Wednesday, 7 February 2018

Namna Ya Kuwa Mtaalamu Ukiwa Bado Unasoma (How to become an Expert While At School)

Kila mtu unayemuona ni mtaalamu katika eneo fulani kuna siku alikua ni mtu mpya kwenye kitu hicho ambacho Leo hii kinamfanya aonekane mtaalamu.

Kitu cha kwanza muhimu katika kufanya jambo lolote ni kuchukua hatua. Na hatua muhimu ya kuchukua ni hatua ya kwanza. Watu wengi hukosa nguvu za kuchukua hatua na hivyo hujikuta miaka nenda rudi unawakuta pale pale. Hawa ni watu wanaosema nitafanya hivi kila kukicha huku hawafanyi lolote.

Kuna mambo unatakiwa kuanza kuyafanya ili kuwa mbobezi/gwiji katika taaluma au kipengele fulani kama bado unasoma.

Mambo hayo ni yafuatayo;

1. Tafuta somo unalolipenda;

Moja wapo ya misemo yangu ni "Hakuna shule au chuo kitakachokwambia Fanya mambo unayoyapenda (follow your passion), lakini watu waliofanikiwa kimaisha ni watu waliofanya mambo wanayoyapenda.

                                   
 
Takwimu zinaonesha kwamba watu wengi hawana furaha na kazi wanazozifanya kwasababu tu wanafanya kazi wasizozipenda. Ukifanya kitu usichokipenda sio rahisi kufanikiwa.

Nisikuchoshe turudi kwenye makala yetu. Ukichagua somo unalolipenda hakikisha kila siku iitwayo leo unalisoma hata kama umebanwa namna gani. Soma vitabu vingi uwezavyo nenda zaidi ya mwalimu wako anavyofundisha kwa maana unatafuta ugwiji. 

Ingia YouTube jifunze mengi ambayo huyaelewi kupitia huko utajifunza maana hakuna sehemu yenye walimu wengi kama YouTube hivyo imani yangu hawezi kukosa mwalimu utakayemuelewa vizuri.

2. Jitolee.

Hili linaweza kusikika kama jambo geni na la ajabu. Lakini kupitia kujitolea utajifunza mengi na utakuwa tayari umebobea katika sekta fulani na utaweza kujua kazi zinafanywaje. Kuna wakati unaweza kusema mimi sina connection lakini ukienda kujitolea na ukaonesha ujuzi wako wa hali ya juu nakwambia ukweli connections zitajileta zenyewe.  Watu watakutafuta maana dunia ya Leo magwiji ni wachache. Utafurahia ukiwa mmoja wao. Ndio maana huwa napenda kusema "Jiconnect na watu watakuconnect."

Chukua fursa hii Leo anza kujitolea sehemu unapoona unaweza kujitolea mfano, unapokuwa likizo na huna kazi za kufanya nenda sehemu inayohusiana na kitu ambacho siku za mbeleni unahitaji kuwa gwiji na omba kujitolea.

3. Tafuta mshauri (Find a Mentor):

Ukitaka kuwa mtu mtaalamu lazima upitie kwenye mikono ya wengine.

Washauri(mentors) ni watu wazuri kwani tayari wamepitia mengi na wanajua mengi kukiko wewe. Watu wenye hekima hawakukosea waliposema "Kuishi kwingi ni kuona mengi.''

Mshauri atakufundisha mambo mengi ambayo ulikuwa huyafahamu na pia atakuongoza vyema kufika mahali unakotaka kufika. Huyu atakuonesha pia changamoto mbalimbali na namna ya kuzikabili. Usije ukafanya kosa ukawa unasomea kitu fulani na haujawahi hata kuongea na mtu yeyote anayefanyia kazi kitu unachosomea, hutakuwa unajichimbia shimo.

Leo hii kazi ya kufanya, kama hauna mshauri hakikisha unamtafuta na nakuhakikishia utajifunza mengi kutoka kwake. Leo hii mimi nimefika hapa kwa kusimama kwenye mabega ya wengine ambao wamekuwa wakinisaidia bila kuchoka. Wewe pia utafika mbali kwa kusimama katika mabega ya wengine. Hakikisha wakati unasoma kama unataka kuwa gwiji unatafuta mshauri ambaye ni gwiji tayari. 

Hebu tizama hapa, Socrates alimfundisha Plato na Plato alikuwa mwalimu wa Aristotle. Hawa wote Leo hii dunia inawatambua kama wanafalsafa muhimu sana na bado mafunzo yao yanatumika. Amakweli chuma hunoa chuma. 

Unataka kuwa gwiji? Hakikisha unayemshauri na mwalimu wa kukufanya kuwa gwiji.

" Mafanikio yako mikononi mwako."

Ndimi: Edius Katamugora
Mwandishi na mhamasishaji.
0764145476
0625951842 (WhatsApp).
Email: ekatamugora@gmail.com

Jipatie kitabu cha Barabara Ya Mafanikio Kwa shilingi 6000/= tu. Piga 0764145476.

Imani yangu ni kwamba Mafanikio ni kitu cha kushirikishana. Mshirikishe na rafiki au ndugu makala hii.

Hii ni blogu rasmi ya Edius Katamugora, hapa utajifunza maendeleo binafsi, utapata makala mbalimbali zinazohusu biashara, elimu, hamasa na maisha kwa ujumla. Karibu sana katika blogu hii.

0 comments: