Tuesday, 7 May 2019

TAA NYEKUNDU NA KIJANI ZA MAISHA


Zamani nilipokuwa nikisafiri na kupita katikati ya jiji palipokuwa na mataa na kukuta taa nyekundu zinawaka nilikasirika sana. Nilitamani muda wote taa ya kijani iwake ili tupite.

Siku hizi nikifika na kuona taa nyekundu inawaka nafurahi na kuona inaelezea hali halisi ya maisha.

Tupo katika zama ambazo kila mtu anataka kila kitu anachokifanya kifanikiwe mara moja. Anataka akianza kuimba basi kila mtu amjue, au akiandika kila mtu amkubali na kusema yeye ni mwandishi bora ambaye hawajawahi kumuona. Hawa ni watu wanaopenda taa za kijani muda wote.

Kwenye safari ya mafanikio yoyote lazima utambue kuna taa nyekundu pia🚨, hizi ni zile nyakati ambapo unakumbana na changamoto, unashindwa, unakumbana na vigingi au mambo hayaendi kama ulivyotarajia.

Ukipenda taa za kijani lazima ukumbatie na taa nyekundu. Wanasema bahari shwari haitoi wanamaji hodari. Wajapani wanasema, "Anguka mara saba simama mara 8." Hawa ni watu waliojua kuwa barabara ya mafanikio sio tambarare.

Ukiona mtu kafanikiwa jua kuna taa nyekundu alizipitia zilimwambia STOP ndiyo maana leo hii anatembelea taa ya kijani.


Siku hizi watu wanapenda mafanikio ya haraka maana watu wengi tunaowaona kwenye mitandao ya kijamii, instagram, Whatsapp, snapchat, facebook, kutaja machache orodha ni ndefu au kwenye muvi na series za Kikorea tunawaona wamefanikiwa kwa urahisi kumbe nyuma yake kuna changamoto na misukosuko tusioiona.

Austin Kleon, mwandishi wa vitabu na mtunzi wa mashairi anasema, "Watu wengi wanapenda kuwa nomino na hawapendi kuwa vitenzi."

Mwalimu wangu wa Kiswahili darasa la sita Fr. Kanuti Jumbe alinifundisha kuwa: Nomino ni neno linalotaka jina la mahali, mtu, kitu, hali au tendo.

Tena akanifundisha kuwa: Kitenzi ni neno ambalo huarifu tendo linalofanyika.

Watu wengi wanapenda kuitwa wanamuziki lakini hawaimbi.

Kuna watu wanapenda kuitwa waandishi lakini hawaandiki.

Kuna watu wanapenda kuitwa wapishi bora lakink hawapiki.

Kuna watu wanapenda kuitwa madizaina lakini hawajawahi kudizaini chochote.

Unachokiandika kwenye bio zako za mitandao kiendane na kile unachokifanya. Hautudanganyi sisi unajidanganya mwenyewe.

Usipende mafanikio ya haraka haraka, sio kila kitu utakachokifanya kitaleta matokeo unayoyataka hapo hapo. 

Kumbuka vitu rahisi hufanywa na wengi, na vinavyofanywa na wengi havina thamani au huwa na thamani kidogo.

Maisha yana taa Nyekundu na za kijani. Lazima upitie taa zote. 

Edius Katamugora
Kijana Wa Maarifa
0764146476
ekatamugora@gmail.com

UNAWEZA KUPATA VITABU VYANGU KUPITIA NAMBARI HAPO JUU:
1. Barabara ya mafanikio = 7000/=
2. Namna ya kuwa mtaalamu =15000/=

Hii ni blogu rasmi ya Edius Katamugora, hapa utajifunza maendeleo binafsi, utapata makala mbalimbali zinazohusu biashara, elimu, hamasa na maisha kwa ujumla. Karibu sana katika blogu hii.

3 comments:

Unknown said...

Hongera sana brother, unatupatia maarifa bora sana.
Mungu akubariki na azidi kuzibariki fikra zako.

Unknown said...

Twashukuru sana kwa chakula bora kwa ajili ya uzuri wa ukuaji wa fikra zetu katika maisha yetu.
Barikiwa sana.

Edius Katamugora said...

Asante sana rafiki karibu sana.