Wakati mwalimu wangu wa mambo yanayohusu ujenzi (building construction) akinifundisha kuhusu ujenzi wa msingi alinielekeza kwamba, katika ujenzi wa msingi (foundation) ni sehemu ambayo unapaswa kuwa makini mno. Tena wakati tunajifunza kuseti msingi (setting out of the foundation) alisema ukikosea kuseti msingi umekosea kuseti nyumba nzima.
Kwenye ujenzi wa msingi hata wasimamizi huwa wakali kama mbogo maana wanajua msingi usipokuwa imara jengo zima litakuwa bovu. Wakati mwingine inatulazimu kujengea nondo na zege ili kujenga msingi imara na wenye nguvu za kustahimili kubeba uzito wa jengo zima. Nafikiri umeelewa kwa ufupi kwanini ujenzi wa nyumba au jengo lolote huanza na msingi.
Kwenye maisha tunapaswa kujenga msingi;
Maisha yetu vilevile yanahitaji ujenzi wa msingi imara katika kila kitu tunachokifanya.
Maisha yetu vilevile yanahitaji ujenzi wa msingi imara katika kila kitu tunachokifanya.
Kwenye malezi ya watoto tunahitaji kuwa na msingi imara. Mtoto inabidi afundishwe adabu njema na heshima akiwa mdogo. Wahenga walisema "Samaki mkunje angali mbichi." Wengine wakawa na haya ya kusema "Mtoto umleavyo, ndivyo akuavyo." Kumbe ukitaka kumpa mwanao malezi bora mfundishe akiwa mdogo. Wanasakolojia wanasema kwamba muda mzuri kumfundisha mtoto malezi bora ni kuanzia pale anapozaliwa hadi kufikia miaka 12.
Mpendwa msomaji mambo mengi yanahitaji msingi. Kama haujajenga msingi usitegemee kufanya mambo makubwa. Mwalimu wako wa darasa la kwanza alianza kukufundisha " a e i o u." Kisha ukaanza kuunganisha silabi na konsonanti kutengeneza neno moja moja, Leo hii unaweza kusoma makala hii nzima bila shida yoyote. Ni msingi mzuri uliojengewa.
Huwezi kufikiria kuweza kuitumia vizuri milioni moja wakati elfu kumi huwezi kuitumia vizuri, wewe utakuwa unatudanganya. Ukishindwa mambo madogo hata makubwa yatakushinda pia.
Mwanafunzi anayetaka kuwa mwanamahesabu mzuri lazima aanze kujua kuhesabu namba na MAGAZIJUTO kisha mambo mengine magumu hufuata. Hawezi kuanza na mambo magumu hesabu itakuwa ngumu mno. Ndiyo maana ukiwa darasa la kwanza moja kutoa 3 (1-3 = haiwezekani. ) Ukifika la tano inawezekana jibu linakuwa hasi mbili (-2).
Huwezi kutoa huduma nzuri kwa wateja (customer care) kwenye biashara kubwa kama kwenye biashara ndogo uliyoanza nayo customer care ilikua hamna. Mambo yataendelea kuwa yaleyale.
Nakumbuka wakati nikiwa jeshini mujibu wa sheria kwenye kozi yetu wakufunzi wetu wa kozi walikuwa wakisema "Mwanajeshi hutengenezwa ndani ya wiki 6 za mwanzo." Na kweli wiki sita za mwanzo wa kozi huwa ni wiki za mateso makali, kuamsha saa kumi usiku, wiki za kukesha na kufanyishwa mazoezi makali na maovyoovyo ya hapa na pale yaani hakuna kupumzika. Ukimaliza wiki 6 unakuwa tayari umetengenezwa mwanajeshi imara anayeweza kukabiliana na mambo mengi, kama vile urukaji wa viunzi na vikwazo, pumzi ya kutosha ya kukimbia, ushirikiano, nidhamu ya hali ya juu, ujanja wa porini (UP), matumizi ya siraha, kutaja machache. Ukimaliza six weeks ni sherehe kubwa ukiwa kuruti.
Jiwekee tabia ya kujenga msingi katika mambo mengi unayoyafanya. Msingi katika maisha yetu ya kila siku ni jambo la muhimu sana. Kama nyumba inahitaji msingi imara, binadamu pia tunahitaji msingi imara katika yale tunayoyafanya.
"Mafanikio yako mikononi mwako."
Ndimi:
Edius Katamugora
Author and motivational speaker
0764145476
0625951842 (WhatsApp)
Email: ekatamugora@gmail.com
Author and motivational speaker
0764145476
0625951842 (WhatsApp)
Email: ekatamugora@gmail.com
Jipatie kitabu cha Barabara Ya Mafanikio kwa shilingi 6000/= tu. Dar es Salaam, Morogoro, Kagera, Iringa, Mwanza tayari vinapatikana. Mikoani tunatuma pia. Mawasiliano; 0764145476/0625951842
Imani yangu mafanikio ni kitu cha kushirikishana. Mshirikishe pia na rafiki, ndugu au jamaa kile ulichojifunza.
1 comments:
Nice
Post a Comment