Friday 7 July 2017

Mambo Magumu Ukiyapatia Muda Yatakuwa Rahisi

Habari mpendwa msomaji wa BIDEISM BLOG. Ni matumaini yangu kwamba u mzima wa afya na unaendelea kupambana na kuweka  jitihada kuhakikisha unasongambele na kufanikiwa.

Tumshukuru Mungu kwa siku nzuri kama ya Leo inayotupa hamasa ya kufanya mambo makubwa. Leo ni siku muhimu kwenye maisha yako, usikubali ipotee.
One day can make you grow.

Karibu katika makala nzuri ya Leo niliyokuandalia.

Nakumbuka nikiwa kidato cha sita nikisoma mchepuo wa PCM katika somo la hesabu kulikuwa na topiki iliyoitwa Probability. Watu wengi waliosoma hesabu kidato cha tano na cha sita wanaifahamu topiki hii vizuri sana.

Kila unayemuuliza atakwambia probability ni ngumu na huwezi kuijibia mitihani.

Yaani toka unaanza kidato cha tano, utaambiwa maneno hayo hivyo hata ukifika kidato cha sita unafahamu kabisa kwamba kuna topiki moja ambayo hata uhitaji kujisumbua kuisoma kwani ni ngumu tu.

Mwalimu wangu wa Hesabu kidato cha sita aliwahi kutuambia kwamba baadhi ya wanafunzi wake aliowahi kuwafundisha na walikuwa hawaijibu topiki hiyo katika mitihani maana maswali ni ya kuchagua walimjibu kwa maneno haya "Mwalimu probability ni probability." Yaani hata ukiifanya kupata maksi zake ni probability.

Kwangu Mimi niliposikia maneno hayo toka kidato cha tano nilibadili upande wa shilingi na kujipanga kupambana na huyo mnyama anayeitwa probability. Tulipofika kidato cha sita uzuri wa mwalimu wangu alikuwa haachi topiki hata moja maana kuna baadhi ya walimu baada ya kugundua topiki hiyo wanafunzi hawaijibii mtihani wameacha kuifundisha kabisa na kuendelea kuwajengea wanafunzi fikra kwamba topiki hiyo ni ngumu na haijibiki. Hali hiyo mwalimu wangu Mr. Amos aliipingana na kujitoa kwa moyo mmoja kufundisha topiki hiyo.

Kusema ukweli toka nianze darasa la kwanza hadi Leo ukiniuliza mwalimu ninayemkubali sitasita kukwambia ni Mr. Amos Kabunhu.

Baada ya kujifunza topiki hiyo niligundua ni topiki rahisi sana na inajibika vizuri tu kwenye mitihani. Lakini wengi waliendelea na ile dhana ya probability ni ngumu.

Nilijitahidi kutafuta maarifa mbalimbali kila kona nilipoyapata yanayohusu topiki hiyo. Kuanzia kwenye Vitabu mbalimbali hadi kwenye madesa (pamphlets). Nia yangu ilikuwa kujibu swali la probability wakati wa mtihan wa Taifa NECTA. Na kila mtu nilimwambia mtaijibia mtihahani topiki hiyo. Wengi walinishangaa na kuona kana kwamba nimechanganyikiwa.

Niliibukia kuwa fundi wa probability na nakumbuka tuliungana na wenzangu kama watatu, na kuunda kikundi kidogo cha watu wanaoijua probability vizuri sana. Darasani tukaanza kuitwa "kamati ya probability."

Wakati wa mtihani wa taifa ulipowadia katika somo la hesabu swali la probability ndilo lilikuwa jepesi sana kwangu na ndilo nililoanza nalo. Kusema ukweli hadi Leo hii mtu anapokuja na kuniambia probability ni ngumu tutabishana hadi kesho na siwezi kumuelewa kabisa.

Tujifunze nini hapa?;

Kwanza kabisa tujifunze kwamba, jambo hata liwe gumu namna gani ukilipatia muda wako litakuwa rahisi. Kila kitu kigumu kikipewa muda kinakuwa chepesi. Kumbuka hata unapoanza kufanya mazoezi. Siku ya kwanza utaumia sana kwenye viungo vya mwili lakini ukizoea utashangaa kuona kufanya mazoezi ni jambo rahisi mno. Ulipoanza kusoma uliona ni jambo gumu lakini Leo unaweza kusoma mwenyewe hadi makala hii. Kuandika hivyo hivyo.

Kumbe kwenye maisha yako mambo magumu ukiyasumbukia na kuyapa muda wako unaweza kuleta mabadiliko makubwa.

Edson Thomas aliweza kutengeneza balbu inayowaka kwa kutumia umeme baada ya kufanya majaribio zaidi ya 1000. Huyu anaweza kuwa fundisho tosha kuhusu jambo ili.

Jambo la pili na la muhimu la kujifunza hapa ni kwamba mawazo na fikra za wengine usizifanye zikawa fikra zako. Watu wakikwambia kwamba kitu Fulani ni kigumu aina maana kwamba kitakuwa kigumu kwako pia. Nakubaliana na Henry Ford aliyewahi kusema "kama unafikiri unaweza au kama unafikiri hauwezi. Majibu yote ni sahihi." Fikra zako wewe zina mchango mkubwa katika maisha yako.

Kuna mtu aliwahi alisema "Nothing is impossible because even the word itself says I'm possible" akimaanisha hakuna kisichowezekana kwa sababu hata neno haiwezekani Lina maana ya inawezekana."

"Mafanikio yapo mikononi mwako."

Ndimi
Edius Katamugora (Bide)
Author and motivational speaker
0764145476
0625951842 (WhatsApp)
Email: ekatamugora@gmail.com

Kitabu changu cha Barabara Ya Mafanikio sasa kinapatikana rasmi. Unaweza kuwasiliana na Mimi kupitia mawasiliano niliyoyaandika hapo juu ili kujipatia nakala yako. Mikoani tunatuma pia.

Washirikishe na wenzako ulichojifunza.

Hii ni blogu rasmi ya Edius Katamugora, hapa utajifunza maendeleo binafsi, utapata makala mbalimbali zinazohusu biashara, elimu, hamasa na maisha kwa ujumla. Karibu sana katika blogu hii.

0 comments: