Thursday, 28 December 2017

Andika Jina Lako Vizuri

Jina zuri ni sawa na kuchimba dhahabu kwenye ardhi yenye bahari ya madini. Utaendelea kuchimba siku zote.
   ~Edius Katamugora ~

Alexander Gramahbell anafahamika kwa kuwa mtu aliyegundua simu.

Mama Theresa wa Calcutta anafahamika kwa kuwa mama Mwenye upendo mkubwa wa kuwahurumia na kuwahudumia wakoma nchini India.

Mark Zukerberg anafahamika kama mwanzilishi wa Facebook.

 

Bill Gates na Paul Allen wanafahamika kama waanzilishi wa Microsoft.

Steve Jobs anafahamika kama mwanzilishi wa kampuni ya Apple.

Nelson Mandela anafahamika kama mkombozi wa Afrika au wengine wanamwita Simba wa Afrika.

Hao ni baadhi ya watu walioandika majina yao vizuri. Ni watu walioishi na wanaoishi maisha ya kuacha alama.

Kuandika jina lako vizuri sio kwamba jina lako limekosewa au unahitaji kalamu na karatasi hiyo sio kweli.

Watu wanaoandika majina yao vizuri ni watu wanaojitoa kwa namna ya pekee. Ni watu wanaofanya mambo ya kuishangaza dunia. Ni watu wanaokwenda hatua ya ziada. Ni watu wanaoacha historia yenye mchango mkubwa katika jamii.

Katika kitabu cha Tatizo Si Rasilimali tulizozipoteza mwandishi Godius Rweyongeza  anasema "Tukimtaja Ronaldo , Mbwana Samatta na Messi picha inayokuja kichwani ni mpira. Je likitajwa jina lako picha inayokuja kichwani ni ipi.?."

Hili ndilo swali analoliuliza mwandishi huyo akitaka kwa jicho la pekee tuweze kuandika majina yetu kwa kalamu zenye wino usiofutika.

Kuandika jina lako vizuri ni nini?

Kuandika jina lako vizuri ni kugusa mioyo ya wengine ni kuwasaidia wengine. Oprah Winfrey aliwahi kusema "Hakuna alama nzuri kama kugusa mioyo ya watu wengine." Naye mwandishi Zig Zigllar akaongeza na kusema 'Utapata chochote unachohitaji kama utajitoa kuwasaidia wengine wapate wanachohitaji." Andika jina lako kwa kuwasaidia wengine. Wasaidie watu wanaokuzunguka.

Kuandika jina lako vizuri ni kufanya kazi kwa bidii; Henry Ford aliwahi kusema "Unapofanya kazi kwa bidii ndipo watu wengine huiita bahati." Ukweli ni kwamba bidii haijawahi kumwangusha mtu yeyote. Nilipikuwa nikisoma Historia ya maisha ya Bill Gates Tajiri namba moja duniani niligundua kwamba kuna wakati ilimpasa alale kwenye chumba cha kompyuta akijifunza kuandika kodi mbalimbali zinazotumika kuandaa programu mbalimbali.

Andika jina lako vizuri kwa kutumia kipaji chako: watu waliofanikiwa sana ni watu wanaotumia vipaji vyao. Ukitumia kipaji chako utaifurahisha dunia lakini pia utakuwa mtu mwenye furaha na amani. Usikubali leo kuficha kipaji chako. Dr. Myles Munroe aliwahi kusema "Utajiri mkubwa huko makaburini watu walikufa na ndoto na vipaji vyao." Hakikisha hauendi kuufaidisha udongo na kipaji chako wakati dunia haijui lolote kuhusu wewe.

Kuandika jina lako vizuri ni kukubali kubadilika. Ninaposema unahitaji kuandika jina lako vizuri namaanisha pia unahitaji kubadili tabia ulizonazo na kuzifanya tabia zenye mfano mkubwa katika jamii inayokuzunguka. Bwana Grant Cardone alikuwa mtu aliyejihusisha katika utumiaji wa madawa ya kulevya aliyepindukia. Baada ya kujitafakari na kuona amepotea kama mwana mpotevu aliacha kutumia vilevi na kuvuta bangi. Leo hii Grant Cardone ni mwandishi maarufu wa vitabu na mshahuri wa maswala ya biashara. Jiulize je tabia zangu zinanisaidia kuandika jina langu vizuri au zinaliharibu.

Kuandika jina lako vizuri ni kufanya yale wengine wanaona hayawezekani na kuyafanya kweli.
Kuna mtu aliwahi kusema "Inauma sana pale unapoona mtu akifanya yale ambayo ulisema hayawezekani." Bwana Thomas Edson baada ya kushindwa Mara 1000 aliweza kugundua balbu ya umeme na leo hii anajulikana kama baba wa umeme. Inawezekana leo hii tusingelikuwa na Umeme kama Edson angelikata tamaa. Kumbe kukata tamaa ni kuacha kuandika jina lako vizuri. Kukata tamaa ni sawa na kuacha kupanda chombo cha usafiri wakati una ndoto za kwenda mahali.

Kuandika jina lako vizuri ni kutatua matatizo makubwa. Dunia ya leo inakosa watu wanaotatua matatizo makubwa katika jamii zinazotuzunguka. Mwanamuziki mmoja aliwahi kusema "Kwangu mimi matatizo umaanisha utatuzi." Akitaka kuonesha matatizo yapo ili yatatuliwe. Ukitaka kuwa mtu mkubwa hakikisha unatatua matatizo makubwa. Tatizo kubwa ni kwamba jamii zinazotuzunguka zimekabiliwa na ulalamikaji wa hali ya juu. Mpendwa msomaji hakikisha watu wanapolalamika wewe unasikiliza malalamiko yao na kuwa mtatuzi na si mmoja wa walalamikaji.

Andika jina lako vizuri kila mahali ulipo.

"Mafanikio yako mikononi mwako."
Ndimi:
Edius Katamugora
Mwandishi na Mhamasishaji
0764145476
0625951842 (WhatsApp)
Email: ekatamugora@gmail.com

Jipatie kitabu cha Barabara Ya Mafanikio kwa Shilingi 6000 tu.
Washirikishe na wenzako kile ukichojifunza.

Hii ni blogu rasmi ya Edius Katamugora, hapa utajifunza maendeleo binafsi, utapata makala mbalimbali zinazohusu biashara, elimu, hamasa na maisha kwa ujumla. Karibu sana katika blogu hii.

0 comments: