Friday, 4 May 2018

MAMBO YA KUFANYA SERIKALI INAPOSEMA HAKUNA AJIRA

                                 

Limekuwa jambo la kawaida kila kukicha ukiamka na kusikia waliosoma kozi fulani ajira zimekwisha. Hatuajiri tena.
Leo utasikia walimu, kesho Wahandisi na kuendelea. Nyakati kama hizi hazina mwisho huu ni mwanzo tu.

Kadri siku zinavyozidi kwenda ufinyu wa ajira unaongezeka. Maendeleo ya Teknolojia pia yanaanza kuwasukuma watu na kuwatoa makazini. Huko Hong Kong nchini China limetengenezwa roboti linaloitwa Sophia. Hili linaweza kufanya kazi zote za uhasibu, kufanya Debate(Mdahalo) na kadhalika. Roboti hilo limepewa uraia wa Saudi Arabia toka Julai 2017. Yanakuja mengi ya namna hii. Inahitaji kujiandaa kukabiliana na hali hii kama Abraham Lincoln alivyowahi kusema "Kama ningepewa masaa matano kukata mti, ningetumia masaa matatu kunoa shoka."

Kama wewe ni mwanafunzi wa chuo au mhitimu inakupasa ushtuke na uangalie tunakoelekea ni wapi. Inakupasa uangalie tunaelekea mahali gani. Unahitaji kuwa mtu anayeweza kuinunua kesho yako. Hapa namaanisha unahitaji kuwa mtu wa kuitazama kesho yako itakuwa ya namna gani. Huku ukitumia vyema wakati huu ulionao.

Imekuwa kasumba kwamba elimu ya watu wengi imejishikiza kwenye vyeti mtu anavyopewa pale anapohitimu.
Wahitimu wengi wa vyuo wanategemea sana vyeti vyao kuliko kawaida. Bila vyeti kuna watu kwao maisha hayana maana. Hapana, haipashwi kuwa hivyo, vyeti vinathibitisha kwamba umesoma lakini usichukue vigezo kwamba bila vyeti hauishi. Kama unaishi kwa mtazamo huo unahitaji kubadilika.
     
     Watu wanaofanya makubwa katika dunia ya Leo hawaulizwi vyeti vyao bali wanaulizwa ujuzi wao na mambo wanayoyafanya. Ukitaka kuthibitisha jambo hilo nenda benki kuomba mkopo, hautaulizwa cheti chako cha darasani bali utaulizwa unamiliki mali kiasi gani. Hali hii itaendelea kuwa hivi siku hadi siku.

Mambo Ya Kufanya Serikali Inaposema Hamna Ajira:
 
1. Tafuta Maarifa
Tumia nguvu zako nyingi, muda wako na hata pesa kutafuta maarifa. Soma vitabu, blogu na hata magazeti yenye maarifa (Sio ya udaku). Soma vitu vingine ambavyo watu wengine hawavisomi. Jana wakati naongea na rafiki yangu Raymond Mgeni nilimuulizia kitabu kinachoitwa The School Of Money kilichoandikwa na Olumide. Alinambia kwamba alikinunua shilingi 120,000/= Unaweza kuona kwa kiasi gani ameweka nguvu katika kutafuta maarifa.
 
      Ukiwa na maarifa watu watakutafuta tu. Hauhitaji kujitangaza. Hebu nikwambie ukweli ambao ulikuwa haujui au haujawahi kuufatilia: ukiona unakosa vitu Fulani jua kwamba kuna maarifa ambayo hauna na wengine wamekutangulia kuyafahamu. Unapoumwa tumbo unaenda kwa daktari sababu haujui sababu ya tumbo kuumwa. Kama ungelijua usingelikwenda hospitali.

Kuwa na maarifa na taarifa sahihi ni jambo la muhimu sana katika karne hii ya ishirini na moja. Dalali wa nyumba anajua   ni wapi nyumba za kupanga zilipo(anakuzidi taarifa) ili lazima umlipe kiasi fulani cha pesa akupe taarifa.

Ukiwa na maarifa hakuna mtu atakaye kutetemesha utatembea kifua mbele na utajiamini katika kufanya mambo yako na hauwezi kuwa kama watu wengine utakuwa mtu wa tofauti. Wekeza katika kutafuta maarifa. Kitu kikubwa na kizuri ni kwamba hakuna anayeweza kukupora kile ulichojifunza. Wanaweza kuchukua nyumba yako, wanaweza kuchukua biashara yako, wanaweza kuchukua hisa zako, wanaweza kuchukua pesa zako, lakini utavipata tena kwasababu hawawezi kuchua MAARIFA yako.

Mteja sikuzote hapangi bei ya bidhaa. Bali bei anapanga mwenye bidhaa.
Wewe pia unaweza kupanga watu wakulipe kiasi gani na watakulipa tu kiasi unachohitaji ili mradi umebeba kitu wanachohitaji.

    Je umebeba maarifa gani ambayo unaweza kuwafanya watu walipe bei unayotaka wewe?

Kama unataka kuwa mtaalamu au gwiji katika sehemu fulani. Watafute watu ambao tayari wamekwisha kuwa wataalamu au magwiji katika sehemu hiyo. Wasome walianzaje, waliwezaje na wamepitia changamoto zipi. Utajifunza mengi.
 
   Hakuna kuhitimu kwa mtu anayejifunza.  Hakuna mahafali kwa mtu anayejifunza. Unaweza kuhitimu chuo lakini hauwezi kuhitimu kujifunza. Nakubaliana na mtu mmoja aliyewahi kusema, "Ukiacha kujifunza unaanza kufa."

2. Jifunze Ujasiriamali
Hakuna aliyezaliwa akiwa mjasiriamali. Kila mtu anayemwona ni mjasiriamali alikuwa na muda na kujitoa na kujifunza ni kwa jinsi gani anaweza kuwa mjasiriamali. Huwa nawaambia watu, usiwacheke hawa wanafunzi wanaouza sambusa, visheti, karanga, nguo na viatu na vipodozi kwasababu kesho na kesho kutwa watakuja kuwa wajasiriamali wakubwa.

Huwa nashangaa pia zinapoitishwa semina zinazohusu biashara na ujasiriamali vyuoni wanafunzi wanaofika ni wachache. Nenda sasa katangaze bashi na sherehe, ukumbi utafurika tena hapo wanalipa kingilio. Kama wewe unaweka vipaumbele katika kufanya bashi nasherehe na mambo ya semina unaona kama yanakupotezea muda. Jiandae kulia mbeleni. Ipo siku utawalipia simu wale jamaa uliosoma nao wakufundishe ujasiriamali na wao watakwambia uwalipe pesa kwa maana utakula muda wao sababu wana mambo mengi ya kufanya. Nasema ukweli maana wanasema, "Ukweli utawaweka huru."

3. Tumia vizuri intaneti na mitandao ya kijamii
Unaweza kujifunza chochote unachotaka kupitia intaneti na mitandao ya kijamii. Lakini ukweli ni kwamba ni maarifa machache utayapata katika mitandao ya kijamii. Twitter, WhatsApp, Instagram na Facebook haviwezi vikakupa ujuzi na maarifa muhimu unayoyataka. Jifunze kuwa na kiasi katika kutumia mitandao ya kijamii, itakusaidia Sana.

4. Tafuta kitu kimoja na hakikisha wewe ni bora.
Ukiona kuna sehemu unaweza kufanya kwa ubora zaidi. Aisee, tumia nguvu zako zote, jifunze kadri uwezavyo hakikisha wewe ni bora katika sehemu hiyo. Ifikie hatua kwamba wakihitaji mtu katika sekta hiyo wewe uwe wa kwanza kutajwa hapo utakuwa umejiweka katika hatua nzuri.

  Kujibrand sio kitu kidogo au rahisi, kunahitaji uvumilivu na kujitoa ndiyo maana wanaweza kufanya wachache. Kama kingekuwa kitu rahisi kila mtu angeweza. Wewe pia unaweza kama ukiamua.

Tangazo: Mengi utayapata katika kitabu kinachoitwa Jinsi Ya Kuwa Mtaalamu Ukiwa Bado Unasoma unaweza kuweka oda yako mapema ili kikitoka uwe nacho. Wasiliana nami kupitia: 0764146476/0758594893

Mafanikio yako mikononi mwako.
Ndimi:
Edius Katamugora
Mwandishi na Mhamasishaji
0758594893
ekatamugora@gmail.com

Usisahau kupakua App yetu kupitia Play Store bure kwa kubofya sehemu iliyoandikwa DOWNLOAD OUR APP FOR FREE mwisho kabisa wa ukurasa huu.

Mafanikio ni kitu cha kushirikishana, washirikishe na wengine.

Hii ni blogu rasmi ya Edius Katamugora, hapa utajifunza maendeleo binafsi, utapata makala mbalimbali zinazohusu biashara, elimu, hamasa na maisha kwa ujumla. Karibu sana katika blogu hii.

0 comments: