Siku moja shetani alitangaza hadharani kufanya mnada ili auze zana zake.
Siku hiyo watu wengi walijotokeza kwenye huo mnada.
Katika zana alizokuwa akiuza kulikuwa na kifaa kizee sana kilichoandikwa, "Hakiuzwi."
Watu waliofika kwenye mnada ule wakamuuliza shetani, kwanini zana hiyo haiuzwi. Akajibu akisema, Naweza kuuza kifaa chochote lakini hiki siwezi kukiuza. Hiki ndicho kifaa ninachotumia sana. Kinaitwa Kukata tamaa na kwakutumia kifaa hiki naweza kuingia kwenye mioyo ya watu, bila hivyo siwezi.
Nikiweza kuweka kifaa hiki katika moyo wa mtu njia huwa imefunguliwa kwangu mimi kuweza kupanda chochote ninachokitaka.
Ukikata tamaa kwenye masomo yako na ukashindwa, utaanza kuwachukia wale wanaofaulu bila sababu.
Ukiwa mzazi na kumkatia tamaa mwanao alioshindwa kwenye mtihani wake wa darasa la kwanza, utaanza kumpa majina ya ajabu ajabu, utamwita mjinga, utamwambia hawezi kufika popote, yeye ni kilaza haujawahi kuzaa mtoto mjinga kama yeye. Maneno hayo hupandwa kichwani mwa mtoto, na yanaweza kufanya maisha yake yote. Haujasikia watu wakisema, maneno huumba!
Askari magereza mmoja aliwahi kuwauliza wafungwa swali ili: ni wazazi wangapi waliwahi kuwaambia mtaishia gerezani, asilimia 95 walinyoosha mkono. Yaani wazazi wao waliwatabiria maisha ya gereza wakiwa bado huru. Wazazi wao waliwakatia tamaa mapema.
Ukikata tamaa kisa umekorofishana kidogo na mpenzi wako, tayari utaanza kutafuta mchepuko. Nimekumbuka kale ka msemo ka Kibonde(R.I.P) " Mchepuko sio dili, baki njia kuu."
Ukikata tamaa kwenye biashara kisa umepata hasara kwenye biashara, utaanza kutafuta waganga eti waje kulinda biashara yako.
Kukata tamaa hufanya uingie kwenye dhambi nyingine ambazo hata kabla haujawahi kufikiria.
Hoja ya msingi ni moja, NI MARUFUKU KUKATA TAMAA.
"Usikate tamaa, una nguvu zaidi ya unavyofikiri," anatukumbusha John Mason, mwandishi wa vitabu naye Nelson Mandela simba wa Afrika aliwahi kusema, "Vitu huwa vinaonekana haviwezi kufanyika mpaka pale vinapofanyika."
Naungana na hoja ya Fannie Flagg aliyewahi kusema, "Usikate tamaa kabla muujiza haujatokea." Watu wengi waliokata tamaa huwa wamebakiza hatua chache za kufikia mafanikio.
Daima kumbuka, mwishoni kila kitu kitakuwa sawa, kama hakijawa sawa huo sio mwisho, endelea kupambana, usikate tamaa.
Siku moja mkuu wa majeshi aliyekuwa ameshambuliwa vya kutosha aliamua kwenda kujificha katika handaki baada ya vita kuonekana imemshinda. Hivyo alijificha ili asiweze kuuwawa.
Akiwa katika handaki lile alishuhudia mdudu akibeba chakula, mdudu yule alikuwa akibeba chakula akifika juu ya andaki alishindwa kuendelea alianguka na kurudi chini. Mara ya pili alianguka tena, huku mkuu wa majeshi akiwa anashuhudia, mara la tatu akaanguka tena. Mdudu yule hakukata tamaa aliendelea kupanda na chakula chake. Mwisho wa siku akafaulu.
Yule mkuu wa majeshi baada ya kuona tukio lile aliamua kurudi vitani, kilichotokea ni historia. Mkuu yule wa majeshi pamoja na wanajeshi wake walishinda katika vita ile.
Wanasema mshindi ni mtu mwenye ndoto, ambaye hakukubali kukata tamaa.
Ukijaribu kukata tamaa kumbuka kampuni ya Coca-Cola iliuza chupa ishirini na tano (25) tu ndani ya mwaka wake wa kwanza wa biashara.
Leo hii mwaka 2019, Coca-Cola wanauza takribani chupa bilioni 1.9 kila siku.
COME & SEE
Edius Katamugora
#KijanaWaMaarifa
0764145476
ekatamugora@gmail.com
#KijanaWaMaarifa
0764145476
ekatamugora@gmail.com
Unaweza kupata vitabu vifuatavyo toka kwangu:
BARABARA YA MAFANIKIO - @7000/=
NAMNA YA KUWA MTAALAMU - @15000/=
0 comments:
Post a Comment