BIDEISM: PERSONAL DEVELOPMENT

Headlines
Loading...

Saturday 1 April 2023

๐— ๐—•๐—œ๐—ก๐—จ ๐Ÿฐ ๐—ญ๐—” ๐—ž๐—จ๐—ช๐—”๐—™๐—”๐—ก๐—ฌ๐—” ๐—ช๐—”๐—ง๐—จ ๐—ช๐—”๐—ฉ๐—จ๐—ง๐—œ๐—ช๐—˜ ๐—ก๐—” ๐—ช๐—˜๐—ช๐—˜.

Kuna watu ukikutana nao siku ya kwanza tu kuna vitu unaviona kwao na wanakuvutia ndani ya muda mchache wa kukutana nao. Watu hawa si kwamba walishuka toka mbinguni kama Mungu alivyokuwa akiwashushia wana wa Israeli Manna, La hasha. 

Watu hawa kuna mbinu wamejifunza zinazowafanya watu wavutiwe nao. 

Zifuatazo ni mbinu zitakazokufanya uwe na ushawishi mkubwa kwa watu tofauti tofauti; 

1. Kumbuka majina ya watu.

Majina ya watu  yana maajabu mengi. "Sauti tamu kuliko zote duniani kwa watu si mziki mkubwa, bali ni majina yao." Alisema Les Giblin naye Dale Carnegie alikoleza akisema, "Majina ni sauti tamu na muhimu katika lugha yoyote duniani." 

Jaribu kukumbuka siku ulipokutana na mtu ambaye hukujua kama anakufahamu na ghafla akakuita kwa majina yako. Nafikiri ulifurahi sana na ulitaka kuwa na mazungumzo zaidi na huyo mtu. Huo ni mfano kidogo wa kuonesha majina yako yalivyo muhimu. 

Rafiki yangu mmoja aitwaye Iddi Amani Mwamwindi amekwenda mbali na kuweka kichwani majina matatu ya watu wote anaowafahau. Yaani akikutana na mimi ataniita Edius Jacob Katamugora. Huwa namshangaa sana lakini nami naendelea kujifunza. Binafsi nimejifunza kusevu jina zaidi ya moja kwenye simu yangu. Kuna aliyeona jina lefu nililosevu kwa simu yangu akashangaa nawezaje vile kuandika majina yote ya mtu. Ni kitu nimejifunza na napenda sana lakini pia kinabisaidia sana.

Majina ya watu ni muhimu ndiyo maana wengine wamejitengenezea majina yao(Brand) na wanatamani wajulikane kwa majina hayo na wanayalinda kwa nguvu kubwa. Msanii Bruno Mars aliwahi kusema, "Kila mtu huniita Bruno, hawaniiti Peter- hilo ni jina langu la serikali." 

Majina ya mtu ni kitambulisho, yanamtofautisha yeye na mwingine.  Hivyo kujua jina la mtu unamfanya ajisikie wa pekee. Ndiyo maana makapuni utengeneza baji zenye majina ya wafanyakazi wao. Tuzo hutolewa zikiwa na majina ya anayepewa tuzo hiyo. Hapo utaona majina yalivyo na umuhimu. 

Jitahidi kujua majina ya mtu na namna yanavyotamkwa. Hii itakuongezea sifa kubwa sana ukutanapo na mtu. Inaonesha upo makini kiasi gani. "Mwanzo wa hekima ni kuviita vitu kwa majina yake sahihi." Alisema Mwanafalsafa Confucius maelfu ya miaka iliyopita. 

Jitahidi sana kukumbuka majina ya watu. Hata kwenye mawasiliano ya simu waite watu kwa majina yao. Kuna tofauti kubwa kuandika au kutamka maneno haya, "Habari za asubuhi." Na "Habari za asubuhi Bw. Edius / Bi. Anna" tofauti ni kubwa kuliko unavyofikiri. 

Miaka ya nyuma Coca cola walikuwa na kampeni ya kutengeneza chupa zilizokuwa na majina ya watu, kampeni hii ilifanya vyema sana. Hata wewe unaweza kuona namna ya kuitumia kwenye biashara yako. Naamini utanipenda. 

2. Sikiliza kwa umakini

Kuwa msikilizaji mkubwa ni kipaji na ni ujuzi. Unaweza kunolewa. Watu wengi ni wazungumzaji na si wasikilizaji. Ajabu kubwa Mungu wakati wa uumbaji alipiga hesabu kali, akatupa mdomo mmoja na masikio mawili ili tuweze kuwa wasikilizaji sana na si wazungumzaji sana. 


Kuwa msikilizaji ni chanzo cha heshima. Mtu huona kwamba umempa heshima kubwa hivyo anatakiwa kurejesha heshima hiyo. 

Kuwa msikilizaji kuna faida kubwa. Kwanza unajifunza mengi. Kuwa mzungumzaji unatoa yale yote unayoyajua. Jikumbushe kila asubuhi kwamba hakuna chochote utakachosema leo kitakachokufunza lolote bali ukitaka kujifunza lazima usikilize. 

"Kama ukifanya kusikiliza na kuchunguza(kudadisi) kazi yako utapata faida kubwa kuliko utakavyoongea," alisema Robert Baden-Powell. Sikiliza ufanikiwe, sikiliza uendelee. "Watu wengi waliofanikiwa ninaowafahamu ni wale wanaosikiliza zaidi ya kuongea." 

Saikolojia inasema huwa tunapenda watu wanaotupenda. Kuwasikiliza watu ni kuwaonesha upendo juu ya maoni yao. Kukubali kupokea yale tu wanayosema lazima na wao wakukubali wewe. 

Leo jipe jukumu la kuwa msikilizaji sana kuliko kuongea. 

Nelson Mandela alipoulizwa ni kitu gani kikubwa alichojifunza kwenye uongozi alisema, "Kuwa mtu wa mwisho kuzungumza." Ujuzi huu alijifunza toka kwa babu yake. Ukiwa mtu wa mwisho kuzungumza maana yake umewapa watu wote nafasi ya kuzungumza na umewasikiliza vema. 

3. Weka pozi kidogo kabla ya kuwajibu watu.

Hata kama unajua majibu weka pozi kidogo katika kutoa majibu yako. Kitaalamu wanasema hesabu tatu (yaani moja, mbili, tatu) kisha toa majibu. 

Ukijipa pozi katika kutoa majibu unawaonesha watu kwamba maswali au kile walichokisema umekichakata kichwani na unatoa majibu mazuri. 

Ukitoa majibu fasta fasta inaonesha kwamba wewe unataka pointi zako zionekane zina mashiko zaidi kuliko zao. Ukifanya hivyo utakuwa umetoka relini na watu hawawezi kuuona umuhimu wako. 

4. Ongelea kuhusu wao

Bahati mbaya huwa tukikutana na watu tunapenda kujisemea ya kwetu, hii ni mbaya sana. Ni kama kujisifia. Hakuna mtu anaweza kushawishika na mtu anayependa sifa zaidi zaidi watakudharau. 

Unapokutana na watu pendelea kuwazungumzia wao kuliko kujizungumzia. 80% iwe kuhusu wao na 20% asilimia iwe kuhusu wewe. Tumia zaidi maneno "wewe" na "yako" na wala si "mimi" au "yangu." 

Ukifuata mbinu hizi nne ulizojifunza leo utakuwa mtu bomba saaaana linapokuja suala la kufahamiana na watu. Nakutakia yote yaliyo mema mpendwa. 

Wenu mtiifu, 

Edius Katamugora 

Kijana wa Maarifa

Monday 31 May 2021

  BARUA KWA MDOGO WANGU (2)

 


Jumapili 2:30

Mei, 30, 2021

Mpendwa Edgar,

Mambo kiddo, ni matumaini yangu kusikia kwamna hujambo make ni jana Jumamosi nilipoongea na wewe kwenye simu mama na kaka walipokuja kukuona shuleni, ingawa mazungumzo yetu yalikua ya muda mchache ndiyo maana nimesukumwa kukuandikia barua hiyo.

Kwanza jana, nilisahau kukuuliza kama tayari umenunua faili nililokwambia kwa ajili ya kuweka barua hizi ninazokutumia. Lakini kwa ninavyokufahamu tayari utakuwa umefanya hivyo.

Lakini pia nikuombe radhi Jumapili iliyopita sikuweza kukuandikia barua yangu ya pili kama nilivyoahidi kwenye barua yangu ya kwanza kwamba nitakuandikia barua kila Jumapili, sio kwamba nilikosa la kukuandikia, hapana, lakini nilitingwa na majukumu. Leo pia ratiba zangu zilikua zimekaza kidogo lakini imebidi nijiibe usiku huu niweza kukuandikia barua hii.

Natamani sana nikwambie mengi yaliyotokea kwenye ulimwengu wangu wiki hizi mbili zilizopita. Lakini kabla sijasahau, kwenye mazungumzo yetu ya jana ulinipa habari njema ambayo nilikupongeza sana lakini kuna kitu cha muhimu nilisahau kukwambia.

Nakumbuka uliniambia kwamba mwezi uliopita ulikuwa wa 13 darasani na mwezi huu umepanda na kuwa 7. Hizi ni Habari njema na za kufurahisha. Nataka nikwambie kitu kimoja mdogo wangu, kwenye mitihani yako mtu pekee unayepaswa kushindana naye ni wewe mwenyewe. Yaani shindana na wewe wa jana. Unajua huko shuleni walimu wanawaambia mshindane na wenzenu kitu ambacho kitakupa ugonjwa ambao unaua watu wengi ugonjwa huo unaitwa kujilinganisha. Kaka yako niliacha kushindana na watu darasani toka kidato cha pili na imenisaidia sana na sijawahi kufeli (labda niongezee).

Kuna jamaa mmoja nilisoma naye shule ya upili (kidato cha tano na sita) kila matokeo yalipotoka alizoea kujilinganisha na wengine, aliumia sana alipoona mtu fulani kamzidi wakati yeye alikua akitoa sana, nilikuja kukutana naye chuo bado ana tabia hiyo hiyo, utakuta analalamika ana G.P.A ya 4, kuna siku kidogo nimtwange kofi mimi nina G.P.A yangu ya 2.8 na nina furaha yeye na GPA ya 4 analalamika kafanya vibaya. Jitahidi sana kuepuka marafiki  wanaolalamika sana. Watu wa namna hii hata ufanyeje huwa wanaona hasi kila kitu.

Hakikisha unajipa changamoto ya wewe kuwa bora kuliko ulivyokuwa jana kila wakati hii itakusaidia utakapomaliza masomo yako na kuja huku mtaani. Huku maisha hayahitaji mashindano bali yanahitaji ushirikiano. Ni kama timu ya mpira, ili ushinde mechi lazima wachezaji wote washirikiane kuanzia golikipa, uje kwa mabeki, kwa mawinga hadi kwa wafungaji.

Jitahidi pia uwasaidie wenzako kwenye vipindi unavyoelewa kuliko wao, usiache kuwasaidia ukiogopa kwamba watakuja kukuzidi, ukiwa na roho ya hivyo nina wasiwasi na maisha yako ya baadae. Unajua nini mdogo wangu, huwa tunafanikiwa kwa kuwainua wengine.

Sikia Edgar, chochote unachokifanya ni uwekezaji ni kama kupanda mbegu, ukipanda mbegu nzuri utavuna mavuno safi. Kuwa mwema kila wakati na kwa kila mtu, bila kujali umri au kipato, itakusaidia sana. Usimkatie tamaa, mtu yeyote. Miujiza hutokea kila siku.

Nayapenda sana maneno haya ya Maya Angelou aliposema, “Watu watasahau ulichosema, watu watasahau ulichofanya, lakini watu hawatasahau jinsi ulivyowafanya wajisikie.”  

Kabla sijaanza kukuandikia barua hii nilikuwa nasoma Makala ya Tajiri toka Zimbabwe na mmiliki wa kampuni ya Econet ameandika hivi, “Usije ukafanya kosa hili. Kuna watu wengi wanaojiambia wenyewe ‘Nikipata pesa nyingi, nitakaa chini na kuanza kuwasaidia wengine’ ngoja nikwambie siri: Hawajawahi fanya hivyo! Na sehemu kubwa ya kujitoa sio pes ani muda. Na kila mtu ana muda kama mwingine, sisi wote ni mabilionea wa muda” Jitahidi utumie muda na nafasi uliyo nayo utafanikiwa sana.

Hivi Edgar, ulinunua kile kitabu cha Ben Carson cha THINK BIG nilichokwambia ununue? Jana jioni nilikuwa nasoma kitabu hicho na kama unakumbuka kwenye barua yangu ya kwanza nilikwambia umtegemee Mungu katika kila jambo, Carson anasema, “Mungu anajali kila eneo la maisha yetu na huwa anatutaka tumuombe msaada.” Ndipo nikarudi na kukumbuka maneno ya mfalme mwenye hekima sana aliyewahi kuishi aliposema, “Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, kabla hazijaja siku zilizo mbaya, wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo.” (Mhubiri 12:1)

Tena nimekuja kugundua, mimi na Ben Carson hatupishani sana. Aliandika kwenye kitabu chake akisema, “Naianza kila asubuhi na sala na kusoma Biblia, mara nyingi kitabu cha Mithali. Nasali na kusoma Mithali kila jioni.” Nafikiri unakumbuka mara ya mwisho nilikuambia usome mithali kila siku, leo nakuongezea vitabu vya Mhubiri na Joshua Bin Sira, visome upatapo muda.

Katika wiki iliyopita nilibahatika kukutana na Shlomo Sivan toka Israeli ambaye sasa tumekuwa marafiki. Kila siku huwa nakusisitiza ufahamiane na watu wengi, kutana na watu wakukutanishe na watu, ndipo utapata madili. Hakuna atakayekupa dili kama hakufahamu wala hakuamini, hakuna!

Sivan anamiliki kampuni ya kutengeneza programu za kompyuta wanazotumia wahandisi ujenzi, kampuni yake inaitwa Sivan Design ikiwa na makao yake makuu nchini Israeli lakini ana matawi katika nchi za Uganda, Zambia, na Nigeria, sasa anataka kuleta ofisi Tanzania na Ethiopia. Rafiki yangu huyu alinionesha kitu kinachoitwa GIS nilipenda sana hicho kitu kwa maana nilikuwa nasikia kina Spezos wakieleza ila niliona jinsi GIS inavyofanya kazi kwenye miradi kama ya umeme na maji. Ama kweli “Kuna mambo mengi bado ya kujifunza” hayo yalikuwa maneno aliyonambia mzungu huyu. Ndiyo maana huwa nakwambia usiende kulala bila kujua umejifunza nini kwa siku husika, hata kama ni jambo dogo wewe jifunze tu. Elimu ni bahari, wahenga walisema.

Rafiki yangu huyu hakuishia hapo aliniambia Habari za binti yake wa miaka 15 ambaye hadi leo hii amejifunza vitu vingi na ameweza kuvimudu. Anasema binti yake alijifunza kutengeneza Cocktail (Hiki kinywaji najua hujawahi kunywa lakini kwasababu ya umri wako siku moja nitakuonjesha Mocktail walau utapatapata kujua jinsi cocktail ilivyo) kupitia Youtube na sasa anatengeneza Cocktail za viwango vya juu. Si hilo tu binti huyo alitaka kujifunza kucheza muziki ndani ya miezi 2 alikuwa akitumia saa 2 kila siku jioni kujifunza, leo hii ni mnenguaji mzuri.

Unajua Sivan aliniambia nini? Mwanae anaweza kujifunza vitu vingi kwa sababu ya kuwa na nia, kudhamiria na kufokasi. Ukiweza pia kuwa na hivyo vitu vitatu nilivyotaja hapo juu mdogo wangu hakuna kitu kitakachokutatiza kujifunza chochote.

Natamani siku moja ukija mjini nikukutanishe na marafiki zangu ambao waliamua kujifunza mambo peke yao na sasa hivi wanaishi huku mjini kwa hayo mambo waliyojifunza.

Nilimuuliza pia Sivan amewezaje kuwa na kampuni kubwa kiasi kile inayotoa huduma dunia nzima, majibu yake yalikuwa haya; tengeneza bidhaa nzuri na watu watakuja kununua na pili tatua matatizo magumu na watu watakuwa tayari kuingia mifukoni mwao na kukupa pesa zao.

Mdogo wangu, leo nimekuandikia mengi, natamani niendelee lakini nikupe mwanya na wewe kuyatafakati maneno haya na kuyafanyia kazi.

Usisahau kuitunza barua hii kwenye faili lako, umalizapo kuisoma.

Nakutakia masomo mema. Kwa kheri!

 

Nakupenda sana mdogo wangu,

Kaka Yako,

Edius Katamugora. 

BARUA KWA MDOGO WANGU (1)

 


Jumapili, 3:59

Mei 09, 2021

Mpendwa Edgar,

Ni matumaini yangu kwamba u mzima wa afya na unaendelea vizuri na masomo yako. Mimi pia naendelea vema  huku nilipo, ni jambo jema na la kumshukuru Mungu sana.

Inawezekana unashangaa kuiona barua hii make hii ni mara yangu ya kwanza kukuandikia barua, lakini nilipata msukumo huu wa kuandika barua hii nilipo pokea salamu kutoka kwako kwenye barua uliyomuandikia mama mwezi uliopita na ukamwambia anisalimie, kusema ukweli siku ile nilifurahi sana, uliifanya siku yangu kuwa njema sana na nilizipokea salamu hizo kwa uzito mkubwa.

Hivyo nimeona nipatapo muda niwe nakuandikia barua najua muda wako wa masomo hauwezi kukuruhusu kuzijibu barua hizi, usijali na wala usiwaze kuhusu hilo. Pamoja na kuwa ratiba zangu zimebana lakini nitajitahidi kila Jumapili niwe nachukua walau saa moja nikuandikie barua. Kimsingi huku kila siku ni kazi kazi kuanzia saa 11 alfajiri niamkapo hadi jioni ya saa 1 jioni nirudipo nyumbani kasoro Jumapili ambayo ni siku ya mapumziko.

Nimeona katika siku hiyo ya mapumziko walau nitenge muda wangu nikuandikie barua kuhusu mambo mbalimbali.

Nakuomba ununue faili jipya ambalo utakuwa ukizitunza barua hizi, kwani zitakusaidia hata baadaye utakapo kuwa umehitimu masomo yako. Nakuomba ulitunze faili hilo kuliko hata unavyotunza faili lako la mitihani. Kuna vitu vingi ambavyo shuleni hatufundishi nilitamani uvijue mapema usije ukajuta kama mimi kaka yako mimi nilifanya makosa sitaki uje kuyarudi. Mimi ni kama lile jiwe lililotupwa kwenye maji ya yaliyotuama ili watu wakanyage  wapite ili wasilowe. Najua sasa hivi huwezi kunielewa lakini naamini kuna siku utakuja kunielewa.

Leo sitaki kuandika mengi lakini nikukumbushe kumtanguliza Mungu uwapo masomoni na katika shughuli zako kila siku. Upatapo muda hakikisha unasoma kitabu cha Mithali kila siku, binafsi nakipenda kitabu hicho kwasababu kinazo sura 31 ambazo ni sawa na mwezi mmoja mrefu hivyo kila siku kuna kitu cha kusoma toka huko.

Upatapo muda na kuzunguka hapo mjini utafute kitabu cha Daktari Ben Carson kiitwacho Think Big na ukisome. Nilitamani kukutumia kitabu hiki wakati natuma barua hii lakini huku nilipo sikukipata.

Nakutakia masomo mema, Kwa kheri,

Nakupenda sana mdogo wangu,

Kaka Yako,

Edius Katamugora

Thursday 13 May 2021

UNAINZAJE SIKU YAKO?
                                     

Kila asubuhi ni namna mpya ya kumshukuru Mungu kutupa uwezo na pumzi ya kuendelea kuishi.

Hii ni fursa wanayoipata wachache na wala si haki. Wakati unashtuka Leo usingizini kuna mtu alikua anavuta pumzi yake ya mwisho.

...Hilo tu linapaswa kukupa sababu ya kumshukuru Mungu wewe kuendelea kuishi. Bado unayo mengi ya kuifanyia dunia.

Hakuna aliyekuja duniani kuzurura wala kusindikiza wengine, lakini muda mwingine tunaishi kama tumekuja kusindikiza wengine.

Kuna Yule mtu anasema, "Kuna wengine wanaishi, sisi tunaishia." 

Nikuombe kitu kimoja usikubali kuishia.

Huo ni utangulizi Tu wala sikupanga kuongelea Jambo hilo lakini nimeona tu niwakumbushe.

Nirudi kwenye swali langu, unainzaje siku yako?

Baada ya kuamka kitandani na kumshukuru Mungu nini hufuata?

Njia njema na tabia tabia unayopaswa kuifanya ni kuianza siku yako kwa kufanya mazoezi ya mwili.

Amka kitandani, nenda barabarani anza kufanya mazoezi. Kimbia fanya jogging, na mengineyo.

Tabia hii inabidi uifanye kabla dunia haijaamka. Wakati wengine wamelala wewe tayari umeamka.

Mazoezi ni afya, jali afya yako. Usisubiri uwe na magonjwa, sijui presha mara kisukari ndo uanze kufanya mazoezi.

Ukitumia nusu  saa kwenda geuka rudi nyumbani utakua umetumia karibia lisaa.

Mazoezi ya asubuhi si kwamba yanakusaidia kiafya tu hata utendaji.

Namna yako ya kufikiri huwa ya tofauti. Yaani unaiona dunia Kwa jicho  la tatu ama upeo tofauti.

Mazoezi yatakufanya uwe na maamuzi yaliyo nyooka.

Mazoezi ni uraibu(addiction) unaotakiwa kuujenga kwasababu si uraibu hasi bali ni chanya.

Uraibu chanya ni  ule unaoboresha maisha yako. Uraibu hasi ni ule unaoharibu ubora wa maisha yako kama vile uvutaji sigara.

Kinachotokea unapofanya mazoezi ya asubuhi kama kukimbia barabarani asubuhi ni kwamba mnamo Dakika ya arobaini ubongo wako unazalisha kemikali zinazojulikana kitaalamu kama "kemikali za kusavaivu(survival chemicals). 

Majina ya kemikali hizi kwa nianvyojua ni beta endorphins na nerophinphrine. Hizi kemikali huufanya mwili ujisikie poa, sana.

Wakati wengine wanaamka wakiwa wamekereka wewe unainza siku yako kwa uchangamfu.

"Maisha huanza kila asubuhi." (Joel Osteen)


Tuesday 11 May 2021

Mambo Haya Yatakufikisha mbali.


1. Sali Sana
2. Soma sana, chimba mambo kwa undani hasa.
3. Soma Biblia/Kurani asubuhi na jioni
4. Kuwa na kitu kimoja unachokisimamia/fanya na hakikisha watu wanakujua kwa hicho.
5. Ongeza mtandao wako wa watu
6. Ishi na watu vizuri.
7. Jifunze ujuzi mpya, dunia inabadilika kila uchao
8. Mawazo ya kibunifu yafanyie kazi, usiyaatamie hayo sio mayai.

Edius Katamugora
0758594893 (WhatsApp)
KUWA WEWE NA AMINI UNACHOKIFANYA


"Wale ambao wanafikiri ni vichaa kiasi cha kutosha, ndio wataibadili dunia" (Steve Jobs)

Kama haupo tayari kuitwa chizi au kuonekana kichaa, basi tambua kwamba mafanikio kwako ni kitendawili.
 
Kwenye unalolifanya watu kuna hatua hawatakuelewa.
Ngoja niwape mfano.

Wakati naanza kuandika post za PUMBA ZA EDIUS huko Facebook, watu wengi walinijia juu, tena wengine Kwa hasira wakisema, Edius unachafua jina lako, mara ooh unakitu kizuri lakini umekipa jina baya. 

Niliwajibu asante. Siku moja dada mmoja akaniomba namba Facebook nikampa, akanipigia. Akaanza kunihubiria kwamba anapenda makala zangu lakini neno Pumba linamkera. Nikamwambia nitabadilisha, nikaendelea sikuacha kutumia neno Pumba.

Siku nyingine akaja mtu ananiandikia waraka mrefu tena akitumia vifungu vya biblia lakini nikasoma Tu hata sikumjibu.

Nimesikia kelele nyingi kuhusu kutumia neno PUMBA ZA EDIUS lakini ambacho wengi hawajui ni kwamba katika vitabu vyangu vyote Pumba za Edius ndo kitabu kimesomwa na watu zaidi ya 30000 tena kinapendwa kuliko kawaida.

Wengine wananiuliza kwamba sina kingine cha dizaini ile. Nawaambia hapana lakini wanaanipa mawazo ambayo nayafanyia kazi.

Nisingeanza na Pumba za Edius inawezekana hii Menta kama Menta isingekuepo.

Unajua kwenye Sanaa unahitaji ubunifu, kama ukitaka kila kitu kiende kwenye mstari, unakufa. Hakuna atakayetaka kazi zako. Binafsi naamini Sana kwenye ubunifu na kujifunza vitu vipya.

Kama wewe ni msomaji Sana. Pumba za Edius haliwezi kuwa neno lenye ukakasi hata kidogo.

Ngoja niwape mifano kuna hivi vitabu sijui mmewahi kuvisoma?

1. The subtle art of not giving a fuck Mark Manson
2. Everything is fucked
3. Nobody wants to read your shit Steven Pressifield

Hapa Tanzania tuna waandishi wa namna hiyo tena ukisoma wanayoandika ni  noma na nusu

Masoud Kipanya ana kitu anakiita Upuuzi wa Masoud

Jamhuri kuna jamaa anaandika makala anajiita Mzee zuzu

Mwananchi kuna jamaa ana makala zina jina la HEKAYA ZA MLEVI. Ukisoma ndo utajua amelewa au yuko soba.

Nimalize Kwa kusema, kuonekana umekua chizi, watu wasikuelewe ni  sahihi pia kikubwa amini unachokifanya.

Kwenye kitabu chake cha Do the Work Steven Pressifield anasema, "A Child has no trouble believing the unbelievable, nor does the genius or the madman. It's only you and I, with our big brains and our tiny hearts who doubt and overthink and hesitate."

Tangazo: Kama utahitaji kitabu cha PUMBA ZA EDIUS nicheki WhatsApp kupitia namba 0758594893 nitakutumia Bure. Tuma neno PUMBA ZA EDIUS utatumiwa kitabu.

Edius was here

Friday 12 March 2021

WATU WAMECHOKA KUSUBIRI. OKOA MUDA WAO


Unasubiri mpenzi wako akutumie SMS baada ya neno “Nikwambie kitu,” anachelewa. Unasubiri maji uliyoweka jikoni yachemke upate chai. Unasubiri gari kituoni, yote yanafika yamejaa. Unasubiri mzigo wako ulioagiza mtandaoni, siku unaona kama zimeganda. Unasubiri siku uliyoambiwa kutolewa ‘out’ haifiki. Ukiwa mtoto unasubiri Krismasi au Pasaka ifike ili uvae nguo mpya, nayo unaona haifiki. Siku mshahara ukitoka kwenye ATM kunakuwa na msululu wa watu, unaona kama haufiki, bado unasubiri. Matokeo ya kidato cha nne yanatoka na unasubiri uone umepangiwa shule gani, kila uchao unaona jamaa wamekaa kimya. Unasubiri matokeo ya usaili wa kazi uliyoomba, bado nayo hayatoki.

Matokeo ya haya yote yanasababisha watu kupoteza uvumilivu. Watu wanataka mambo yanayookoa muda. Tazama kote utaona wazi, Taxify ilikuja ili kuokoa muda, rice cooker inaokoa muda, gesi zinaokoa muda wa kupika, sehemu zenye nembo ya FAST FOOD wote hawa wanataka upate chakula fasta, ulipe usepe chao. Kuna ambao wakienda kwenye duka la simu kununua chaja utasikia wakisema, “Nahitaji fast chaja,” kuna watu ni wavivu hadi kutafuna miwa sasa wanatengenezewa juisi ya miwa. Kuna ambao wanasafiri na ndege wanavaa track suit na sendo ili tu wasipoteze muda kuvua mkanda na viatu wakati wa CHECK IN. wale wanaopiga picha za passport size utasikia wakitangaza, “Pata passport size ndani ya dakika 3”

  Haya yote ni kukufanya uonekane haupotezi muda. Ukipatia kuokoa muda wa watu umetoka kimaisha. Jiulize leo, je hiki ninachokifanya au ninachotaka kufanya kinaokoa muda wa watu?