Tuesday, 1 January 2019

2019: MANENO KIDOGO MATENDO KAMA YOTE






EDIUS KATAMUGORA
0764145476
ekatamugora@gmail.com

Siku, wiki, miezi, miaka inapita mbele yangu mimi, kwanini nisimshukuru Mungu kwa kunilinda vema. Asante Mungu kwa kutujalia kuuona mwaka mpya.
Ni majaliwa yake Mungu, kuuona mwaka. Wengi walitamani kuuona mwaka mpya wa 2019 lakini hawakubahatika kufika. Mimi ni nani Bwana nisikushukuru? Nasema asante kwa mara ya pili. Kushukuru ni kuomba tena.

Wakati tunauanza mwaka mpya nimeona ni vyema nikushirikishe kauli mbiu yangu nitakayoitumia mwaka huu wa 2019, binafsi naiita, Maneno kidogo, matendo kama yote. Miaka mingi huwa tunaweka mipango mingi lakini mipango hiyo huishia katika maneno na wala si vitendo. 2019 ni mwaka wa vitendo wala si maneno.

Unapouanza mwaka huu ningependa nikushirikishe baadhi ya mambo yatakayokusaidia ili mwaka huu uwe bora kwako.

Moja, katika kila jambo unalolifanya mshirikishe Mungu. Mtangulize Mungu mbele. “Anza siku yako na Mungu, maliza siku yako na Mungu,” alisema Rick Warren, mwandishi wa vitabu, naye Ben Carson anaongeza akisema, “Usiwe mkubwa zaidi ya Mungu.”

Mungu ndiye aliyekuumba na anajua alikuleta duniani uje kutimiza kusudi gani hivyo ukimtanguliza yeye mambo yako yatakuwa safi. Kuna vitu haviwezi kufanyika bila kusali.

Unapomtanguliza Mungu kwenye unachokifanya, yeye anakupa mwangaza ni wapi upite ili uifikie hatima yako.

Pili, acha kulalamika. Malalamishi hayajawahi kumtoa mtu mahali alipo na kumpeleka katika hatua nyingine. Imekuwa kawaida kila ukikutana na mtu anasema, “Vyuma vimekaza,” wakati huo huo kuna watu wanaishi maisha yao ya kawaida kila siku wanaendelea kufurahia maisha na kula kuku kwa mrija na hauwezi kuwasikia hata siku moja wakisema sijui vyuma vimekaza. Sikia rafiki yangu, vyuma haviwezi kuachia ukiendelea kubweteka na kulalamika.

Hakuna nchi iliyoendelea kwa kuwa na wananchi wanaolalamika. Wakati wengine wanalalamika wewe usiwe upande wao. Chezea hapo hapo wanapolalamikia hiyo inaweza kuwa fursa yako.

Tatu, ongeza chanzo cha kipato. Chanzo kimoja cha kipato ni utumwa. Hakuna aliyetajirika kwa kuwa na chanzo kimoja cha kipato. Kadri unavyokuwa na vyanzo vingi vya kukuingizia kipato ndivyo unavyokuwa na pesa nyingi mfukoni. Kama ni mfanyakazi umeajiriwa anzisha hata biashara ndogo ya pembeni inayoweza kukuingizia kipato,fanya miradi nje ya kazi yako.

Mto wenye vyanzo vingi vya maji ndio huwa na maji mengi. Hivyo hivyo mtu mwenye fedha nyingi huwa na vyanzo vingi vya fedha. Tafakari, chukua hatua.

Nne, wekeza kwenye maarifa. Jiulize ni vitabu vingapi umesoma mwaka uliopita?
Kuna watu toka wamemaliza shule hawajawahi kusoma kitabu chochote. Takwimu zinaonesha kwamba mtu wa kawaida husoma vitabu vinne kwa mwaka na milionea wa kawaida husoma vitabu ishirini na nne kwa mwaka. Usishangae kwanini milionea anaweza kutengeneza kipato mara sita zaidi ya mtu wa kawaida kwa mwaka.

Unapokuwa na maarifa ni rahisi kufanya kazi kwa ufanisi. Leo hii karne tuliyomo ni karne ya maarifa na taarifa. Ukiwa na maarifa na taarifa sahihi siku zote utakuwa kiongozi.

“Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa.” (Hosea 4:6) Maarifa yanapotumika kwa viwango vikubwa tunapata hekima. Hakuna maarifa, hakuna hekima. “Mwanangu, uchume maarifa tangu ujana hata kuwa mwenye mvi nawe utapata hekima.” (Yoshua Bin Sira 6:18)

Tano, weka malengo. Andika malengo yako. Unahitaji kuwa na malengo ya kifedha, kiroho, kiafya, kielimu, malengo katika kazi zako. Malengo yaendane na maono yako. Maono ni jinsi unavyojiona siku zijazo huku ukiishi leo. Wanasema kesho bora inategemeana na unavyoiandaa siku ya leo.

Wakati unapanga malengo ya mwaka huu kwanza kabisa angalia ni vitu gani ulipanga kuvifanya mwaka jana na havikukamilika. Vikamilishe kwanza, anza sasa kufanyia kazi malengo yako ya mwaka huu.

Uchunguzi unaonesha kwamba malengo mengi hufa wiki ya pili ya mwezi Februari. Watu wengi huanza Januari kwa mbwembwe lakini baadae wanaachana na malengo yao. Njia rahisi ya kuepukana na hili ni kuweka malengo madogo kila siku ya kukusaidia kufikia malengo yako.

Tumia dakika 15 kila siku kupanga ratiba yako ya siku nzima hii itakusaidia kuongeza uzalishaji kwa asilimia 20.

MANENO KIDOGO, MATENDO KAMA YOTE

EDIUS KATAMUGORA
#KijanaWaMaarifa
0764145476
ekatamugora@gmail.com

Hii ni blogu rasmi ya Edius Katamugora, hapa utajifunza maendeleo binafsi, utapata makala mbalimbali zinazohusu biashara, elimu, hamasa na maisha kwa ujumla. Karibu sana katika blogu hii.

0 comments: