Tuesday, 15 May 2018

TAFAKARI KUHUSU SIKU YA FAMILIA DUNIANI

Habari mpendwa msomaji wa makala makini za Bideism Blog. Ni matumaini yangu u mzima wa afya na unaendelea vizuri. Itumie vyema siku yako ya Leo hakikisha haiendi wala kupotea hivi hivi. Siku moja inaweza kukufanya ukue. "One day can make you grow."



Karibu sana kupata  chakula cha akili nilichokuandalia siku ya Leo. Leo hii dunia nzima inasherehekea siku ya Familia duniani. Tarehe 15 mwezi wa tano kila mwaka. Hivyo nimeona tufanye tafakari fupi kuhusu familia zetu katika siku hii nzuri sana ya Leo inayohusu familia.

  ∆ Tafakari Kuhusu Siku Ya Familia Duniani:

1. Usitamani kuzaliwa katika familia isiyo yako. Hauwezi kuchagua wazazi. Pambana ili siku moja watu wengine watamani kuzaliwa katika familia yako. Inawezekana.

 Ukiona kuna familia ziko mahali pazuri jua kwamba kuna watu walipambana kuzifikisha hapo zilipo. Jua kwamba kuna watu walienyeka na kuteseka kuzifikisha hapo zilipo.

    Nguvu uliyonayo ukiamua kuitoa, unaweza kubadili  historia ya familia yako, unaweza hata kubadili historia ya nchi yako. Nakubaliana na Bill Gates, tajiri namba moja duniani aliyewahi kusema, "Kuzaliwa maskini sio kosa lako, kosa lako ni kufa maskini."

2. Chukua muda na iombee familia yako izidi kukua na kustawi katika upendo, mshikamano, furaha, maarifa na amani.

3. Familia sio tu wale uliozaliwa nao. Familia unaweza kuwa marafiki zako wa karibu (Your Confidants), watu unaofanya nao kazi na kushirikiana katika mambo mbalimbali (Your Partners).

4. Chukua notibuku yako yako na andika vitu kumi ambavyo unataka kuviona katika familia yako. (Kalamu na karatasi vina nguvu kubwa katika kuweka malengo). Andika chochote ambacho siku moja unatamani kukiona katika familia yenu. Napoleon Hill aliwahi kusema, "Chochote akili inachokiwazia na kukiamini, inaweza kukileta katika uhalisia." "Whatever the mind can conceive and believe, the mind can achieve."

5. Mtoto mwenye heshima na hekima ni lulu na ni dhahabu tena ni kama kito chochote chenye thamani katika familia yake. "Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, maana hii ndiyo haki, Waheshimu baba yako na mama yako, amri hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi: Upate heri, ukae siku nyingi katika dunia." (Waefeso 6:1-3)
"Mwana mwenye hekima humfurahisha babaye, bali mpumbavu, humdharau mamaye" (Mithali 15:20)

6. Ukiwa baba wa familia, walee watoto wako katika adabu na usiwe chanzo cha kuwaharibu. Usizifishe ndoto za watoto wako lakini pia kumbuka kumpenda mke wako. "Nanyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, bali waleeni katika adabu na maonyo ya Bwana." (Waefeso 6:3)
"Enyi wanaume wapendeni wake zenu." (Waefeso 5:25a)

7. Mwanamke mwenye hekima na heshima ataijenga nyumba yake mwenyewe bali asiye na hekima na heshima ataibomoa familia yake. "Enyi wake, watiini waume zenu." (Waefeso 5:22) "Kila mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake, bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe." (Mithali 14:1)

"Mafanikio yako mikononi mwako."

Ndimi:
Edius Katamugora
Mwandishi na Mhamasishaji
0758594893
Email: ekatamugora@gmail.com
Facebook: Edius Katamugora
Instagram: ediuskatamugora

Mafanikio ni kitu cha kushirikishana. Usisite kuwashirikisha marafiki zao tafakari hii muhimu kuhusu familia zao.

Unaweza kupata App ya Blog yetu ili upate makala za blog hii punde tu zinapokuwa hewani. Shuka chini kabisa mwa ukurasa huu. Bofya sehemu iliyoandikwa Download Our App For Free utatupata moja kwa moja.

Hii ni blogu rasmi ya Edius Katamugora, hapa utajifunza maendeleo binafsi, utapata makala mbalimbali zinazohusu biashara, elimu, hamasa na maisha kwa ujumla. Karibu sana katika blogu hii.

0 comments: