Monday, 3 September 2018

IPO WAPI TALANTA YAKO?



IPO WAPI TALANTA YAKO?
________________________________________

Dr. Myles Munroe aliwahi kusema, "Sehemu tajiri kuliko zote duniani sio kule kwenye visima vya mafuta nchini Kuwait, Iraq au Saudi Arabia. Wala sio kwenye machimbo ya dhahabu na almasi yaliyoko nchini Afrika ya kusini. Ingawa inaweza kushangaza lakini sehemu tajiri kuliko zote hapa duniani ni umbali mchache toka nyumbani kwako. Sehemu hiyo ni makaburini. Huko zimezikwa ndoto ambazo hazijawahi kukamilishwa, nyimbo ambazo hazijawahi kuimbwa, vitabu ambavyo hazijawahi kuandikwa, michoro ambayo haijwahi kuchorwa, mawazo ambayo hayajawahi kushirikishwa, uvumbuzi ambao haujawahi kufanyika, maono ambayo hayajawahi kufikiwa na kusudi ambazo hazijawahi kutimizwa. Makaburi yamejaa utajiri uliozikwa. Ni shida iliyoje!"

Kufuatia maneno hayo yanayosikitisha Dr. Myles alitutaka sisi kutumia kwa ufasaha vipaji na talanta tulizojaliwa ili kuifanya dunia iwe mahali penye furaha.

Kuna watu wengi ambao wamejaliwa vipaji lakini wanavificha hawataki kuvitumia na kuvionesha. Mpendwa msomaji Mungu alikuumba ili ukitumie kipaji chako kwa manufaa yako na manufaa ya watu wanaokuzunguka.

Kwanini sasa umeficha kipaji chako? Kwanini umezika kipaji chako?

Hadithi ya Talanta:

( Matayo 25:14-30 )

Watumishi Watatu Walioachiwa Talanta

“Pia Ufalme wa mbinguni utafananishwa na mtu aliyekuwa anasafiri, akawaita watumishi wake na kuwakabidhi mali yake.

“Yule aliyepewa talanta tano alikwenda mara moja kuzifanyia biashara akapata talanta tano zaidi. Yule aliyepewa tal anta mbili akafanya hivyo hivyo, akapata mbili zaidi. Lakini yule mtumishi aliyepata talanta moja, alikwenda akachimba shimo akaifukia huko.

“Baada ya muda mrefu yule bwana wa hao watumishi alirudi akakagua hesabu za fedha zake alizowaachia. Yule mtumishi aliyepokea talanta tano akaja, akaleta talanta tano zaidi. Akasema, ‘Bwana ulinikabidhi talanta tano, hizi hapa, nimezalisha talanta tano zaidi.’ Bwana wake akamwambia, ‘Umefanya vizuri sana, mtumishi mwema na mwaminifu; umekuwa mwaminifu katika machache; nitakupa mamlaka juu ya vitu vingi zaidi. Njoo ufurahi pamoja na bwana wako.’

Yule mwenye talanta mbili naye akaja. Akasema, ‘Bwana, ulinikabidhi talanta mbili. Nami nimepata faida, hizi hapa talanta mbili zaidi.’ Bwana wake akajibu, ‘Umefanya vizuri sana, mtumishi mwema na mwaminifu; umekuwa mwaminifu katika machache, nami nitakupa mamlaka juu ya vitu vingi zaidi. Njoo ufurahi pamoja na bwana wako.’

Kisha yule mtumishi aliyepokea talanta moja akaja, akasema, ‘Bwana, nilijua kwamba wewe ni mtu mgumu, unavuna ambapo hukupanda na kukusanya ambapo hukutawanya mbegu. Kwa hiyo niliogopa, nikaenda nikaificha talanta yako ardhini. Hii hapa mali yako.’

Lakini Bwana wake akamjibu, ‘Wewe mtumishi mwovu na mvivu! Ulijua kwamba ninavuna nisipopanda na kukusanya nisipota wanya mbegu? Mbona basi hukuweka fedha zangu benki ili nita kaporudi nizichukue na faida yake? Mnyang’anyeni hiyo talanta mumpatie yule mwenye talanta kumi.’ Kwa maana kila mtu mwenye kitu ataongezewa, naye atakuwa navyo kwa wingi. Lakini kwa yule asiye na kitu, hata kidogo alicho nacho atanyang’anywa.

‘Mtupeni huyo mtumishi asiyefaa nje kwenye giza, huko kuta kuwa na kilio na kusaga meno.’ ”

Tujifunze nini kutokana na hadithi hii?

Kwanza kabisa tujifunze kuvitumia vipaji vyetu bila kuvificha na kuvizika tusifanane kama mtumishi aliyepewa talanta moja. Kuna mtu aliwahi kusema "Kila mtu amezawadiwa, lakini ni watu wachache hufungua maboksi ya zawadi zao." Usiruhusu kuwa mmoja wa watu wasiotumia vipaji vyao.

Jambo la pili la kujifunza hapa ni kwamba kipaji ni mtaji tosha. Ukiwa na kipaji wewe ni tajiri mkubwa sana lakini utajiri huo utaupata endapo utaamua kutumia kipaji chako.

Mwandishi maarufu Jim Rohn aliwahi kusema "Wewe ni maskini kwasababu watu hawajui lolote kuhusu wewe." Kama watu wakijua kipaji chako watakuwa tayari kukulipa na maisha yako yatakwenda vizuri. "Kipawa ni kama kito cha thamani machoni pake yeye aliyenacho; Kila kigeukapo hufanikiwa." (Mithali 17:8)

Tatu, jifunze kufanya mambo kwa ubora na kwenda hatua ya ziada. Swali na kujiuliza hapa kila siku ni nitafanyaje kitu hiki ninachokifanya zaidi ya jana? B.C. Forbes anasema, “Mtu ambaye hutoa huduma ya utimilifu kwa uwezo wa unyenyekevu atachaguliwa kwa majukumu ya juu, kama vile mtumishi wa kibiblia ambaye aliongeza paundi moja iliyotolewa na bwana wake alifanya kuwa kiongozi wa miji kumi.”

Maisha ni uaminifu:

Katika maana kubwa mbili za maisha ambazo ni; maisha ni mtihani lakini pia maisha ni uaminifu. Mungu amekuumba na kukupatia kipaji fulani akijua kwamba unaweza kukitumia vizuri zaidi ya mtu mwingine yeyote. Hivyo usipokitumia unavunja uaminifu huo. Amka sasa fufua kipaji chako. Huenda kikawa kipaji cha uandishi kama changu, kipaji cha ufundi, kipaji cha kuimba, kipaji cha ushonaji, kipaji cha uhamasishaji, kipaji cha kucheza michezo mbalimbali, kipaji cha kufundisha, kutaja machache.

Wataalamu wanasema kila mtu anapozaliwa anazaliwa na vipaji na uwezo kuanzia 500-700. Je kati ya hivyo 500-700 umekosa kimoja cha kuishirikisha jamii inayokuzunguka?

Kipaji ni nini?
Kiufupi kipaji ni kitu unachoweza kukifanya kwa urahisi bila kutumia nguvu nyingi. Kama ni kufundisha hautatumia nguvu nyingi, kucheza mpira, kushona, kuimba, kupamba, kutaja machache.

Utawezaje kutambua kipaji chako?

Hapa nitaomba uchukue kalamu na karatasi au notibuku kisha ujiulize maswali yafuatayo na uandike majibu yake.

Ni vitu gani unapendelea kuvifanya?

Mara nyingi vitu unavyopendelea kuvifanya huwa ni kipaji chako. Mimi napenda sana kuandika hivyo kuandika ni kipaji changu. " Waafrika wana methali isemayo, 'Mahali moyo wako ulipolalia ndipo miguu huamkia.' Ukitazama mambo yanayokuzunguka yanaonesha kile unachopendelea. Kwa mvuvi unasikia harufu ya samaki. Kwa mwandishi pamejaa magazeti. Kwa mwalimu amezungukwa na vitabu. Daktari amezungukwa na madawa na vitabu juu ya magonjwa mbalimbali." Anasema Dr. Fr. Faustin Kamugisha.
2.Ni mambo gani ulipendelea kufanya ukiwa mtoto?

Mara nyingi vipaji huanza kujionesha toka mtu akiwa mtoto mdogo. Waulize ndugu na hata wazazi, ulipokuwa mdogo ulipenda kufanya mambo gani. Au kama unayakumbuka yaandike pia.

3. Ni kitu gani unaweza kufanya bila kulipwa pesa?

4. Ni kitu gani unaweza kufanya vizuri zaidi ya mtu mwingine yeyote?
Kuna mambo ambayo ukifanya kila mtu anakusifu na wakati mwingine kukuona mtu wa ajabu. Andika ni mambo gani hayo. Au kama ni kazini, darasani au mahali popote usipokuwepo wewe hayaendi sawa.

5. Ni ujuzi gani ambao nimezaliwa nao?

6. Kama ningejulikana kwa kitu Fulani kikubwa. Je kingekuwa kitu gani?

Piga picha miaka 5 au kumi ijayo ukiingia katika mkusanyiko wa watu unataka wakutambue kama nani?

Hayo ni baadhi ya maswali ambayo yanaweza kukusaidia kutambua kipaji chako.

Anza Mara moja kutumia kipaji chako.
Kuna watu wengi ambao walikwisha tambua vipaji vyao lakini bado hawavitumii. Wataalamu wa mambo ya ubongo wanasema ili mtu awe mbobezi katika kipaji Fulani anahitaji masaa yasiyopungua elfu kumi.

Hivyo unahitaji muda mwingi wa kufanyia mazoezi kipaji chako. Tumia walau dakika 30-60 kama umebanwa ukiwa unafanya mazoezi.

Jikutanishe na watu waliofanikiwa katika kutumia kipaji chako na ujifunze kutoka kwao. Wahoji changamoto wanazokumbana nazo na wamefanyaje hadi kufikia hapo walipo. Itakusaidia sana na utajifunza mengi.

Soma vitabu na makala kila siku.
Kipaji kina mahusiano makubwa na ubongo. Ni kama misuli, Ili itanuke lazima ifanyishwe mazoezi mara kwa mara hivyo jitahidi kusoma vitabu na makala mbalimbali zinazohusiana na kipaji chako. Bila maarifa utakosa mengi.

Uzuri ni kwamba karibia kila kipaji Leo hii kuna mtu amekiandikia kitabu au makala inayoweza kukusaidia. Au unaweza kusoma historia za watu walikuwa na kipaji kama chako.

Wahenga walisema "Elimu ni bahari." Hivyo usichoke kujifunza. Kama utajifunza kila siku utakuwa mtu wa tofauti kubwa na watu lazima wakutafute wakulipe pesa.

Usikubali kuficha kipaji chako.
Kipaji chako ni mtaji.
Kipaji chako ndiyo mafanikio yako.
Kipaji chako ni fursa tosha ambayo inakupasa uichangamkie haraka iwezekanavyo.

"Kipawa ni kama kito cha thamani machoni pake yeye aliyenacho; kila kigeukapo hufanikiwi." (Mithali 17:8)

"Mafanikio yako mikononi mwako."

Ndimi:
Edius Katamugora
#KijanaWaMaarifa
Mwandishi na Mhamasishaji
0764145476
0758594893
ekatamugora@gmail.com

Hii ni blogu rasmi ya Edius Katamugora, hapa utajifunza maendeleo binafsi, utapata makala mbalimbali zinazohusu biashara, elimu, hamasa na maisha kwa ujumla. Karibu sana katika blogu hii.

0 comments: