Tuesday 17 April 2018

UKIJIFICHA NA FURSA ZINAJIFICHA

                                  


Kuna watu wanajua mambo mengi lakini hawataki kutoka nje na kuonesha yale waliyojaaliwa. Kuna watu wana ujuzi mkubwa lakini hawataki kuonesha ujuzi wao. Kuna watu wanamawazo mazuri ya biashara lakini hawataki kuanza kuyafanyia kazi.

Kila unayemwona kafanikiwa ni kwamba aliona fursa mahali Fulani akaanza kuifanyia kazi na ikampa matokeo makubwa. Unaweza ukawa na kipaji Zaidi ya watu wengi lakini wale wanaojitoa na kuonesha kipaji chao ndio dunia inawapokea na kuwaona kuwa ni bora. Ukijificha na fursa zinajificha pia. Ukijificha na fursa zinakukimbia. Katika kitabu chake cha Think And Grow Rich mwandishi Napoleon Hill anaamzungumzia mtu aliyeitwa Edwin Barnes huyu alikuwa na wazo na ndoto ya kufanya biashara pamoja na baba wa umeme duniani ambaye ni mgunduzi wa Balbu ya umeme, Thomas Edson. Bwana Barnes alimwendea Thomas Edson na kumweleza kuwa yeye anaweza kumsaidia kufanya mauzo makubwa ya bidhaa alizokuwa akizingua. Mungu si Athumani, Bwana Edwin alikubaliwa kuanza kufanya kazi na Thomas kama mtu aliyehusika na mauzo. Ukijificha  na fursa zinajificha.

Bishop T.D. Jakes alikuwa muhubiri katika kijiji kinachoitwa West Virginia huko Marekani. Siku moja binti mmoja alimsikia Bishop T. D. Jakes akihubiri. Binti huyu aliona kitu ambacho T.D. Jakes anaweza kuieleza dunia. Hivyo aliamua kwenda kwa mchungaji wake kumwomba amruhusu T.D.Jakes ahubiri pale kanisani kwao. Mchungaji alimwambia binti yule, “Unauhakika na mtu huyu au ni kama wengine ambao hujidai wanalijua neno la Mungu?.” Binti yule alijibu, “Ndiyo nina uhakika na mtu huyo.” Kisha mchungaji akamwambia, “kwakuwa nakuamini wewe nitampa nafasi.” Baada ya kupata nafasi ya kuhubiri, siku ya kwanza akiwa anahubiri Paul Crouch mmoja kati ya waanzilishi wa TBN (Trinity Broadcasting Network) alimsikia na alipendezwa na mahubiri yake, kisha akasema, itanipasa kumweka mtu huyu katika vipindi vya televisheni yangu. Kilichofuata ni historia. Fursa, haziji zikiwa na muhuri wa thamani yake, aliwahi kusema mtu mmoja na mlango wa fursa hauna  alama ya “SUKUMA” au “VUTA”. Kila fursa inapojitokeza mbele yake anza kuifanyia kazi huwezi jua kesho na kesho kutwa itakupeleka wapi.

Kitabu ulichonacho kiandike.
Nyimbo ulizonazo ziimbe.
Makala ulizonazo ziandike.
Ushauri ulionao utoe.
Mashairi uliyonayo yaandike.
Biashara uliyonayo ianzishe.
Kipaji ulichonacho, kitumie.
Ujuzi ulionao utumie.

Hakikisha unatumia fursa zinazokuja mbele yako kwa uweledi  wa hali ya juu.
Ilimlazimu Thomas Edson aanze kufunga umeme bure katika maofisi kabla ya mtu yeyote hajatamani hata kutizama kile alichokifanya.

Huko London nchini Uingereza, Gordon Ramsey alikuwa na wazo la biashara ambalo lilikuwa ni kuwafundisha wafungwa jinsi ya kutengeneza keki, ambazo ziliuzwa nje ya gereza kwa wananchi. Hii iliwasaidia wafungwa kupata fedha za kujikimu na pia kupata ujuzi ambao ungewasaidia kupata na kufanya kazi baada ya muda wao wa kifungo kuisha. Wewe pia unaweza kuwa Gordon Ramsey kwa kuifanya dunia iwe mahali pa furaha baada ya kuchukua fursa unayoificha. Jitoe sasa na onesha fursa uliyoibeba mkononi maana ukijificha na fursa zinajificha.

"Mafanikio yako mikononi mwako."

Ndimi:
EDIUS KATAMUGORA
0758594893
ekatamugora@gmail.com 

Hii ni blogu rasmi ya Edius Katamugora, hapa utajifunza maendeleo binafsi, utapata makala mbalimbali zinazohusu biashara, elimu, hamasa na maisha kwa ujumla. Karibu sana katika blogu hii.

0 comments: