Saturday, 7 October 2017

Nitaanzisha Biashara Yangu 2017 III

Habari mpendwa msomaji wa Bideism Blog. Ni matumaini yangu kwamba hujambo na umeamka salama kutimiza majukumu yako ya Leo.
                  
Nikuombe radhi kwa Jana kutoendelea na makala zetu za Nitaanzisha Biashara Yangu 2017 kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu.

Juzi tuliona namna ya kupata wazo la biashara. Ambapo tuliona vitu vitatu vinavyoweza kukusaidia kupata wazo la biashara vikiwemo 1) Anzia na familia yako. (2) Vitu unavyopendelea kuvifanya. (3) Kupitia kusafiri.

Kama hukuweza kusoma makala hiyo bofya hapa; Nitaanzisha biashara Yangu II ili tuweze kwenda pamoja.

Leo nitaendelea kufundisha jinsi ya kupata wazo la biashara kama nilivyokuahidi.

4) Kupitia marafiki na mazungumzo.
Unaweza kupata mawazo mengi ya biashara Kupitia mazungumzo na rafiki zako. Rafiki yako anaweza kukuonesha fursa ambazo wewe ulikuwa huzijui ambazo ukizifanyia kazi unaweza kuleta mabadiliko makubwa.

Mara nyingi marafiki nilionao ni watu ambao wananifungua kiakili kuhusu biashara. Rafiki Yangu na kaka Yangu Godius Rweyongeza siku zote tukizungumza tunaoneshana jinsi ya kufanya biashara mpya, kununua hisa na kuwekeza katika maeneo mbalimbali.

Je wewe ukiwa na rafiki zako huwa mnazungumza nini? Au ndo mnapiga tu stori ilimradi siku ziende. Kuna msemo maarufu unasema "Wewe ni watu watano unaokaa nao muda mwingi." 

Jiulize je marafiki zangu watano ninaotumia nao muda mwingi ni wakina nani na wananisaidia vipi kufunguka kifikra na kibiashara.

"Kama unazungukwa na watu kumi lakini hakuna hata mmoja unayefanya naye biashara. Yakubidi ubadilishe mzunguko wako." Alisema mtu Fulani.

5). Kupitia Malalamiko Ya Watu.
Biashara kubwa huundwa ili kuondoa shida flani. Na shida zinakutwa mahali ambako watu wanalalamika. Watu wakilalamika kuhusu ukosefu wa Huduma za kipesa kama vile MPESA na TigoPesa ni jukumu lako kuanzisha huduma hizo mtaani kwako.

Ukiweza kutatua malalamiko ya watu unaweza kuwasaidia watu wengi na watakuwa tayari kukulipa.

Aliyetengeneza mwavuli aliona watu wakilalamika kuhusu mvua.

Aliyetengeneza kofia aliona watu wakilalamika kuhusu jua.

Aliyetengeneza magari na vyombo vya moto aliona watu wakilalamika kuhusu umbali mrefu.

Aliyefungua hospitali aliona watu wakiugua hapo mtaani kwenu na wakabaki wakilalamika yakwamba hamna hospitali.

Mimi nimeona watu wakilalamika kuhusu kukosa wapi pa kuanzia ili wafungue biashara nikaamua kuandika makala haya ili niwasaidie.

Malalamiko ya watu ni fursa. Ukisikia watu wakilalamika usikubali kuwa mmoja wa walalamikaji. Uzuri wa bara letu la Afrika limejaa shida na matatizo mengi hivyo walalamika ni wengi kupita kiasi. Cheza na malalamiko ya watu. Nakwambia ipo siku utakuja kuninunulia soda.

(6). Mambo ambayo hayaendi sawa.
Kumekuwa na kasumba ya watanzania wengi kufanya biashara moja eneo flani. Yaani huyu akiona kuna frame ya nguo hapa naye kesho atakuja kuuza nguo zake hapohapo la ajabu wote wanauza nguo zilezile. Mwingine ndo kaona huyu kafungua biashara ya majiko ya gesi ya Oryx naye kesho anakuja pembeni na kuuza majiko ya Oryx. Watu wa namna hii wanakosea sana.

Mara zote mjasiriamali ni mtu mbunifu. Hivyo kama unataka kuanza biashara ambayo flani kaianza tayari hakikisha umemsoma jirani yako ipasavyo. Tambua yeye anakosea wapi na mapungufu yake ni yapi. Sasa wewe jaza hapo kwenye mapungufu yake.

Mfano kwa watu niliowaeleza hapo juu.
Mtu "X" anafanya biashara ya nguo: tabia za biashara yake;
1. Anachelewa kufungua.
2. Hana lugha nzuri kwa wateja
3. Nguo zake zina quality ndogo.

Sasa wewe ukiamua kufanya biashara ya nguo Fanya yafuatayo:
 
1. Wahi kufungua na funga wa mwisho kila siku.

2. Tumia lugha nzuri kwa wateja wako. Waambie karibu tena hata kama mtu hajanunua nguo yoyote. Tena kila muda kuwa mtu wa tabasamu. Wachina wanasema "Mtu asiye tabasamu haruhusiwi kufungua duka."

3. Tafuta nguo za quality ya juu kuliko za jirani yako. Ikiwezakana ongeza nguo ziwe tofauti tofauti. Sio jirani yako anauza nguo za kike na wewe hivyo hivyo unauza nguo za kike tena hamna utofauti. Nikukumbushe neno la juzi, "Ujasiriamali ni kuwahi. Ukiwahiwa umekwisha."

Jitofautishe kila unapoamua kufanya biashara. Hata kama upo kwenye biashara tayari kila Mara jitahidi kumsoma jirani yako.

Tukutane kesho kwa mwendelezo wa makala hii ambapo nitazungumzia jinsi ya kupata mtaji wa biashara.

Imani Yangu mafanikio ni kitu cha kushirikishana. Mshirikishe na rafiki yako ulichojifunza.

Ndimi
Edius Katamugora

Mwandishi, Mjasiriamali na Mhamasishaji.
0764145476
0625951842 (WhatsApp)
Email: ekatamugora@gmail.com

Hii ni blogu rasmi ya Edius Katamugora, hapa utajifunza maendeleo binafsi, utapata makala mbalimbali zinazohusu biashara, elimu, hamasa na maisha kwa ujumla. Karibu sana katika blogu hii.

0 comments: