“Nilipokuwa na
pesa kila mtu aliniita kaka,” ni msemo wa watu wa Poland. Bila kuwa na pesa
utadharauliwa. Bila pesa hakuna atakayekuwa tayari kukusikiliza. “Ndipo niliposema;
Bora hekima kuliko nguvu, walakini hekima ya maskini hudharauliwa, wala maneno
yake hayasikilizwi.” (Mhubiri 10: 16) Unaweza kuwa na mawazo au hoja nzuri za
kujenga na kuibadili dunia lakini kwasababu u maskini watu hawatakuwa tayari
kukusikiliza.
Bofya hapa kusoma: MAENEO MATATU (3) PESA ILIKOJIFICHA (1)
Eneo la pili
ambako pesa imejificha ni katika ujuzi na maarifa. Ujuzi na maarifa vinakufanya
uweze kuwa mtaalamu katika kile kitu ambacho unatamani kuwa gwiji.
Watu wenye ujuzi
ndio wanaopandishwa vyeo kila kukicha. Watu wenye ujuzi ndio ambao wakikosa
mahali fulani mambo hayaendi. Dunia ya leo inawapokea wataalamu na watu wenye
ujuzi na maarifa kwa mikono miwili na zulia jekundu.
Biashara
utakayoanzisha inahitaji ujuzi. Ujuzi wa kuuza, ujuzi wa kuwasiliana na wateja,
kutaja machache.
Kazi unayoifanya au utakayoifanya
inahitaji ujuzi. Ukiwa na ujuzi watu watakuwa tayari kukulipa kiasi chochote
unachohitaji. Watu wengi hawako tayari katika kukuza ujuzi wao. Tatizo kubwa la
ukosefu wa ajira limechangiwa na watu wengi kuwa na vyeti vyenye alama zinazomeremeta
lakini hawana ujuzi. Ndiyo maana Profesa Elisante Gabrieli wakati fulani
aliwahi kusema, “Waajiri wananunua ujuzi wakati huo huo wahitimu wanauza vyeti
vyao.”
Ukiwa shuleni tafuta ujuzi, usitafute alama kubwa ambazo ndani yake
hazijabeba ujuzi wowote.
Jiulize leo hii
wewe una ujuzi gani unaoweza kukuingizia pesa mfukoni? Kama kuna ujuzi wowote
ulionao tumia jitihada zako nyingi kuuendeleza. “Kitu ambacho wote tunaweza
kukimudu ni juhudi. Weka muda wako mwingi kuwa mtaalamu kwenye kila kitu unachokifanya.
Itakupa faida maana watu wengi hawafanyi hicho kitu,” anasema Mark Cuban.
Unaweza kuwa na kipaji kikubwa
lakini unahitaji ujuzi wa kuendeleza kipaji chako. Kuna watu wengi wanavipaji
vikubwa lakini wanapata kipato kidogo lakini wengine wana vipaji vidogo lakini
wanapata kipato kikubwa. Tofauti kubwa kati ya watu hao wawili ni katika juhudi
ya kuendeleza ujuzi unaoendana na vipaji vyao.
Will Smith aliwahi kusema, “Haijalishi
una kipaji kiasi gani, kipaji kitakufelisha, kama hauna ujuzi. Ujuzi
unapatikana katika kufanya mazoezi. Fanya kazi kwa bidii na jitoe kwa nguvu
zako zote kila siku iitwayo leo.”
Tumia muda wako
mwingi kuendeleza ujuzi wako na kutafuta maarifa. Watu wanasema “Muda ni mali.”
Muda ni kama maji yanayomwagika kwenye maporomoko hayawezi kurudi juu. “Kama
hauthamini muda wako, watu wengine hawawezi kuuthamini. Acha kutoa bure muda
wako na kipaji chako. Thamini unachokijua na anza kuwatoza watu pesa,”
alishauri Kim Garst. Naye The Joker anasisitiza akisema, “Kama wewe ni bora
kwenye kufanya kitu fulani, usikifanye bure.”
Ujuzi ni kama
oksijeni, bila oksijeni hauishi, bila ujuzi sahau kuhusu pesa.
Sehemu ya tatu
pesa ilikojificha ni kwenye ugumu wa kukutoa ulipo. Kila unachokifanya
hakikisha wewe ndiye bora na kinara. Ukiona watu wanaweza kukubadilisha mara
moja mahali ulipo jua kwamba bado haujawa gwiji au kinara katika unachokifanya.
Pambana na hakikisha watu wakihitaji
huduma fulani unayoitoa wewe, utajwe ukiwa mtu wa kwanza. Hakikisha
unajulikana. Watu wanapenda kufanya biashara na watu wanaouwajua.
Kuna msemo usemao, “Si kile unachokijua
bali ni watu wangapi unawajua.” Kadri unavyojuana na watu wengi zaidi ndivyo na
fedha yako inaongezeka. Kadri unavyotoa huduma nzuri kwa watu wengi, watu hao wanakwenda
na kutangaza sifa zako mahali kwingine na jina lako linazidi kukua.
Ukiwa kazini hakikisha unafanya kazi
kiasi kwamba ikitokea siku wanafanya mabadiliko na kuondoa wafanyakazi wewe
usiwe mmoja wao.
Hakikisha watu wanajua unafanya nini. Fanya
mambo kwa utofauti na viwango vya juu. Usifanye kama kila mtu anavyofanya.
Ukifanya kama kila mtu anavyofanya utabaki kuwa kama wao. Julikana kama
Coca-Cola. “Coca-Cola ni biashara pekee duniani, haijalishi ni nchi gani, mji
au kijiji gani ulipo, kama mtu akikuuliza unafanya nini na ukasema unafanya
kazi Coca-Cola, hautawahi kujibu swali, “Hicho ni nini?,” alisema Muhtar Kent.
Ndimi
EDIUS KATAMUGORA
0764145476
ekatamugora@gmail.com
0 comments:
Post a Comment