Sunday, 22 July 2018

UCHAMBUZI WA KITABU CHA BUY THE FUTURE (UNUNUE WAKATI UJAO)



Mwandishi: Dr. Mensa Otabil

Dr Mensa Otabil ni mchungaji maarufu nchini Ghana, ni mjasiriamali na mhamasishaji pia. Mafunzo yake kupitia video kama vile YOUTUBE yamewajenga watu wengi. Dr Otabil pia ni mwanzilishi wa Chuo Kikuu kinachoitwa CENTRAL UNIVERSITY COLLEGE kilichopo nchini Ghana. Amekuwa akihubiri kwa muda mrefu. Lengo lake ni kuona watu wanachojifunza katika biblia wanakiweka katika matendo na si maneno tu. Afrika ina dini nyingi lakini maendeleo ni kidogo. Kwanini? Kwasababu watu wengi tunafundishwa Biblia kwa kutojua yale tunayofundishwa hatuweki katika matendo na maisha yetu ya kila siku. Hapo ndipo Dkt. Otabil anatuandikia kitabu hiki kizuri kinachoitwa BUY THE FUTURE.


UCHAMBUZI: Ukurasa 1-16
Inakuwaje watu wanazaliwa sehemu moja, wanasoma shule moja, muda mwingine wanakaa dawati moja, wanafanya mazoezi yaleyale lakini mwisho wa siku baada ya miaka kadhaa unaweza kukuta mmoja kafanikiwa zaidi ya mwingine.

Kuna watu ulisoma wote darasa moja au kidato kimoja au hata chuo kimoja lakini leo hii umewazidi kimafanikio au wamekuzidi.
Yanatokeaje haya yote?

Mwandishi wa kitabu hiki anatueleza kisa cha mapacha wawili waliozaliwa tumbo moja lakini wakaishia kuwa na maisha ya tofauti. Mmoja anafanikiwa na kuwa mtu wa mataifa na mwingine mtu wa kawaida. Mapacha Hao ni Yakobo na Essau wana wa Isaka na Rebeka.

Essau alimuuzia Yakobo haki yake ya kuwa mzaliwa wa kwanza kwa supu ya nyama na mkate na mambo yote yaligeukia hapo kwenye maisha yake. Yakobo alibarikiwa na baba yake kuwa mkuu wa mataifa, na Essau alibaki kuwa mtu wa kawaida.

Watu waishia kuwa na maisha ya tofauti kutokana na sababu kuu mbili:
1. Tabia wanazozikuta katika mazingira waliyokulia
2. Namna wanavyoitikia kwa tabia hizo.

Watu wengi wanaishi kutokana na tabia walizofundishwa na wazazi wao au hata jamii inayowazunguka.

Sasa namna tunavyoitikia kutokana na tabia za mazingira ndipo tofauti hujitokeza. Mwingine akizaliwa katika familia maskini anaona bado anahitaji kupambana ili aitoe familia yake katika lindi la umaskini, mwingine anaona umaskini ni haki yake, kama alizaliwa maskini basi atabaki kuwa maskini hadi kufa.

Kitu kingine kinachosababisha tunakuwa na maisha ya tofauti ni chaguzi tunazozifanya. Essau aliuza haki yake ya mzaliwa wa kwanza kisa chakula hakujua kama kuzaliwa mtu wa kwanza ni kitu cha muhimu zaidi ya chakula. Je chaguzi unazozifanya ni sahihi?

Mwisho kabisa kitu kinachosababisha watu wanakuwa na maisha tofauti ni VIPAUMBELE.

Wakati kuna mtu anasaka elfu 30 ili aende pale House of Wisdom anunue kitabu cha Dr. Mengi, I CAN, I MUST, I WILL, mwingine anatafuta elfu 30 ananunue jezi mpya ya Critiano Ronaldo ya Juventus.

Wakati mwingine ananunua gazeti ili atizame kurasa za uchumi kuangalia kuhusu soko la hisa la Dar Es salaam, mwingine ananunua gazeti ili ajue kama yule mbwa aliyepotea amepatikana au la. Tofauti inaanzia hapo.

Unakuta mtu anakumbuka gori lililofungwa kwenye kombe la dunia la mwaka 2006 lakini hakumbuki hata mambo yake ya kifedha yanaendaje. Hajui anamiliki akiba kiasi gani.

Ukitaka kuwa tofauti na wengine, hakikisha vipaumbele vyako vinaangalia wakati ujao. Usitafute furaha ya muda mfupi, tafuta furaha ya muda mrefu.

Itaendelea....

#KijanaWaMaarifa
Edius Katamugora
0764145476/ 0758594893
ekatamugora@gmail.com
www. bideism.blogspot.com

Hii ni blogu rasmi ya Edius Katamugora, hapa utajifunza maendeleo binafsi, utapata makala mbalimbali zinazohusu biashara, elimu, hamasa na maisha kwa ujumla. Karibu sana katika blogu hii.

0 comments: