Saturday 28 April 2018

"Mwombe Mungu huku ukiwa umeweka nguvu zako pia." Ni msemo wa Wahaya wa Tanzania.

Unaweza Kuwa unajiuliza  huyu aliyeandika makala hii Leo anamaanisha nini au Ni kweli unaweza kumsaidia Mungu?.
Ndiyo unaweza kumsaidia Mungu tena kwa asilimia mia moja.

 
 (KUPATA KITABU PICHANI WASILIANA NAMI KWA NAMBA:0764145476)

Wakati unaumbwa uliumbwa kutimiza kusudi fulani ndiyo maana mwalimu Adabert Chenche ana msemo ninaoupenda sana usemao, "Maisha huanza pale unapojua kusudi lako." Ni kweli huo ndio muda muafaka wa maisha kuanza na kama haujatambua kusudi lako ni sawa na kujiita mwogeleaji gwiji wakati unaogelea kwenye kidimbwi kidogo.

Kuna watu wengi wanamwomba Mungu awasaidie kutimiza malengo na ndoto zao lakini hakuna lolote la zaidi wanalolifanya zaidi ya kuomba.

Ndiyo maana nikaja na makala hii inayoenda kwa kichwa cha "MSAIDIE MUNGU."
Maana yangu nataka kukwambia kwamba hata kama unaomba namna gani, Mungu hatokusaidia kama hufanyi lolote kujisaidia. "Mungu hachezi mchezo wa kubahatisha," aliwahi kusema mwanafizikia Albert Einstein. Kumbe kumsaidia Mungu maana yangu ni kwamba ukitaka kufanikisha jambo lolote kwa kumuomba Mungu hakikisha na wewe unaweka juhudi fulani ndiyo maana nakwambia "MSAIDIE MUNGU, huku ukiwa umeweka nguvu zako pia." Wengine wenye hekima na maarifa wakaenda mbali na kusema, "Mungu huwasaidia wale wanaojisaidia."

Kumbe ukiwa unamuomba Mungu akusaidie  biashara ikue kwa kupata wateja wengi na wa uhakikia, hakikisha MUNGU akukute ukiwa unatoa huduma nzuri kwa wateja, unafungua biashara yako mapema, kutaja machache. Ukimwomba Mungu akusaidie upandishwe cheo kazini kwako, hakikisha kwanza unafanya kazi kwa juhudi, mtizamo wako ni chanya, unawasiliana vizuri na watu, upo tayari kujitoa kufanya kazi fulani hata kama haulipwi, waheshimu watu, wahi kazini kila siku na hauna sababu zisizo na mbele wala nyuma za kutofika kazini mara kwa mara. Kama ni mwanafunzi muombe Mungu akusaidie ufaulu lakini kumbuka kuweka bidii katika kusoma, hakikisha na wewe unamsaidia Mungu. Tunakosea sana pale tunapokazana kuomba lakini hakuna hatua yoyote tunayoichukua.

Ukitaka Mungu akuzidishie katika kipawa na kipaji ulichonacho, toka nje acha kujifungia ndani na kipaji chako, Mungu atakukuta ukiwa umeanza kuonyesha kipaji chako.
Ukitaka kutimiza malengo na ndoto zako, Muombe Mungu lakini kumbuka kumsaidia Mungu pia. Muda mwingine tunaweza kusema mbona fulani hasali kama Mimi lakini mambo yake yako sawa, huyo anakuzidi kitu kimoja anachukua hatua. Anamsaidia Mungu.

Hata kwenye Biblia Yesu alikuwa anawasaidia wale wenye imani ndiyo maana wengine walikuwa wanajitahidi hata kugusa vazi lake ili wapone. Wengine walidiriki kupita juu ya paa ili washuke katikati alipokuwa Yesu. Watu wa namna hii Yesu aliwaambia, "Imani yako imekuponya." Zakayo alikuwa mfupi lakini ufupi wake haukuwa kikwazo akaamua kupanda mti, ndiyo ilikuwa fursa ya yeye kuonekana.

Msaidie Mungu, akusaidie.

"Mafanikio yako mikononi mwako."

Ndimi:
Edius Katamugora
0758594893
ekatamugora@gmail.com

Mafanikio ni kitu cha kushirikishana. Usisahau kuwashirikisha ndugu na rafiki zako.

Hii ni blogu rasmi ya Edius Katamugora, hapa utajifunza maendeleo binafsi, utapata makala mbalimbali zinazohusu biashara, elimu, hamasa na maisha kwa ujumla. Karibu sana katika blogu hii.

0 comments: