unapata bumu usitumie pesa yako vibaya. Usitakae kufanana na kina Beyonce na Chris Brown kwa laki tano. Anza kuweka akiba. Pili usitake kumfurahisha kila mtu. You can never please everyone. "Sizifahamu siri zote za Mafanikio, lakini nafahamu kwamba ukitaka kushindwa, anza kumfurahisha kila mtu." Anasema Rick Warren mwandishi wa kitabu cha The purpose of driven Life

2. Tumia walau dakika 30-60 ukijifunza mambo ya kitivo (faculty) yako kila siku. Hii ndiyo kanuni wanayoitumia wataalamu unaowaona na kukutana nao katika sekta mbalimbali. Walatini wanasema "Repetitio Est Mater Studiorum." Wakimaanisha "Marudio ndiye mama wa kujifunza." "Repetition is the mother of studies."

3. Tafuta mshauri (Mentor) wa masomo yako. Huyu atakusaidia namna ya kupambana na changamoto mbalimbali hasa za kazi unayoisomea na pia atakuwa mhamasishaji mkubwa kwenye masomo yako.

Kama unasomea ualimu tafuta mwalimu aliyeko kazini.
Kama unasomea uhandisi tafuta mhandisi aliyeko kazini.
Kila unachosomea tafuta mtu anayefanya kazi unayotaka kuifanya hapo mbeleni ili awe mshauri wako.


SOMA: TAA NANE ZINAZOWAMULIKA WANAFUNZI WA VYUO NA WAHITIMU WA VYUO.

4. Onesha na endeleza kipaji chako. Hakuna muda mzuri wa kuonesha na kuendeleza kiapaji chako kama muda wa masomo ya chuo.
Wengine wanasema "Hakuna muda," lakini chuo muda upo wa kutosha. Wenzio wakienda bata wewe endeleza kipaji chako, wenzio wakienda kuangalia Mpira na series wewe jikunje na endeleza kipaji chako. Amka mapema tena lala ukiwa umechelewa. Ipo siku mtaongea kwa lugha tofauti.

5. Soma vitabu na makala mbalimbali.
Hapa simaanishi vitabu vya darasani bali namaanisha vitabu vinavyoelezea na kufundisha kuhusu maisha ya kila siku. Vitabu vinavyohusu maendeleo binafsi (self-development, self help books and motivational books), vitabu vinavyohusu biashara, ujasiriamali na kadhalika. Kumbuka pia siongelei vitabu na makala za udaku.

Watu wanaosoma computer programming wana msemo unaosema "Garbage in, garbage out." Yaani uchafu unoaingiza ndani ndiyo uchafu utakaoutoa. Ukiingiza program vibaya lazima upate majibu tofauti. Ukisoma habari za udaku na umbea ni wazi kwamba hata stori zako zitakuwa za umbea.

Uchunguzi wangu mdogo umenionesha kwamba wasomi wengi hasa walioajiriwa hawapendi kabisa kusoma vitabu lakini mabosi wao wanapenda sana kusoma vitabu. Usipotaka kusoma vitabu na kujifunza utaendelea kuwa na mawazo yaleyale miaka nenda rudi na bosi wako ataendelea kukutawala
.
Stephen Covey mwandishi maarufu wa kitabu cha "The 7 Habits Of Highly Effective People" aliwahi kusema "Ujuzi wa mtu hupotea kila baada ya miaka miwili." Kama hautakuwa tayari kujifunza kwa kusoma vitabu na makala mbalimbali jiweke tayari kupoteza ujuzi wako na hautakuwa na soko tena.

Watu wote unaowaona wamefanikiwa ni wasomaji wazuri wa vitabu. Ni watu wanaopenda kujifunza kila siku.
 
Oprah Winfrey anajulikana kwa kusoma kitabu cha "Think and Grow Rich" cha Napoleon Hill mara 13 mfululizo kabla ya Mafanikio yake.
 
Warren Buffet tajiri namba 3 na mwekezaji namba moja duniani, yeye hutumia robo tatu ya muda wake kusoma Vitabu.
 
Mwl. Julius K. Nyerere aliacha maktaba yenye vitabu zaidi ya 8000.
 
Tupac Shakur alisoma vitabu zaidi ya 1000. Kumbuka kuyafanyia kazi yale unayoyasoma. Usisome ilimradi tu na wewe uonekane unasoma vitabu.

Kwenye kitabu cha Barabara Ya Mafanikio nimeelezea zaidi kuhusu umuhimu wa kusoma vitabu. Unaweza kujipatia nakala 
yako kwa mawasiliano yangu hapo chini ya makala hii.

7. Badili mtizamo wako. Badilisha namna ya kuona chuo kama sehemu ya kula bata. Ukibadili unachofikiri, utabadili unachokiona na utapata matokeo tofauti. Beba asilimia mia ya majukumu yako yote. Mhamasishaji Jim Rohn aliwahi kusema "Huwezi kuomkodisha mtu akupigie PUSH-,UP zako."

8. Jifunze namna ya kuwasiliana (Endeleza namna yako ya kuwasiliana) ( Develop your communication skills):
Jifunze namna ya kuongea mbele za watu, hasa wanadarasa wako. Ongea vizuri na watu. Maana hapa utajifunza kitu kinachoitwa "Customer care." "Ukifungua kinywa chako" anasema mhamasishaji Les Brown "Unaiambia dunia wewe ni mtu wa namna gani."

"Uwezo wa kuongea na kuwasiliana vizuri umekuwa zawadi kubwa kwa wahitimu wa vyuo wanapoombwa kuongelea kitu Fulani wakati wa usaili," anasema Stephen E. Lucas mwandishi wa kitabu cha "The Art Of Public Speaking."

"Umuhimu wa ujuzi wa kuwasiliana ni muhimu kwa wasanifu majengo, wachumi, walimu na wanasayansi. Hata wale waliokuwa wataalamu katika mambo kama ya uhandisi wa ujenzi (Civil Engineering) na uhandisi wa ufundi mitambo (Mechanical Engineering) mwajiri anahitaji namna unavyoweza kuwasiliana katika kuonesha ufundi stadi wako," anamalizia Stephen E. Lucas.

9. Tafuta plan B. Usifikirie kuajiriwa, fikiri kujiajiri badala ya kufikiri kuajiriwa. Takwimu za sensa ya mwaka 2012/
zinaonesha kwamba kila mwaka huhitimu wanafunzi milioni mbili huku wakiajiriwa watu laki mbili tu kila mwaka. Je una uhakika wa kupata ajira kwenye hao milioni mbili? Jiulize tu darasa lenu mpo wangapi, pili angalia Tanzania nzima watu wanaosoma kile unachosomea ni wangapi?

SOMA: MWANACHUO FIKIRIA NJE YA BOX

Miaka ya 1965 baada ya uchumi wa Marekani kukua kwa kuwepo kwa viwanda vingi. Zilipatikana ajira milioni 7000 huku viwanda vyote vikitoa ajira milioni 400 tu (Chanzo: Kitabu cha Innovation and Entrepreneurship kilichoandikwa na Peter F. Drucker). Kumbe hata viwanda vikijengwa vingapia Tanzania vitapunguza asilimia kidogo tu ya tatizo la ajira.  Tafuta plan B, fikiria nje ya boksi.

"Mafanikio yako mikononi mwako."

Ndimi:
Edius Katamugora
Mwandishi na Mhamasishaji
0764145476
0625951842 (WhatsApp)
email; ekatamugora@gmail.com
Instagram: ediuskatamugora

Imani yangu ni kwamba Mafanikio ni kitu cha kushirikishana. Mshirikishe na rafiki na ndugu yako kile ulichojifunza.

Karibu kujipatia kitabu cha Barabara Ya Mafanikio kwa bei ya shilingi 6000/= tu. Tuwasiliane 0764145476/ 0625951842.

Hii ni blogu rasmi ya Edius Katamugora, hapa utajifunza maendeleo binafsi, utapata makala mbalimbali zinazohusu biashara, elimu, hamasa na maisha kwa ujumla. Karibu sana katika blogu hii.

1 comments:

Songambele said...

Hii ni Makala ya mwaka. Kama walengwa wataisoma vizuri basi mambo yatabadilika sana huyo mbeleni.