Monday, 22 January 2018

Badili Mawazo Yako Kuhusu Mahali Ulipo

                                
















"Hakuna kitu kizuri au kibaya
               Lakini kufikiri hufanya kitu kiwe kizuri au kibaya."
                                  ~William Shakespeare~

Huko Amerika ya Kusini nchini Paraguay kuna kijiji kimoja kinachojulikana kama Cateura. Hii ni sehemu iliyofanana kabisa na uswahili ambayo imezungukwa na dampo kubwa sana. Kila mahali kila kona ndani ya kijiji cha Cateura ni uchafu tu umezagaa.

Cateura inazofamilia takribani 2500 zinazoishi maeneo hayo ambapo  watu wengi wanaoishi maeneo hayo wanaishi kwa kuchukua takataka zilizotupwa katika dampo hilo na kizirudisha katika matumizi ya kawaida.

Ripoti ya mwaka 2010 ya UNICEF kuhusu Cateura inasema zaidi ya tani 1500 za taka hutupwa katika eneo hilo kila siku. Watu wengi si wasomi katika eneo hilo. Watoto wa Cateura ndio hukusanya takataka katika eneo hilo na kwenda kuziuza. Maji katika eneo hilo si salama kabisa, siku za mvua mji unafurikwa na maji yaliyoambukizwa na yenye vijidudu na bacteria.

                      
                

Sikumoja Favio Chavez, mtaalamu wa mazingira alikuwa na wazo la kushangaza, wazo la kuwapa watoto kitu ambacho hawakuweza kukipata. Kitu hicho ni kucheza muziki katika bendi. Ingawa alikuwa amefundishwa kama mwanamuziki na alikuwa amewahi kuanzisha vikundi vya muziki hapo nyuma, alijua kwamba familia nyingi,ikiwezekana hakuna hata moja ambayo ingeweza kununua kifaa cha muziki. Ambapo anasema hata tarumbeta lina thamani zaidi ya nyuma.

Baada ya kukaa na kufikiria aligundua yakwamba suluhisho lilikuwa ndani ya mikono yake. Dampo lile lilikuwa na vitu vingi ambavyo vingeweza kutumika kutengeneza vifaa vya muziki. Hivyo kutoka katika dampo hilo waliweza kutengeneza ngoma, gitaa, tarumbeta n.k

"Siku moja nilianza kuwafundisha muziki watoto wanaookota taka damponi nikitumia vifaa vyangu." Anasema Chavez  "Lakini nilifikia hatua wanafunzi wakawa wengi ndipo nilipoamua na kujaribu kuanza kutumia wachache." Hapo ndipo Chavez alikuwa na nguvu za kusema "Dunia inapotutumia takataka, sisi tunairudishia muziki."

Huo ndio ukawa mwanzo wa kutengeneza bendi kutoka katika dampo. Leo hii bendi huyo inaowatumbuizaji wapatao 30, wakizunguka dunia kutoka burudani katika nchi za Argentina, Brazil na Ujerumani.

"Nilitengeneza bendi hii kuifundisha dunia na kuongeza uelewa lakini pia ni meseji kwa jamii kuwajulisha kwamba ingawaje wanafunzi hawa wapo katika umaskini  wa kutupwa, wanaweza kuchangia kitu katika jamii. Wao pia wanahitaji fursa." Anamalizia Favio Chavez

Inawezekana Leo hii unawaza na kufikiri kwamba mahali ulipo Leo sio mahali sahihi kwako. Familia uliyozaliwa sio familia sahihi, mkoa, nchi, mtaa, kijiji sio sehemu sahihi kwako. Kazini ulipo sio mahali sahihi, shule ulipo, sio shule sahihi, chuo unachosoma, sio chuo sahihi. Masomo unayosoma sio masomo sahihi.

Jua kwamba mahali ulipo katika maisha yako sasa panapita lakini ni mahali ambapo ulipaswa kuwa. Umefikia hatua uliyopo ili ujifunze yale unayotakiwa kujifunza, ili uwe mtu anayetengeneza maisha ambayo unayataka.

Hata kama maisha ni magumu na yenye changamoto, tena maisha yanapokuwa magumu na yenye changamoto ni fursa kwetu kujifunza na kuwa vizuri zaidi ya tulivyokuwa hapo nyuma.  Hupo katika hatua ya kuandika historia ya maisha yako na hakuna stori nzuri isiyokuwa na shujaa ambao wamekumbana na changamoto na kuzitatua. Ukweli ni kwamba jinsi changamoto inavyokuwa kubwa ndipo stori yako inavyozidi kuwa nzuri zaidi.

Leo hii unahitaji kuwa kama watoto wa Cateura, dunia inapokutumia takataka, wewe unairudishia muziki. Watu wakiweka vizingiti katika kazi yako, usiichukie kazi yako. Fanya zaidi ya hapo. Shule uliyopo hata kama haijawahi kufaulisha mwanafunzi hata moja , sema mimi nitakuwa mtu wa kwanza kutengeneza historia ya shule hii.  Masomo unayosoma watu hata wakisema ni magumu kiasi gani usikate tamaa na kuona huwezi kuyafaulu, soma zaidi, soma  vitabu vingi, tizama video nyingi zinazofundisha somo lako. Kumbuka ni yaleyale maji ya moto ambayo hukifanya kiazi kiwe laini na pia kulifanya yai kuwa gumu.

Mahali ulipo ni mahali sahihi, badilisha picha na fikra za mahali ulipo. Piga picha nzuri ya mahali ulipo. Wakati dunia inaona taka na kuzitupa Cateura, Favio Chavez yeye aliona bendi ya muziki. Zig Ziglar alisema "Picha unayoichora katika akili yako utaifanyia kazi ili kuifanikisha. Unapobadili picha zako unabadili na utendaji."

Inawezekana unachukia na kuona umezaliwa na wazazi Fulani au katika familia ya kimaskini. Mungu alifanya hivyo makusudi ili wewe uwe mtu wa kuibadili familia yenu kutoka katika Lindi la umaskini wa kutupwa na kuipeleka katika utajiri. Hahitajiki mtu mwingine bali ni wewe. Ndiyo maana Bill Gates aliwahi kusema "Kuzaliwa maskini sio kosa lako. Kufa maskini ni kosa lako." Badili Leo mawazo yako kuhusu familia yako.
Badili mawazo yako kuhusu nchi yako. Badili mawazo yako Leo, kuhusu kazi yako. Badili mawazo yako kuhusu shule yako.

Jaribu kuwa na fikra chanya kama alivyokuwa Favio Chavez na kuibadili dunia yako ya mahali ulipo. Inawezekana dunia inakutumia takataka kama walivyokuwa watu wa Cateura. Je wewe umewahi kufikiri namna ya kuzigeuza taka hizo na kuirudishia dunia muziki?

         "Muda mwingine unaweza kufikiri, umezikwa, kumbe          umepandwa."
                             ~Edius Katamugora ~

Mafanikio yako mikononi mwako

Ndimi;
Edius Katamugora
Mwandishi na mhamsishaji.
0764145476
0625951842 (WhatsApp)
Email: ekatamugora@gmail.com
Instagram; ediuskatamugora

Jipatie kitabu cha Barabara Ya Mafanikio kwa shilingi 6000/= Mawasiliano hapo juu.

Imani yangu ni kwamba mafanikio ni kitu cha kushirikishana. Washirikishe na wenzako kile ulichojifunza.

Hii ni blogu rasmi ya Edius Katamugora, hapa utajifunza maendeleo binafsi, utapata makala mbalimbali zinazohusu biashara, elimu, hamasa na maisha kwa ujumla. Karibu sana katika blogu hii.

0 comments: