Saturday, 1 April 2023

๐— ๐—•๐—œ๐—ก๐—จ ๐Ÿฐ ๐—ญ๐—” ๐—ž๐—จ๐—ช๐—”๐—™๐—”๐—ก๐—ฌ๐—” ๐—ช๐—”๐—ง๐—จ ๐—ช๐—”๐—ฉ๐—จ๐—ง๐—œ๐—ช๐—˜ ๐—ก๐—” ๐—ช๐—˜๐—ช๐—˜.

Kuna watu ukikutana nao siku ya kwanza tu kuna vitu unaviona kwao na wanakuvutia ndani ya muda mchache wa kukutana nao. Watu hawa si kwamba walishuka toka mbinguni kama Mungu alivyokuwa akiwashushia wana wa Israeli Manna, La hasha. 

Watu hawa kuna mbinu wamejifunza zinazowafanya watu wavutiwe nao. 

Zifuatazo ni mbinu zitakazokufanya uwe na ushawishi mkubwa kwa watu tofauti tofauti; 

1. Kumbuka majina ya watu.

Majina ya watu  yana maajabu mengi. "Sauti tamu kuliko zote duniani kwa watu si mziki mkubwa, bali ni majina yao." Alisema Les Giblin naye Dale Carnegie alikoleza akisema, "Majina ni sauti tamu na muhimu katika lugha yoyote duniani." 

Jaribu kukumbuka siku ulipokutana na mtu ambaye hukujua kama anakufahamu na ghafla akakuita kwa majina yako. Nafikiri ulifurahi sana na ulitaka kuwa na mazungumzo zaidi na huyo mtu. Huo ni mfano kidogo wa kuonesha majina yako yalivyo muhimu. 

Rafiki yangu mmoja aitwaye Iddi Amani Mwamwindi amekwenda mbali na kuweka kichwani majina matatu ya watu wote anaowafahau. Yaani akikutana na mimi ataniita Edius Jacob Katamugora. Huwa namshangaa sana lakini nami naendelea kujifunza. Binafsi nimejifunza kusevu jina zaidi ya moja kwenye simu yangu. Kuna aliyeona jina lefu nililosevu kwa simu yangu akashangaa nawezaje vile kuandika majina yote ya mtu. Ni kitu nimejifunza na napenda sana lakini pia kinabisaidia sana.

Majina ya watu ni muhimu ndiyo maana wengine wamejitengenezea majina yao(Brand) na wanatamani wajulikane kwa majina hayo na wanayalinda kwa nguvu kubwa. Msanii Bruno Mars aliwahi kusema, "Kila mtu huniita Bruno, hawaniiti Peter- hilo ni jina langu la serikali." 

Majina ya mtu ni kitambulisho, yanamtofautisha yeye na mwingine.  Hivyo kujua jina la mtu unamfanya ajisikie wa pekee. Ndiyo maana makapuni utengeneza baji zenye majina ya wafanyakazi wao. Tuzo hutolewa zikiwa na majina ya anayepewa tuzo hiyo. Hapo utaona majina yalivyo na umuhimu. 

Jitahidi kujua majina ya mtu na namna yanavyotamkwa. Hii itakuongezea sifa kubwa sana ukutanapo na mtu. Inaonesha upo makini kiasi gani. "Mwanzo wa hekima ni kuviita vitu kwa majina yake sahihi." Alisema Mwanafalsafa Confucius maelfu ya miaka iliyopita. 

Jitahidi sana kukumbuka majina ya watu. Hata kwenye mawasiliano ya simu waite watu kwa majina yao. Kuna tofauti kubwa kuandika au kutamka maneno haya, "Habari za asubuhi." Na "Habari za asubuhi Bw. Edius / Bi. Anna" tofauti ni kubwa kuliko unavyofikiri. 

Miaka ya nyuma Coca cola walikuwa na kampeni ya kutengeneza chupa zilizokuwa na majina ya watu, kampeni hii ilifanya vyema sana. Hata wewe unaweza kuona namna ya kuitumia kwenye biashara yako. Naamini utanipenda. 

2. Sikiliza kwa umakini

Kuwa msikilizaji mkubwa ni kipaji na ni ujuzi. Unaweza kunolewa. Watu wengi ni wazungumzaji na si wasikilizaji. Ajabu kubwa Mungu wakati wa uumbaji alipiga hesabu kali, akatupa mdomo mmoja na masikio mawili ili tuweze kuwa wasikilizaji sana na si wazungumzaji sana. 


Kuwa msikilizaji ni chanzo cha heshima. Mtu huona kwamba umempa heshima kubwa hivyo anatakiwa kurejesha heshima hiyo. 

Kuwa msikilizaji kuna faida kubwa. Kwanza unajifunza mengi. Kuwa mzungumzaji unatoa yale yote unayoyajua. Jikumbushe kila asubuhi kwamba hakuna chochote utakachosema leo kitakachokufunza lolote bali ukitaka kujifunza lazima usikilize. 

"Kama ukifanya kusikiliza na kuchunguza(kudadisi) kazi yako utapata faida kubwa kuliko utakavyoongea," alisema Robert Baden-Powell. Sikiliza ufanikiwe, sikiliza uendelee. "Watu wengi waliofanikiwa ninaowafahamu ni wale wanaosikiliza zaidi ya kuongea." 

Saikolojia inasema huwa tunapenda watu wanaotupenda. Kuwasikiliza watu ni kuwaonesha upendo juu ya maoni yao. Kukubali kupokea yale tu wanayosema lazima na wao wakukubali wewe. 

Leo jipe jukumu la kuwa msikilizaji sana kuliko kuongea. 

Nelson Mandela alipoulizwa ni kitu gani kikubwa alichojifunza kwenye uongozi alisema, "Kuwa mtu wa mwisho kuzungumza." Ujuzi huu alijifunza toka kwa babu yake. Ukiwa mtu wa mwisho kuzungumza maana yake umewapa watu wote nafasi ya kuzungumza na umewasikiliza vema. 

3. Weka pozi kidogo kabla ya kuwajibu watu.

Hata kama unajua majibu weka pozi kidogo katika kutoa majibu yako. Kitaalamu wanasema hesabu tatu (yaani moja, mbili, tatu) kisha toa majibu. 

Ukijipa pozi katika kutoa majibu unawaonesha watu kwamba maswali au kile walichokisema umekichakata kichwani na unatoa majibu mazuri. 

Ukitoa majibu fasta fasta inaonesha kwamba wewe unataka pointi zako zionekane zina mashiko zaidi kuliko zao. Ukifanya hivyo utakuwa umetoka relini na watu hawawezi kuuona umuhimu wako. 

4. Ongelea kuhusu wao

Bahati mbaya huwa tukikutana na watu tunapenda kujisemea ya kwetu, hii ni mbaya sana. Ni kama kujisifia. Hakuna mtu anaweza kushawishika na mtu anayependa sifa zaidi zaidi watakudharau. 

Unapokutana na watu pendelea kuwazungumzia wao kuliko kujizungumzia. 80% iwe kuhusu wao na 20% asilimia iwe kuhusu wewe. Tumia zaidi maneno "wewe" na "yako" na wala si "mimi" au "yangu." 

Ukifuata mbinu hizi nne ulizojifunza leo utakuwa mtu bomba saaaana linapokuja suala la kufahamiana na watu. Nakutakia yote yaliyo mema mpendwa. 

Wenu mtiifu, 

Edius Katamugora 

Kijana wa Maarifa

Friday, 28 May 2021

  UFAHAMU MTANDAO MPYA WA CLUBHOUSE NA KWANINI UNATAKIWA KUWA HUKO MARA MOJA

 


Miezi miwili iliyopita rafiki yangu Innocent Swai ambaye huwa anaandika katika gazeti la Citizen, (makala zake nyingi huwa zinahusu mambo ya teknolojia) alinipigia simu na katika maongezi yetu alitambulisha kitu kipya. Kitu hicho kipya ulikuwa ni mtandao wa Clubhouse.

Clubhouse ni mtandao ulioanzishwa machi 2020, miezi miwili baadae yaani Mei 2020 Clubhouse ilikua na watumiaji 1500 hadi Desemba 2020 mtandao huo ulikuwa na watumiaji 600,000. Hadi kufikia Januari 2021 mtandao huo ulikuwa na watumiaji zaidi ya milioni 10 kwa wiki.

Kuanzia mwaka jana mtandao huo ulipoanzishwa hadi Aprili mwaka huu mtandao huo ulikuwa ukipatikana kwa watumiaji wa simu zenye uwezo wa IOS hadi mwezi Mei mwaka huu (2021) mtandao huu umeanza kupatikana kwa watumiaji wa Android. Ni bahati yangu pia kuwa miongoni mwa watumiaji wa Android walioanza kutumia mtandao huo mara moja ulipopatikana kwenye simu za Android.

CLUBHOUSE NI NINI?


 

Inawezekana mpaka sasa  unajiuliza mtandao wa clubhouse upoje na je ni kama ilivyo mingine kama vile whatsapp, Instagram, facebook, tiktok na mingineyo.

Clubhouse yenyewe ipo tofauti kidogo. Mtandao huu unatumia njia ya sauti pekee ambayo watumiaji huweza kujiunga kwenye club mbalimbali ili kusikiliza mada ambazo zinakuwa kwenye club tofauti tofauti.

Na uzuri ni kwamba mnapomaliza mazungumzo yenu yanafutika hapo hapo.

Fikiria leo umeingia kwenye chat room unapenda muziki na unasikiliz Daimond au Alikiba wakizungumzia namna wanavyotengeneza muziki mzuri.

Au waza wewe ni mwanasoka na unaingia kwenye chat unakutana na Samatta akizungumzia mada ya mchezaji bora anakuwaje.

Au tuseme wewe ni mjasiriamali, unaingia unakuta Moh Dewji au Dangote wakieleza mbinu mbalimbali za kufanikiwa kwenye ujasiriamali.

Au unapenda mambo ya siasa, utamsikiliza Zitto Kabwe na Januari Makamba wakiwa kwenye jukwaa moja na wakichangia hoja mbalimbali.

Hii ndiyo clubhouse itakayokuwezesha si tu kukukutanisha na watu lakini pia kujifunza mambo mbalimbali kwa gharama nafuu ambazo tumezoea watu wakiwa wanatumia gharama kubwa kufika kwenye semina na warsha mbalimbali.

Wakati naandika makala hii nipo kwenye jukwaa la wanamuziki ambapo watu wanaimba na watu wengine wanawapa nini cha kuongeza. Mtandao kama huu unaweza kukutanisha na watu ambao wanaweza kuwekeza kwako, kama usipojificha. Ama kweli sasa dunia ni kama kijiji.

Hata wachungaji pia wanaweza kuutumia mtandao huu kulitangaza neno la Mungu. Hii ndiyo Clubhouse.

Ili kupata kujiunga na mtandao huu lazima mtu aliyejiunga na mtandao huu akuweke ndo unaanza kupatikana kwenye mtandao. Ukifungua jina la mtandao wa mtu fulani utaona aliwekwa na mtu fulani ambaye alitangulia kuwa kwenye mtandao hupo.

Mfano mimi Edius Katamugora niliwekwa na Jacob Mushi.

Kama unataka kujiunga na mtandao huu unaokua kwa kasi sana. Pakua App yake inayopatikana bure playstore au Apple store kisha muombe mtu akuunge.

Naweza kukupa huduma hiyo pia, sevu namba yangu 0764145476 (Edius Katamugora) kisha niambie nisevu yako na ukishaipakua App utajisajili kisha italeta ombi la wewe kutaka kujiunga.

Jiunge na ulimwengu huu mpya wa teknolojia inayokuwezesha kujifunza toka kwa magwiji.

Tafadhali, usomapo ujumbe huu, share na kwa wenzako pia. Sharing is caring.

Imeandaliwa Na

Edius Katamugora

0764145476 

Tuesday, 11 May 2021

YAH: KUWA NA MAHUSIANO YANAYOELEWEKA


Mojawapo ya kitu kitakacho kufikisha mbali ni kuwa na mahusiano yanayoeleweka.

Sio rahisi kukuta mtu ana wake wengi ukakuta ana maisha yaliyonyooka, tazama hata vijana ambao unakuta kila uchao anamahusiano na mtu mpya, akili zao ni  kupata pesa za kula na kuvaa, full stop.

Hawawezi kingine, hawana malengo hawana mipango na hakuna kitu chochote cha maana wanachofanya.

Ukiwa na mahusiano mengi lazima muda wako ufie huko, utaongea na huyu ukimaliza utampigia huyu. Au ukimaliza kuonana na huyu utaenda kwa kwa yule matokeo yake ni kupoteza muda Tu.

Kwenye Kitabu cha Matatizo si tatizo (Matatizo ni Daraja) Fr. Faustin Kamugisha ametoa stori ya HENRY FORD.

Henry Ford ni mwanzilshi wa kampuni ya kutengeneza magari aina ya Ford.

Akiwa anatimiza Jubilei ya miaka 25 ya ndoa yake, MC alimuuliza aseme nini Siri ya mafanikio ya ndoa yake.

Alijibu, "Siri ni ile ile ninayo tumia kwenye magari, sijawahi badili modeli ya gari."

Wewe unabadili modeli kila siku. Unakutana na mdada mwaka mmoja tu amekuwa kwenye mahusiano na watu 7 tofauti unajiuliza maswali hadi unakosa jibu.

Wakaka ndo usiseme, Leo anapost huyu kesho Yule, yaani vurugu mechi.

Niliandika kwenye kitabu changu cha PUMBA ZA EDIUS "Hakuna fomula inayosema kwamba ukitoka kwenye uhusiano mmoja unganisha na kuanza mwingine. Muda mwingine unahitaji kuwa peke yako ujitafakari na kugundua ulifeli wapi. Jipe muda. Sio lazima kila wakati uwe kwenye uhusiano, muda mwingine unahitaji kuwa na uhusiano na wewe mwenyewe."

Kabla ya kuandika kitabu chake cha THINK AND GROW RICH Napoleon Hill aliwahoji matajiri Zaidi ya 500 ili kupata majibu ya nini kiliwafanya wawe matajiri kuwa na mahusiano yanayoeleweka lilikuwa jibu mojawapo.

Usichukulie poa mahusiano, Yana mchango mkubwa kwenye kufanikiwa au kutofanikiwa kwako.

Imeandaliwa Na
Edius Katamugora
ekatamugora@gmail.com
0758594893 (WhatsApp)

Friday, 12 March 2021

WATU WAMECHOKA KUSUBIRI. OKOA MUDA WAO


Unasubiri mpenzi wako akutumie SMS baada ya neno “Nikwambie kitu,” anachelewa. Unasubiri maji uliyoweka jikoni yachemke upate chai. Unasubiri gari kituoni, yote yanafika yamejaa. Unasubiri mzigo wako ulioagiza mtandaoni, siku unaona kama zimeganda. Unasubiri siku uliyoambiwa kutolewa ‘out’ haifiki. Ukiwa mtoto unasubiri Krismasi au Pasaka ifike ili uvae nguo mpya, nayo unaona haifiki. Siku mshahara ukitoka kwenye ATM kunakuwa na msululu wa watu, unaona kama haufiki, bado unasubiri. Matokeo ya kidato cha nne yanatoka na unasubiri uone umepangiwa shule gani, kila uchao unaona jamaa wamekaa kimya. Unasubiri matokeo ya usaili wa kazi uliyoomba, bado nayo hayatoki.

Matokeo ya haya yote yanasababisha watu kupoteza uvumilivu. Watu wanataka mambo yanayookoa muda. Tazama kote utaona wazi, Taxify ilikuja ili kuokoa muda, rice cooker inaokoa muda, gesi zinaokoa muda wa kupika, sehemu zenye nembo ya FAST FOOD wote hawa wanataka upate chakula fasta, ulipe usepe chao. Kuna ambao wakienda kwenye duka la simu kununua chaja utasikia wakisema, “Nahitaji fast chaja,” kuna watu ni wavivu hadi kutafuna miwa sasa wanatengenezewa juisi ya miwa. Kuna ambao wanasafiri na ndege wanavaa track suit na sendo ili tu wasipoteze muda kuvua mkanda na viatu wakati wa CHECK IN. wale wanaopiga picha za passport size utasikia wakitangaza, “Pata passport size ndani ya dakika 3”

  Haya yote ni kukufanya uonekane haupotezi muda. Ukipatia kuokoa muda wa watu umetoka kimaisha. Jiulize leo, je hiki ninachokifanya au ninachotaka kufanya kinaokoa muda wa watu?

Tuesday, 23 February 2021

  NAMNA SIMU YAKO INAVYOATHIRI MFUMO WA USINGIZI

 Uchunguzi uliofanywa na Tume ya Usingizi ya Marekani mwaka 2011 uliokuwa na kichwa cha, “Mawasiliano ndani ya chumba cha kulala,” uligundua kwamba asilimia 95 ya walishiriki walitazama simu zao  ndani ya saa moja kabla ya kwenda kulala.

 

Mwaka 2016 uchunguzi ulifanywa kwa vijana 2750 huko Uingereza uligundua kwamba 45 asilimia walisema kwamba wamekuwa wakicheki simu zao wakiwa usingizini na 42 asilimia walisema walilala na simu karibu kabisa na kitanda chao.

                           

Pia, uchunguzi uliofanywa na kampuni ya Accel na Kampuni ya Teknolojia ya data Qualitrics, unasema kwamba asilimia 53 ya vijana wa kizazi kipya hutazama barua pepe zao(emails) katikati ya usiku wa manane.

Naye mwandishi Catherine Prince anasema, asilimia 80 ya Waamerika hutazama  simu zao katika kipindi cha nusu saa toka wanapokuwa wameamka.

