Kuna Watu Wanajiona Mapanzi
_________________________
Ili kuifahamu kwa kina nchi ya Kanaani ilimpasa Musa awatume wapelelezi wakaipeleleze nchi ambayo Wana Wa Israeli walikuwa wakielekea.
Basi Musa akachagua mpelelezi mmoja kutoka makabila 12 ya Israeli. Hivyo wapelelezi wapatao 12 wakaenda kuipeleleza Kanaani.
Musa aliwaagiza wakatizame nchi ile mambo yafuatayo, kama nchi ni ya namna gani, watu wanaokaa ndani yake kama ni dhaifu au hodari, kwamba ni wachache au wengi.
Wakatizame nchi ile kama ni mbaya au njema. Kwamba ni nchi ya unono au njaa.
Basi wakaenda huko na baada ya siku 40 wakarudi kwa Musa na Haruni kutoa ripoti ya walichokiona.
Wapelelezi kumi wakasema, nchi ile ni ya maziwa na asali na watu wanaoishi kule ni majitu makubwa kiasi kwamba wao walijiona mapanzi.
Wakaleta taharuki kubwa.
Ndipo akasimama Yoshua na Kalebu wapelelezi wawili waliosalia wakasema nchi ile ina maziwa na asali na watu wa nchi ile ni kama chakula chetu. Hakika tutawashinda. (Hesabu 13,14)
Kuna watu bado wanajiona mapanzi kama walivyojiona wapelelezi. Ni kweli kwamba kile unachokiona unakipata. "Aonavyo mtu nafsini mwake ndivyo alivyo" (Mithali 23:7)
Unajiona wewe ni maskini wa kutupwa ni wazi kwako utaendelea kuishi kimaskini maskini.
Unajiona mjinga ambaye hata ufundushweje huwezi elewa chochote. Ni kwamba bado unajiona kama panzi.
Ukweli ni kwamba vile tunavyojiona ndivyo tunavyotoa matokeo. Hauwezi kufikiria kushindwa, ukawa mshindi. Hata utokee muujiza gani.
Kila kitu huanzia kwenye fikra zetu, kisha uhamia kwenye maneno yetu baadaye matendo hufuata.
Acha kujiona huwezi lolote, wewe si mzuri, wewe si hodari unajidanganya mwenyewe. Picha unayoijenga kichwani kwako ndiyo picha itakayoonekana kwa wengine duniani.
Ukijiona mbaya, hata ufanyeje dunia itakuona mbaya.
Ulishawahi kuvaa nguo ukaona haujapendeza? Ukitoka nje na kuanza kutembea utakuwa mtu wa kujishtukia ukijua haujapendeza na watu wengine wanaona haujapendeza.
Ndiyo maana hata kwenye biblia tunasoma maneno kama haya, "Mimi ni mweusi, lakini napendeza." (Wimbo Ulio Bora 1:5), "Katika mambo yote ninayifanya ninashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyenipenda (Warumi 8:37)
Acha kujiambia maneno yanayokurudisha chini kwani ndiyo yanayoleta uhalisia wako.
Jitoe na kuwa kama kina Yoshua na Kalebu, acha kujiona kama mapanzi. Hata ukiwa katika nyakati za udhaifu wako jisemee maneno ya Joeli, " Aliye dhaifu na aseme, Mimi ni hodari" (Joeli 3:10)
Chunga sana fikra zako zinakuwa maneno yako.
Chunga sana maneno yako yanakuwa matendo yako.
Na Edius Katamugora
Content Creator
Creative Writer
0764145476
ekatamugora@gmail.com
0 comments:
Post a Comment