Sunday 20 May 2018

Mambo madogo tunayoyafanya kila siku ndiyo yanatupeleka kufanya mambo makubwa. Mwandishi huanza kwa kuandika kurasa moja na hatimaye hukamilisha kitabu kizima. Mtoto akizaliwa aanzi na kukimbia, lazima, atambae, aanze kujaribu kutembea na kuanguka baadae atembee kisha ataweza kukimbia.

 (Picha hapo juu inaonesha gereji ambapo kampuni ya Apple ilianzishwa.)

Hatua ndogo ndogo tunazochukua kila siku ndizo zinatufikisha mbali.
Wachina wana msemo usemao, "Safari ya maili elfu moja huanza na hatua moja." Huwezi kufika mbali kama hutaki kuchukua hatua ya kwanza.

Anzia hapo hapo ulipo na kidogo ulichonacho, utafikia pakubwa unapopataka.

Usitake kila kitu kikamilike ndipo uanze kufanya, utasubiri nenda rudi.

Nikukumbushe tu, wakati Henry Ford anatengeneza gari lake la kwanza, gari hilo lilikuwa haliwezi kurudi nyuma (Kupiga reverse)  lakini hilo kwake halikuwa kikwazo.

Jeff Bezos mwanzilishi na mmiliki wa kampuni ya Amazon alianzisha Amazon katika chumba kidogo, chumba kimoja akiwa na kompyuta moja. Leo hii Amazon ni kampuni ya kimataifa iliyoanza kwa kuuza vitabu tu mtandaoni lakini Leo hii inauza karibia kila kitu. Leo hii Amazon imemfanya Jeff Bezos kuwa tajiri namba mbili duniani na wakati mwingine ameweza kumpiku Bill Gates na kuwa tajiri namba moja.

Kampuni ya Apple ilianzishwa na Steve Jobs pamoja na Steve Wozniak katika gereji iliyokuwa nyumbani kwa kina Job mwaka 1976 huko Cupertina, Calfornia nchini Marekani lakini Leo hii ni kampuni kubwa duniani inayotengeneza bidhaa aina ya Apple. Steve Jobs anasema, "Watu wenye nia, wanaweza kuibadili dunia."

Anza na kidogo ulichonacho. Anzia hapo hapo ulipo. Hajalishi upo katika mazingira gani haijalishi upo wapi. Inawezekana upo katika mazingira magumu lakini kumbuka, bahari shwari haitoi wanamaji hodari. Wewe anza tu. Watu waliokubali kuanzia chini wamefika mbali Leo. Kwanini na wewe usianzie hapo ulipo na hatimaye ufike mbali. Kubali kupiga hatua ya kwanza. 

"Tena ujapokuwa huo mwanzo wako ulikua ni mdogo lakini mwisho wako utaongezeka sana." (Ayubu 8:7)

Mafanikio yako mikononi mwako.
#KijanaWaMaarifa
© Edius Katamugora
0758594893
ekatamugora@gmail.com

Facebook: Edius Katamugora
Instagram: ediuskatamugora

Hii ni blogu rasmi ya Edius Katamugora, hapa utajifunza maendeleo binafsi, utapata makala mbalimbali zinazohusu biashara, elimu, hamasa na maisha kwa ujumla. Karibu sana katika blogu hii.

0 comments: