Monday, 4 May 2020

ELIMIKA NA EDIUS (4)


Mfahamu William Kamkwamba Kijana Mbunifu Toka Malawi
_________________________________________________

Leo NdegeπŸ›¬ yetu iliyotoka nchini Paraguay inafanikiwa kutua katika kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Lilongwe nchini Malawi. Tunaanza safari ya saa 2.30 kuelekea Wimbe Kasikazini mwa Malawi na kufika kijijini  Masitala. Hapa alizaliwa jamaa anaitwa William KamukwambaπŸ‘‡πŸΎπŸ‘‡πŸΎπŸ‘‡πŸΎ



William alizaliwa Agosti 5, mwaka 1987 huko Dowa Malawi, ni mtoto wa pili kuzaliwa katika familia ya watoto 7 wa Bw. Trywell na Bi. Agnes. Alianza kusoma katika shule ya msingi Wimbe na kuhitimu darasa la 8 kisha akajiunga na shule ya sekondari Kachokolo.

Kutokana na ukame mkali ulioikumba Malawi mwaka 2001 wazazi wake walishindwa kulipa dola 80 sawa na shilingi 184,000/= kama karo hivyo William alishindwa kuendelea na masomo miezi kadhaa baada ya kuanza kidato cha kwanza. Kwa miaka 5 mfululizo hakuweza kwenda shule. Unaambiwa ukame huo ulisababisha karibu familia nyingi kufa njaa, huku Kamkwamba na familia yake wakila mlo mmoja tu kwa siku ulioliwa usiku tu.

Akiwa na miaka 14 badala ya kusema huo sio mwisho wake alianza kuazima vitabu na kujisomea kutoka katika maktaba ya shule aliyokuwa akisoma. Ndipo alipogundua mapenzi yake kwenye mambo ya kielekroniki. Siku moja aliona kitabu kilichoitwa Using Energy ambacho kilikuwa na jalada lenye picha ya tabaini ya pangaboi.







Huo ukawa mwanzo wa yeye kutengeneza pangaboi (windmill) lililoweza kuzalisha umeme wa kumulika taa na kupunguza gharama za kutumia mafuta ya taa yaliyotumika kuwasha chemli na vibatari.

Mfano wa kwanza wa pangaboi William alitumia mota ya redio, kisha akatengeneza pangaboi lake la kwanza lenye urefu wa mita 5 akitumia skrepa za baiskeli, feni ya trekta, shock abzoba ya zamani pamoja na miti.

Aliunganisha pangaboi hilo pamoja betri ya gari, kwa kufanya hivyo aliweza kuzalisha umeme wa kuwasha taa 4 pamoja na kuchaji simu za majirani zao. Mfumo huu ulitengenezwa pamoja na swichi na saketi breka iliyotengenezwa kutumia misumali, waya na sumaku. Anasema wakati anaanza watu wengi waliona ni kichaa na mama yake mzazi akiwemo.

Pangaboi lilirefushwa tena na kufikia urefu wa mita 12 ili liweze kunasa upepo juu ya miti. Pangaboi la 3 liliweza kuzalisha maji yaliweza kutumika kumwagilia mashamba. Habari za William zikaanza kusambaa kama virusi vya Corona.



Taasisi nyingi zikaanza kusafiri kilomita na kilomita kuja kijijini kwa kina William kutazama maajabu ya Kamkwamba. Gazeti la Malawi Daily Times liliandika makala ndefu kuhusu yeye.

Soyapi Mumba na McKay ambao walikuwa wahandisi katika taasisi ya Baobab Health Partnership nchini Malawi waliandika blogu kuhusu yeye na habari zikamfikia Emeka Okafor meneja programu za TEDGlobal.

TEDGlobal ni jukwaa maalumu kwa wafikiriaji na wavumbuzi. Kama haujawahi kusikiliza maongezi ya TedTalk aisee umepitwa na vingi. Nenda YouTube ukatizame.

Emeka Okafor akafanya juhudi,za kumtafuta,William Kamkwamba ili aweze kuwahutubia watu. Spichi ya William kwenye TEDTalk iliyofanyika jijini Arusha Tanzania mwaka 2007 ilimfanya apate washauri, mamenta, wafadhili na makampuni ya kufadhili masomo yake na project nyinginezo.

Kwenye spichi yake anasema hakuwahi kusafiri nje ya Malawi wala kupanda ndege wala kulala katika hoteli, ni uvumbuzi wake huo tu uliomfanya aweze kuvipata vyote hivyo.



William alihitimu chuo cha Dartmouth mwaka 2014. Kamkwamba ameandika kitabu cha historia yake kiitwacho The boy Who Harnessed The wind ambacho pia kilimpa dili la kutengeneza muvi yenye jina hilo kupitia kampuni ya Netflix. Itafute The Boy Who Harnessed the Wind uicheki.




Mwaka 2013 gazeti la TIME lilimtaja kama Kamkwamba katika orodha ya vijana 30 chini ya miaka 30 wanaibadili dunia. Mwaka 2010 katika chuo kikuu cha Florida kitabu chake kilichaguliwa kama kitabu cha watu wote (common book) ambapo kila mwanafunzi aliyejiunga chuoni hapo alitakiwa kuwa nacho.

Mwaka 2014 kitabu hicho pia kilichaguliwa kama kitabu cha watu wote (common book) katika vyuo vya Auburn na Michigan kwenye kitivo cha uhandisi. Kamkwamba alifika kwenye vyuo hivyo ili kujadili kitabu chake na kuhusu maisha yake.



Funzo: Usipuuzie ubunifu. Popote ulipo unaweza kubuni kitu na dunia nzima ikakujua.

#ElimikaNaEdius
✍🏽MwishoπŸ™πŸ½πŸ™πŸ½πŸ™πŸ½

Edius Katamugora
Content Creator
Creative Writer
0764145476
ekatamugora@gmail.com

Hii ni blogu rasmi ya Edius Katamugora, hapa utajifunza maendeleo binafsi, utapata makala mbalimbali zinazohusu biashara, elimu, hamasa na maisha kwa ujumla. Karibu sana katika blogu hii.

0 comments: