Friday 12 March 2021

WATU WAMECHOKA KUSUBIRI. OKOA MUDA WAO


Unasubiri mpenzi wako akutumie SMS baada ya neno “Nikwambie kitu,” anachelewa. Unasubiri maji uliyoweka jikoni yachemke upate chai. Unasubiri gari kituoni, yote yanafika yamejaa. Unasubiri mzigo wako ulioagiza mtandaoni, siku unaona kama zimeganda. Unasubiri siku uliyoambiwa kutolewa ‘out’ haifiki. Ukiwa mtoto unasubiri Krismasi au Pasaka ifike ili uvae nguo mpya, nayo unaona haifiki. Siku mshahara ukitoka kwenye ATM kunakuwa na msululu wa watu, unaona kama haufiki, bado unasubiri. Matokeo ya kidato cha nne yanatoka na unasubiri uone umepangiwa shule gani, kila uchao unaona jamaa wamekaa kimya. Unasubiri matokeo ya usaili wa kazi uliyoomba, bado nayo hayatoki.

Matokeo ya haya yote yanasababisha watu kupoteza uvumilivu. Watu wanataka mambo yanayookoa muda. Tazama kote utaona wazi, Taxify ilikuja ili kuokoa muda, rice cooker inaokoa muda, gesi zinaokoa muda wa kupika, sehemu zenye nembo ya FAST FOOD wote hawa wanataka upate chakula fasta, ulipe usepe chao. Kuna ambao wakienda kwenye duka la simu kununua chaja utasikia wakisema, “Nahitaji fast chaja,” kuna watu ni wavivu hadi kutafuna miwa sasa wanatengenezewa juisi ya miwa. Kuna ambao wanasafiri na ndege wanavaa track suit na sendo ili tu wasipoteze muda kuvua mkanda na viatu wakati wa CHECK IN. wale wanaopiga picha za passport size utasikia wakitangaza, “Pata passport size ndani ya dakika 3”

  Haya yote ni kukufanya uonekane haupotezi muda. Ukipatia kuokoa muda wa watu umetoka kimaisha. Jiulize leo, je hiki ninachokifanya au ninachotaka kufanya kinaokoa muda wa watu?

Monday 8 March 2021

Edius Katamugora Afunguka Mazito Kuhusu Kitabu cha Jinsi ya Kuzifikia Ndoto Zako
 Asema Ni kitabu Bora Kuwahi Kuandikwa Kwenye Eneo Lake

Edius Katamugora ni mwandishi mbobevu akiwa ameandika vitabu kadhaa kwenye maendeleo binafsi. Amepata nafasi ya kusoma kitabu cha JINSI YA KUFIKIA NDOTO ZAKO na haya hapa ndiyo anayosema;

“Wakati ujao unamilikiwa na wale wanaoamini katika uzuri wa ndoto zao,” alisema Eleanor Rososevelt mke wa aliyewahi kuwa rais wa Marekani Franklin D. Roosevelt.

Je, wewe una ndoto na unaamini kwamba inaweza kuwa kweli? Kama ni kweli basi kitabu hiki kinakuhusu sana lakini kama wewe pia unazo ndoto lakini bado hauamini kama zinaweza kutimia basi kitabu hiki ni mwanga katika njia yenye giza nene.


Ndoto sio kile unachokiota wakati umelala bali ndoto ni kitu kinachokufanya ukose usingizi. Kwa msingi huo ukiendelea kulala sio rahisi kutimiza ndoto zako, bali ukiamka unaweza kuzifanya ndoto zako kuwa kweli.


Baada ya Mama Teresa kufanikiwa na kuwa maarufu kwa sababu aliwahudumia wagonjwa na watu waliokuwa wakifa katika mitaa ya Calcutta, India, watu ambao aliwahamasisha walimtafuta. Muda mwingi walisema, “Ooh Mama Teresa! Nataka kufanya unachokifanya” Nataka kuacha kila kitu ninachomiliki na kujiunga na kazi yako!” Muda wote alikuwa akiwajibu kwa maneno haya matatu, “Tafuta Calcutta yako.”


 Kwa lugha rahisi tunaweza kusema “Fuata ndoto yako” ni huyu huyu mama Teresa aliyesema, “Kama kila mmoja akisafisha uwanja wake dunia nzima itakuwa safi” kwa mantiki hiyo kama kila mtu akifanya jambo kuhusu ndoto yake dunia inaweza kuwa sehemu nzuri sana.


Binafsi naamini kwamba kila mtu anazo ndoto ambazo anatakiwa kuzifanyia kazi, mwandishi wa kitabu hiki ameandika kwa uzuri na ubora wa juu mbinu na namna mbali mbali za kuzifikia ndoto zako.


Wenye ndoto ni wale watu wanaosema maneno, “Liwalo na liwe” lazima nitimize ndoto zangu. Nilipokuwa natizama filamu ya kizungu iitwayo The Shawshank Redemption nilijifunza kitu kimoja kwamba ukiamua kufanya chochote unaweza kukifanya kikubwa ni kuweka nia na matumaini. Andy Dufresne ambaye aliweza kutoroka gerezani anasema, “Kuwa Bize Ukiishi au kuwa bize ukifa ” maneno haya yamewekwa wazi na mwandishi anapotukumbusha kwamba kuna kitu tunahitaji kufanya kwa ajili ya ndoto zetu, lazima siku tukiondoka tuniani tuache alama.


Mwandishi wa kitabu hiki amenitafakarisha sana aliposema, huwa tukifa wanasema, ร„pumzike kwa amani,” anaendelea kusema kwamba “Kuna watu hawasitaili kuambiwa ampumzike kwa amani maana muda wao mwingi hapa duniani ulikuwa wa kupumzika”.


Amka sasa usibweteke anza kuzifanyia kazi ndoto zako. Kumbuka kwamba watu wote waliofikia ndoto kubwa hawakuanzia pakubwa walianzia padogo. Kuna aliyewahi kusema, “Kinachoanzia juu ni kaburi tu”, hata kama vitu fulani havijakamilika wewe anza tu.


Kwenye safari ya kuifikia ndoto yako au kuzifikia ndoto zako lazima ukumbane na vigingi, lakini kumbuka hakuna ushindi bila mapambano lazima uyashiriki mapambano hayo.


 Kila hatua mpya inahitaji wewe mpya na mbinu mpya lazima uwe umejipanga.


Inawezekana umekua ukisaidia kutimiza ndoto za wengine, sasa ni wakati wako kuamka na kuanza kufanyia kazi ndoto zako, unaanzaje kuzifanyia kazi ndoto hizo, mwongozo ulio katika kitabu hiki ni dira tosha iliyosheheni madini na ramani ya kukupeleka kule unakotaka kufika na hata zaidi.


Nafikiri kitabu hiki ni kitabu bora zaidi kukisoma katika vitabu vya Kiswahili nilivyowahi kusoma kuhusu nama ya kuzifikia ndoto zangu, kimenijenga sana na nimepata vitu vingi vipya ambavyo kweli sikuvifahamu.


Mwandishi wa kitabu hiki, Godius Rweyongeza ni mtu ambaye nimemfahamu na kumfuatilia kwa muda mrefu, mambo mengi anayoyaandika ni yale ambayo tayari anayafanyia kazi na yameleta matokeo hivyo ukifuata kile alichoandika ndugu Godius hautaacha kufika mbali sana.


Nikusihi ukisome kitabu hiki si mara moja bali mara nyingi uwezavyo kwani madini yaliyo humu ni lulu tosha ya kukuvusha wewe katika hatua uliyopo na ukafika katika hatua zingine.


Pia maneno unayoyasoma humu yaweke katika matendo, kuwa na vitu vingi kichwani bila kuviweka katika matendo ni sawa na kuwasha gari bila kuliondoa, haufiki kokote. Ukitaka kufika mbali fanya kwa matendo.


Mwisho wa yote kumbuka, dunia inawapokea kwa mikono miwili wale wanaofanya mambo katika matendo na kwa ubora wa hali ya juu, kwa msingi huo naunga hoja ya Ralph Waldo Emerson aliyewahi kusema, “Kama mtu akiandika kitabu kizuri, akahubiri mahubiri mazuri, au akatengeneza mtego wa panya mzuri kuliko jirani yake, hata akijenga nyumba yake msituni, dunia nzima itatengeneza njia hadi mlangoni kwake.”


Utumie muda wako vizuri maana kila kitu ni zao la muda. Vitu vyote vizuri unavyoviona vilitengenezwa ndani ya muda fulani. Tumia muda wako kujiendeleza na kujifunza kuhusu mambo yanayohusu ndoto zako, tumia muda wako kwa wengine na mwisho tumia muda wako kutengeneza huduma au bidhaa fulani. Hivi ndivyo watu wote wenye ndoto kubwa walivyofanya na kufikia hatua za juu.


Nampongeza sana na tena sana ndugu Godius Rweyongeza kwa kitabu hiki kizuri kinachoelimisha, hamasisha, tafakarisha lakini pia kinaburudisha kupitia stori mbalimbali alizotuwekea humu.


 *Ukianza kusoma kitabu hiki hutokichoka!* 


Ndimi,

Edius Katamugora (Kijana wa Maarifa)

Mwandishi kitabu cha Yusufu Nina Ndoto. 



Rafiki yangu, bila shaka umeona aliyosema Edius Katamugora. Binafsi sima Cha kuongeza labda kukwambia tu kuwa sasa ni zamu yako kupata kitabu hiki. Nakala ngumu ya kitabu hiki ni elfu 20 tu. 


Ukiihitaji soft copy ya kitabu hiki pia inapatikana pamoja na vitabu vingine Viwili kwa elfu 19,999.

Karibu Sana. Tuwasiliane kwa 0755848391 karibu

Tuesday 23 February 2021

  NAMNA SIMU YAKO INAVYOATHIRI MFUMO WA USINGIZI

 Uchunguzi uliofanywa na Tume ya Usingizi ya Marekani mwaka 2011 uliokuwa na kichwa cha, “Mawasiliano ndani ya chumba cha kulala,” uligundua kwamba asilimia 95 ya walishiriki walitazama simu zao  ndani ya saa moja kabla ya kwenda kulala.

 

Mwaka 2016 uchunguzi ulifanywa kwa vijana 2750 huko Uingereza uligundua kwamba 45 asilimia walisema kwamba wamekuwa wakicheki simu zao wakiwa usingizini na 42 asilimia walisema walilala na simu karibu kabisa na kitanda chao.

                           

Pia, uchunguzi uliofanywa na kampuni ya Accel na Kampuni ya Teknolojia ya data Qualitrics, unasema kwamba asilimia 53 ya vijana wa kizazi kipya hutazama barua pepe zao(emails) katikati ya usiku wa manane.

Naye mwandishi Catherine Prince anasema, asilimia 80 ya Waamerika hutazama  simu zao katika kipindi cha nusu saa toka wanapokuwa wameamka.

                             

Takwimu zinasema kwamba nusu yetu hutazama simu zetu usiku wa manane tukishtuka toka usingizini (Vijana wenye miaka 25-34 ni zaidi ya 75 asilimia)

Inawezekana takwimu zote nilizozitaja hapo juu zinakuhusu kwa namna moja ama nyingine. Ni wachache wetu hawana tabia ya kuweka simu mbali na kitanda wanacholalia, tena wengine huweka simu zao chini ya mito wanayolalia. 

                                              

Ni wazi pia kwamba, watu wengi hutazama simu zao mara tu waamkapo. Yaani wengi wa watu siku hizi kitu cha kwanza wanachokumbuka mara tu waamkapo ni simu zao.

Je simu zetu zinaathiri vipi mifumo yetu ya usingizi?

Kila usiku saa mbili hadi tatu kabla ya muda wako wa kulala, kuna kitu homoni ambayo huzalishwa kwenye ubongo wako, homoni hiyo huitwa kwa kitaalamu melatonin. Melatonin  huuambia mwili wako kwamba sasa ni usiku hivyo unapaswa kusinzia.

Kukikucha ambapo mwanga wake ni wa bluu, mwanga huu hupiga nyuma ya jicho asubuhi, na ubongo wako huacha kutoa melatonin.Unajisikia kuamka na tayari mwili wako upo tayari kuianza siku.

Muda unapofika na mwanga wa bluu ukaanza kupotea (pale linapokuja giza au taa za umeme zinapowashwa), melatonin huanza kutoka tena.

Unajua ni kitu gani kingine hutoa mwanga wa bluu? Simu. Pale tunapotumia simu zetu, au kopyuta mpakato kabla ya kwenda kulala, mwanga wa bluu huwa unauambia ubongo wako kwamba sasa ni mchana lazima huwe macho. Kwa namna nyingine tunaifanya mifumo yetu ya mwili iende tofauti na vile tunavyopaswa kuwa na kuharibu mfumo wa ubora wa usingizi tunaopaswa kulala.

 Kushika simu zetu mara tu kabla ya kulala ndicho kitu kinatufanya muda mwingine tushtuke usiku wa manane na kushika simu tukiangalia yale yaliyojili wakati tumelala. Wengine wamekua wakikosa usingizi kiasi kwamba hata muda wa kufanya kazi wanasinzia. Hawa ni watu wanaoua usiku.

Kutokana na kitengo cha Afya ya Usingizi cha Chuo Kikuu cha Harvard cha nchini Marekani wanasema, kuwa na usingizi wa muda mfupi “Inaweza kuathiri uwezo wa kuhukumu, unavyojisikia (mood), uwezo wa kujifunza na uwezo wa kutunza kumbukumbu na inaweza kuleta athari mbaya za ajari na majereha.”

Baadhi ya waliofanya chunguzi kuhusu usingizi wamepata matokeo kwamba kupungua kwa muda wa usingizi unaweza kusababisha unene wa kupindukia na magonjwa ya siku hizi kwasababu ya kupungua kwa mfumo wa mmeng’enyo wa chakula unaotokana na muda wa kupumzika.

Hata matumizi kidogo yam wanga yanaweza kusababisha upungufu wa usingizi. Uchunguzi uliofanywa na wachunguzi wa Chuo Kikuu cha Harvard uligundua kwamba ukitumia IPad kusoma usiku kabla ya kwenda kulala inasababisha kutozalishwa kwa kemikali ya melatonin kwa asilimia 53.

Kupitia chunguzi hivyo ni vyema mno kupunguza ukaribu na simu zetu nyakati za usiku. Kuna vitu vingi sana ambavyo tumekuwa tukivifanya kwenye simu zetu kama mazoea na hatujui kama vina athari kubwa kwetu.

Mambo ya kufanya;

Punguza matumizi ya simu nyakati za usiku.

Hakikisha haulali karibu na simu yako, iweke mbali hii itakusaidia kuepuke tabia ya kushika simu yako usiku wa manane.

Iweke simu yako katika ukimya (silence) ili unapoingia ujumbe wowote wakati wa usiku usikulazimishe kushika simu yako.

Imeandaliwa na

Edius Katamugora

0764145476

ekatamugora@gmail.com 

Saturday 20 February 2021

FANYA HAYA KUWA MAARUFU/MTU WA WATU

                                       

Umewahi kujiuliza kwanini mtu fulani anapendwa sana na watu, au mtu fulani anajulikana sana kwa watu na wewe hujulikani? Au umewahi kujiuliza kwanini mtu fulani unayemjua kuna marafiki zako wengine ambao hutegemei hata kama wanamjua lakini unakuta wanamjua.

 

Je jambo kama hili hutokeaje? Je watu hao ni watu wa namna gani?

Kuna siku nilikuwa nikitembea mjini na rafiki yangu tukaingia kwenye ofisi moja, katika angaza angaza macho nikaona kibao cha ofisi fulani, katika ofisi hiyo kuna mtu anafanya kazi hapo ni rafiki yangu sana wa muda mrefu, lakini sikujua kama wanayo ofisi katika sehemu hile tuliyokwenda.

Yule mtu niliyekuwa naye nikasikia anasema, “Hapa kuna rafiki yangu fulani anafanya kazi katika ofisi hii,” chap kwa haraka nikamuuliza anaitwa nani? Akataja jina, nikashtuka, alitaja jina la yule mtu ninayemfahamu.

Basi bwana nikamuuliza ulimfahamu vipi huyu mtu, akanijibu, “Yule jamaa ni mtu,” Hapo ndipo nikatambua kumbe kuna tofauti kubwa kati ya binadamu na mtu.

Ndipo nikaanza kufanya uchunguzi watu ambao wana tabia za yule mtu rafiki yetu huwa wanaishi vipi na watu na wanafanyaje mambo yao.

Kama unataka kuwa kama mtu niliyemzungumzia fanya mambo haya kuwa maarufu au mtu wa watu;

1.Wajali watu bila kujali wana nini 

                      

Jali kila mtu bila kuangalia ni mkubwa au mdogo ana cheo au ana cheo. Waheshimu watu wote, usiwabague. Kosa kubwa ambalo watu hufanya ni kuwanyenyekea wale tu ambao ni wakubwa wao au wale ambalo wanaweza kuwasaidia. Mtu akija ofisini kwako msaidie huwezi jua kesho na kesho kutwa atakuwa nani. Kuna watu ambao wanajuta kama wangejua Rais Magufuli atakuja kuwa Rais basi wangemtendea mema ili baadae awakumbuke lakini hawakuitumia fursa hiyo vizuri. Wasaidie watu kadri uwezavyo. Jijengee utaratibu wa kwamba kila mtu unayekutana naye ana fursa ya kukusaidia au wewe kumsaidia. Nyenyekea ule vya watu. 

2. Kuwa msikilizaji mzuri, wahase wengine waongee kuhusu wao 

                      

Watu wengi wanapenda kuongea na hawapendi kusikiliza. Tumepewa ndomo mmoja na masikio mawili vitumike vyote kwa uwiano sawa, yaani ongea kidogo na sikiliza sana. Unapoongea unatoa kile unachokijua tu lakini unaposikiliza kuna vitu vingi unajifunza. Nelson Mandela aliwahi kuulizwa ni nini siri ya kuwa kiongozi bora, alijibu, “Ili uwe kiongozi bora jifunze kuwa wa mwisho kuongea,” anasema alipokuwa mdogo baba yake alipokuwa akienda kwenye vikao alikuwa akiwasikiliza watu wote kisha anakuwa wa mwisho kuongea.

Wasikilize watu wanaposema shida zao, sikiliza kuelewa na usisikilize ili uwahi kujibu. Wahase watu waongee zaidi kuhusu wao. Dale Carnegie alikuwa akiendesha darasa la NAMNA YA KUONGEA HADHARANI (PUBLIC SPEAKING COURSE) kuna siku akaishiwa kabisa maneno au mambo ya kufundisha. Ndipo alipoanza kuwaruhusu wanafunzi wake kila mmoja anyanyuke na aanze kuongea kuhusu yeye. Alishtuka kuona watu wengi wanafunguka mambo mengi na wanapenda hasa kufanya hivyo. Aligundua jambo kubwa kwamba watu wanapenda kuongea kuhusu wao. Hayo yakampelekea aandike kitabu kiitwacho HOW TO WIN FRIENDS AND INFLUENCE PEOPLE. Watu maarufu pia waliweza kuingia kwenye darasa lake mmoja wapo akiwa Tajiri na mwekezaji mkubwa Warren Buffet.

Unaambiwa ukiingia ofisini kwa Warren Buffet cheti pekee alichotundika ukutani kwake ni kile alichopewa baada ya kuhitimu kozi ya Dale Carnegie.

    Jifunze kwa kila mtu uanyekutana naye, nakubaliana na Ralph Wardo Emerson aliyewahi kusema, “Kila mtu ninanyekutana naye ni mkubwa kwa njia moja ama nyingine. Kwa kulitambua hilo najifunza kutoka kwake.” 

      3. Tabasamu

              
                       

Tabasamu hubeba ujumbe mzito kwenye uso wa anayelitoa. Tabasamu linasema,, mimi ni mwenye furaha, mimi naufurahia wakati uliopo, mimi nayafurahi maisha, mimi hata iweje sinuni, tabasamu linasema kama nimeshindwa leo kesho nitafaulu. Wachina wana msemo usemao, “Kama huwezi kutabasamu, usifungue duka.” Tabasamu ni ishara ya kuwakaribisha watu wawe karibu yako. Unapokutana na mtu mpya mtazame machoni na kisha tabasamu. Mtu huyo anaondoka na furaha kwamba ulimpokea vyema. Usiwe mtu wa kununa nuna watu watakukimbia.

4. Ongea katika namna ya yale wanayoyapenda watu wengine  

U   Unapokutana na watu ongelea vitu wanavyopenda wao na si unavyopenda wewe, utawaboa. Ongelea matatizo yao na uyape suluhu. Watu watakukimbilia kama wewe ni mtatua matatizo na si mleta matatizo. Kuwa mmoja wa watatua matatizo ya watu, wenye matatizo ni wengi duniani na wale wanaotatua matatizo ni wachache mno kuliko kawaida. “Kama hutatui tatizo wewe ni tatizo,” anasema Mchungaji Sunday Adelaja.

       5.Wapongeze watu bila unafiki

     Mtu fulani anapofanya kitu kizuri kuwa tayari tena mstari wa mbele kumpongeza, mtie faraja na mtie moyo kuwa aendelee kusonga mbele. Usiwe mtu anayechukia mafanikio ya mwenzako. Wanaofanikiwa wanaendelea kufanikiwa kwasababu wanafurahia kuona wenzao wanafanikiwa. Mafanikio hayahitaji wivu, wivu ni kidonda, ukishiriki utakonda. Toa pongezi kila inapohitajika, usisubiri wengine waanze, hata mtu akifanya jambo dogo namna gani kama limefanikiwa mpongeze, ataona unajali. Na watu wanaanza kujali baada ya kuona na wewe unajali.

Imendaliwa Na,

Edius Katamugora

ekatamugora@gmail.com

0764145476 

Tafadhali sambaza (share) ujumbe huu kwa rafiki zako. Sharing is caring.