Kuna methali moja inasema, “Tuliza moyo wako sehemu moja kama mbwa anayepikiwa paka.” Watu wengi wanapenda kutengeneza jina na pia wanapenda kutengeneza pesa.
Kama una nia ya kutengeneza mambo mawili kwa wakati mmoja nikushauri leo anza na kutengeneza jina. Ukitaka kutengeneza vyote kwa pamoja ni Dhahiri kuwa utashindwa mapema. Tuliza moyo wako sehemu moja kama mbwa nayepikiwa paka. Kila siku huwa napenda kusema watu wanapenda kufanya kazi na mtu wanayemfahamu, watu wanapenda kufanya biashara na mtu wanayemfahamu, watu wanapenda kushirikiana na watu wanaowafahamu.
Usipende kutengeneza pesa wakati bado haujajulikana. Hakikisha kwanza watu wanakufahamu, watu wakikufahamu pesa zitafuata. Toa kitu cha thamani na kilicho bora watu hawataacha kuja kwako. Penda unachokifanya maana kuna nyakati pesa itakosa na kitakachokusukuma kuendelea kufanya kitu unachokifanya ni mapenzi dhidi ya kazi yako. Nakubaliana na Samantha Wills, mwanamitindo wa Vidani na mjasiriamali aliyewahi kusema, “Kama unapenda unachokifanya na unakifanya vizuri, pesa itafuata.”
Anza kutoa thamani, thamani itakufanya ujulikane, watu unaowahudumia watapeleka sifa zako. Kama sifa zako ni nzuri watu wengine watapenda kushirikiana na wewe au kuja kutazama kile ukifanyacho. Nenda hatua ya ziada, toa zaidi ya kile watu wanachotegemea. kila siku jiulize nitawezaje kukipandisha hadhi kitu ninachokifanya? Swali hilo litakupa motisha zaidi ya kufanya kwa hatua ya ziada Zaidi ya ulivyofanya jana.
Tumia muda wako mwingi kujenga jina lako kwanza. Watu wakisikia Edius Katamugora ni nani, waweze kusema ni mtu wa namna gani, hata wengine wakaseme kwa wengine. Nilipoandika kitabu changu cha kwanza kinachoitwa Barabara Ya Mafanikio lengo langu kubwa lilikuwa watu wajue mimi ni mwandishi baada ya hapo ndipo niwashe moto kama wote. Sikupata faida kubwa katika mauzo lakini faida kubwa niliyoipata ni watu kuwaambia watu mimi ni nani na ninafanya nini. Nimekutana na watu wengi ambao husema, “Nimekuwa nikikuona mtandaoni hatimaye leo nimekutana na wewe ana kwa ana, unafanya kazi nzuri.” Watu kama hao huwa naona kama nadaiwa pakubwa sana kwani bado safari ni ndefu nahitaji kuwafikia watu wengi zaidi na zaidi.
"MAFANIKIO YAKO MIKONONI MWAKO."
Ndimi:
Edius Katamugora
#KijanaWaMaarifa
0764145476
0758594893 (WhatsApp)
ekatamugora@gmail.com
0 comments:
Post a Comment