Hakuna wakati mzuri ambao unaweza
kujifunza mambo mengi kama wakati wa mazoezi ya vitendo. Bahati mbaya wanafunzi
wengi hawajui thamani ya muda huu. Wengi huona kama wanapoteza muda na hufanya
mambo ili mradi tu siku ziende amalize muda wake wa mazoezi kwa vitendo. Faida
kubwa ya muda wa mazoezi ya vitendo ni kwamba muda huo huwa unajifunza mambo
ambayo utakuwa ukiyafanyia kazi ukiwa kazini. Mambo mengi unayojifunza darasani
hautayatumia ukiwa kazini kikubwa utakachotumia ni kile unachojifunza katika
mazoezi ya vitendo.
Mambo unayotakiwa kuyafanya muda wa
mazoezi ya vitendo:
·
- Wahi mapema katika eneo lako la kazi.
Tabia ya kuwahi kazini hautaijenga
pale utakapo kuwa umeanza kazi bali unaijenga kabla ya kuanza kazi. Jitahidi
kuamka mapema na kuwahi kila siku katika eneo lako unakofanyia mazoezi ya
vitendo.
- · Waheshimu Watu wote.
Heshima haiuzwi dukani. Jitahidi kuwa
na heshima katika eneo unalofanyia kazi, wasalimu watu wote bila kubagua
vitengo vyao vya kazi. Siku moja wakati niko katika mazoezi ya vitendo dada
mmoja aliniita na kuniambia maneno haya, “Wewe dogo mimi nakukubali sana.”
Nikamuuliza kwanini? Akasema, “Nitafute baadae nitakwambia kwanini maana sasa
hivi nina kazi nafanya.” Muda wa mapumziko nilimtafuta na kumuuliza kwanini
alisema vile muda ule. Akaniambia, “Yaani wewe una heshima sana, wenzako huwa
hata hawatusalimii na sijui kwa sababu sisi ni vibarua. Inaonekana kwenu
ulifunzwa adabu vyema na mama yako.” Maneno yale yaliniingia kichwani na toka
siku hiyo kila mtu ambaye huwa nikipishana naye nikiwa katika mazoezi ya
vitendo huwa siachi kumpa salamu. Napenda kuwa mtu wa watu. Kumbuka watu
wanajali endapo wakijua na wewe unawajali. Kanuni ipo hivyo.
- · Jifunze kutoka kwa mtu yeyote mwenye ujuzi
Kama ukiona mtu ana kitu fulani
anakijua aisee chukua muda wako na jifunze kutoka kwake, haijalishi unamzidi
umri au elimu wewe muombe akufundishe. Binafsi nimejifunza mambo mengi kutoka
kwa mafundi wa ujenzi wakati wa mafunzo ya vitendo zaidi ya ninanvyo jifunza
kwa injinia anayenisimamia. Jifunze kutoka kwa mtu yeyote utapata kujifunza
mambo mengi. Niliwahi kukutana na kijana anayeitwa Shabani ambaye elimu yake
ilikuwa ya kidato cha nne lakini alikuwa akifanya kazi katika maabara ya udongo
inayohusiana na vipomo vya barabara, kijana yule alikuwa akijua mambo mengi
yanayohusiana na barabara zaidi yangu mimi kwani nilikuwa ndo nimemaliza mwaka
wa kwanza chuo hivyo muda mwingi nilikuwa nikifanya kazi naye na nilijifunza mambo mengi kutoka
kwake.
- Jitoe na fanya kazi kwa bidii
Mahali unapofanyia mazoezi kwa vitendo
inaweza kuwa njia moja ya kukupa ajira endapo utakuwa mtu wa kujitoa na kufanya
kazi kwa bidii. Ukijituma na kujitoa kwa uwezo wako wa hali ya juu watu
unaofanya kazi nao watakupenda na muda wote watapenda kufanya kazi na wewe.
Hakuna anayependa mtu mvivu. Kujituma na kufanya kazi kwa bidii muda wa mazoezi
ya vitendo kunaweza kukufungulia fursa mpya ambazo hata hukuzitarajia. Kuna
watu wengi wameajiriwa katika kampuni na taasisi ambazo walifanyia mazoezi ya
vitendo. Sifa iliyowafanya wawe hapo ni kujituma, nidhamu na bidii
waliyoionesha huko nyuma. Hata kama una ndoto ya kujiajiri kujituma ni suala la
muhimu sana. Fanya kazi kana kwamba unaifanyia kampuni yako ili siku ujiajiri
mambo uwe umekwisha yazoea kwamba kazi huwa zinafanywaje.
- Epuka Utoro
Kama umepangiwa kwenda kufanya mazoezi
ya vitendo kila siku kwa wiki nane mfululizo epuka kuwa mtoro. Heshimu muda huo
kana kwamba ni kazi yako ambayo tayari umekwisha ajiriwa na unapewa mshahara.
Heshimu muda huo kana kwamba ni kampuni yako ambayo unaifanyia kazi na
unahitaji kuingiza kipato. Ukifanya kazi kwa mtazamo huo hautakuwa na akili za
kuwa mtoro. Utoro utakuchafua. Endapo utahisi kama hautaweza kufika katika eneo
lako siku hiyo kwa sababu zilizo nje ya uwezo wako kama msiba au ugonjwa ni
vyema ukatoa taarifa.
- Maliza kazi unazopewa mapema
Jitahidi kila unapopewa kazi uimalize
mapema hii itakuongezea sifa kwa watu unaowafanyia kazi na pia itakuongezea
uzalishaji. Jitahidi kuifanya kwa ubora pia usiwe mtu wa kukurupuka. Ukimaliza
kazi uliyopewa omba kazi nyingine.
- ·Ongeza muda wa ziada
Sio lazima kama umepangiwa na chuo
chako kufanya mazoezi kwa vitendo kwa wiki nane ufanye kwa wiki nane basi. Kama
una muda wa ziada unaweza kuongeza muda kama wiki moja au mbili. Hii inaitwa
kujitolea na nimeizungumzia mara nyingi huko nyuma. Kujitolea ni alama za ziada
unazojipatia na pia kunakuongezea sifa zaidi. Wanafunzi wengi wakikaguliwa huwa
wanaacha kwenda kwenye maeneo yao ya mazoezi ya vitendo na hufikiri labda
wanakikomoa chuo au msimamizi wao kumbe wanajikomoa wenyewe. Kama unautafuta
utaalamu ni bora ukaongeza muda wa ziada. Kama unakumbuka vizuri kanuni ya
masaa 10000, kuongeza muda ni chaguo bora sana kwako.
- · Usikate mawasiliano
Ukiwa katika eneo lako la mazoezi kwa
vitendo ni wazi kwamba utakuwa umejenga urafiki na kufahamiana na watu
mbalimbali. Ukimaliza muda wako endelee kuwasiliana na watu huo, urafiki wenu
usiishie hapo. Huu ndio muda wa kuanza kujuana na watu mbalimbali. Hawa
wanaweza kukufungulia milango ya fursa mpya.
"Mafanikio yako mikononi mwako."
Ndimi
Edius Katamugora
#KijanaWaMaarifa
0764145476
0758594893
ekatamugora@gmail.com
0 comments:
Post a Comment