Pesa imejificha
katika maeneo makuu matatu, sehemu ya kwanza pesa ilikojificha ni katika
uhitaji.
Biashara yoyote kubwa yenye mafanikio ni
biashara inayotoa suluhu kwa mahitaji yanayohitajika katika jamii. Ukiweza
kutatua uhitaji wa watu kwenye jamii yako au kutatua matatizo ya watu kwenye
jamii yako pesa itakufuata.
Tatizo la watu wengi, wengi wanaoanzisha
biashara zinazokufa kila kukicha ni kwasababu hawatoi majibu ya mahitaji ya
watu katika jamii. Kuanzisha biashara ambayo haitoi suluhisho la mahitaji ya
watu ni sawa na kujibu swali ambalo haujaulizwa.
Kijana mmoja aliyependa kusoma vitabu
aliona kuna shida katika ununuaji wa vitabu akaona kuna uhitaji wa kampuni ya
kuuza vitabu mtandaoni. Akaiita kampuni yake Amazon. Huyu ni Jeff Bezos ambaye
leo hii anatajwa kama tajiri namba moja duniani.
Usijaribu hata siku moja kutoa huduma fulani
bila kuona kama kuna uhitaji. Mimi nimeona ni vyema leo hii kufundisha mada hii
kwasababu nimeona kuna watu wengi wanatamani kujua pesa inakojificha.
Pesa unayoipata au kuipokea haiendani na
kitu unachokifanya lakini inaendana na uhitaji uliopo.
Jamii inayotuzunguka inauhitaji mkubwa lakini
ni watu wachache wanaoona uhitaji huo. “Kuna watu hawawezi kuziona fursa hata
kama zikiwapiga puani,” anasema Strive Masiyiwa.
Kuna hadithi moja ambayo watu wengi katika
eneo la biashara hupenda kuizungumza, sijui umewahi kuisikia? Hadithi hiyo ipo
hivi: Kampuni moja ya uuzaji wa viatu ilihitaji kupanua soko la biashara yake,
hivyo ikaamua kumtuma kijana ambaye alikuwa mfanyakazi katika kampuni hiyo
kwenda katika kisiwa fulani kuchunguza kama kuna uhitaji wa viatu mahali huko.
Kijana yule alipofika katika kisiwa kile
akakuta watu wa kule hawavai viatu kabisa. Kijana yule akatuma ujumbe kwenye
makao makuu ya kampuni yake, ujumbe huo ulisomeka; “Hakuna kabisa soko la
viatu, watu wa huku hawavai viatu.” Kijana yule alirudishwa na kampuni ikaamua
kumtuma kijana wa pili.
Kijana huyu alikuwa makini sio kama yule wa kwanza
alipofika katika kile kisiwa na kukuta watu hawavai viatu yeye akatuma ujumbe
uliosomeka, “Soko ni kubwa, tumeni makonteina ya viatu.” Kijana huyu wa pili
aliona fursa. Fursa ni kama maembe, ukisubiri yaiive, wenzako wanakula na
chumvi.
“Kuwa na rundo
la matatizo. Usiruhusu pesa liwe tatizo mojawapo.” Ni msemo wa Grant Cardone.
Watu wengi ni maskini kwasababu hawajajitoa
kutatua mahitaji yaliyoko katika jamii inayowazunguka. Jiulize swali leo,
kunauhitaji wa kile unachokifanya? Je, kuna uhitaji wa huduma unayoitoa?
Unapoanza kutatua uhitaji wa watu hakikisha
unaongeza thamani kwenye maisha ya watu. “Lengo la biashara ni kutengeneza
wateja,” anasema Peter Drucker, guru wa mambo ya manejimenti.
Ili wateja waje kwenye biashara yako lazima
utoe thamani. Kwa msingi huo nakubaliana na Henry Ford aliyewahi kusema,
“Biashara yoyote inayotengeneza pesa pekee ni biashara ya kimaskini.” Biashara
yoyote unayoona inafanikiwa ni ile inayofanya maisha ya watu yawe bora na ya
kufurahia.
“Toka siku yangu
ya kwanza ya kuwa mjasiriamali maono yangu makubwa ya kutimiza ni kufanya maisha
ya watu yawe bora,” anasema Richard Branson, mfanyabiashara mwenye makampuni zaidi ya mia nne na mwandishi wa kitabu cha Screw It, Let's Do It.
Ukitoa huduma nzuri na bidhaa bora watu
watakuwa tayari kukulipa. Watu watahitaji kufanya kazi na wewe.
Kuna aina mbili za uhitaji unazotakiwa
kuzifahamu.
Aina ya kwanza ya uhitaji ni uhitaji uliopo. Anayefungua duka la
nguo ametizama mahitaji ya watu katika mavazi. Aliyefungua mgahawa ametizama
mahitaji ya watu katika kupata chakula safi. Anayeanzisha saluni mtaani kwako
anatizama uhitaji wa watu katika kuweka vichwa vyao katika hali ya kupendeza na
kuvutia. Daktari anayeanzisha zahanati au kituo cha afya ametizama uhitaji wa
watu katika mambo yanayohusu afya.
Mahitaji ya pili
ni yale unayoweza kutengeneza. Watu wanaweza kuwa hawaoni mahitaji ya kitu
mpaka ukianzishe wewe. Inawezekana watu wengi wanalalamika kuwa uchafu umekuwa
kero mtaani kwako, kumbe hiyo ni fursa ya kuanzisha kampuni ya kukusanya taka.
Watu
hawakuhitaji facebook lakini Mark Zuckerberg aliona anaweza kutengeneza mtandao
unaoweza kuwakutanisha watu wengi kwa wakati mmoja. Huo ndio ukawa mwanzo wa
Facebook iliyoanzishwa mwaka 2004.
(Soma mwendelezo wa makala hii kupitia link hapo juu)
(Soma mwendelezo wa makala hii kupitia link hapo juu)
USISAHAU KUSHARE MAKALA HII KWA RAFIKI YAKO AJIFUNZE PIA.
NA
EDIUS KATAMUGORA
Kijana wa maarifa
0764145476
ekatamugora@gmail.com
Unaweza kupata vitabu vyangu vifuatavyo:
1. BARABARA YA MAFANIKIO ==>7000/=
2. NAMNA YA KUWA MTAALAMU ==> 15000/=
Wasiliana nami kupitia namba hii 07641415476
0 comments:
Post a Comment