                             

Takwimu zinasema kwamba nusu yetu hutazama simu zetu usiku wa manane tukishtuka toka usingizini (Vijana wenye miaka 25-34 ni zaidi ya 75 asilimia)

Inawezekana takwimu zote nilizozitaja hapo juu zinakuhusu kwa namna moja ama nyingine. Ni wachache wetu hawana tabia ya kuweka simu mbali na kitanda wanacholalia, tena wengine huweka simu zao chini ya mito wanayolalia. 

                                              

Ni wazi pia kwamba, watu wengi hutazama simu zao mara tu waamkapo. Yaani wengi wa watu siku hizi kitu cha kwanza wanachokumbuka mara tu waamkapo ni simu zao.

Je simu zetu zinaathiri vipi mifumo yetu ya usingizi?

Kila usiku saa mbili hadi tatu kabla ya muda wako wa kulala, kuna kitu homoni ambayo huzalishwa kwenye ubongo wako, homoni hiyo huitwa kwa kitaalamu melatonin. Melatonin  huuambia mwili wako kwamba sasa ni usiku hivyo unapaswa kusinzia.

Kukikucha ambapo mwanga wake ni wa bluu, mwanga huu hupiga nyuma ya jicho asubuhi, na ubongo wako huacha kutoa melatonin.Unajisikia kuamka na tayari mwili wako upo tayari kuianza siku.

Muda unapofika na mwanga wa bluu ukaanza kupotea (pale linapokuja giza au taa za umeme zinapowashwa), melatonin huanza kutoka tena.

Unajua ni kitu gani kingine hutoa mwanga wa bluu? Simu. Pale tunapotumia simu zetu, au kopyuta mpakato kabla ya kwenda kulala, mwanga wa bluu huwa unauambia ubongo wako kwamba sasa ni mchana lazima huwe macho. Kwa namna nyingine tunaifanya mifumo yetu ya mwili iende tofauti na vile tunavyopaswa kuwa na kuharibu mfumo wa ubora wa usingizi tunaopaswa kulala.

 Kushika simu zetu mara tu kabla ya kulala ndicho kitu kinatufanya muda mwingine tushtuke usiku wa manane na kushika simu tukiangalia yale yaliyojili wakati tumelala. Wengine wamekua wakikosa usingizi kiasi kwamba hata muda wa kufanya kazi wanasinzia. Hawa ni watu wanaoua usiku.

Kutokana na kitengo cha Afya ya Usingizi cha Chuo Kikuu cha Harvard cha nchini Marekani wanasema, kuwa na usingizi wa muda mfupi “Inaweza kuathiri uwezo wa kuhukumu, unavyojisikia (mood), uwezo wa kujifunza na uwezo wa kutunza kumbukumbu na inaweza kuleta athari mbaya za ajari na majereha.”

Baadhi ya waliofanya chunguzi kuhusu usingizi wamepata matokeo kwamba kupungua kwa muda wa usingizi unaweza kusababisha unene wa kupindukia na magonjwa ya siku hizi kwasababu ya kupungua kwa mfumo wa mmeng’enyo wa chakula unaotokana na muda wa kupumzika.

Hata matumizi kidogo yam wanga yanaweza kusababisha upungufu wa usingizi. Uchunguzi uliofanywa na wachunguzi wa Chuo Kikuu cha Harvard uligundua kwamba ukitumia IPad kusoma usiku kabla ya kwenda kulala inasababisha kutozalishwa kwa kemikali ya melatonin kwa asilimia 53.

Kupitia chunguzi hivyo ni vyema mno kupunguza ukaribu na simu zetu nyakati za usiku. Kuna vitu vingi sana ambavyo tumekuwa tukivifanya kwenye simu zetu kama mazoea na hatujui kama vina athari kubwa kwetu.

Mambo ya kufanya;

Punguza matumizi ya simu nyakati za usiku.

Hakikisha haulali karibu na simu yako, iweke mbali hii itakusaidia kuepuke tabia ya kushika simu yako usiku wa manane.

Iweke simu yako katika ukimya (silence) ili unapoingia ujumbe wowote wakati wa usiku usikulazimishe kushika simu yako.

Imeandaliwa na

Edius Katamugora

0764145476

ekatamugora@gmail.com 

Wednesday, 10 February 2021

SABABU 4 MUHIMU KWANINI UANZE KUTUMIA EMAIL (BARUA PEPE) MARA MOJA  KUANZIA SASA

 Uchunguzi wangu mkubwa nilioufanya siku za hivi karibuni nimegundua kwamba watanzania wengi hawana kabisa utaratibu wa kutumia email mara kwa mara. Wengi wa watu niliowafanyia uchunguzi hawana kabisa email na hata wale wenye nazo hawajui namna ya kuzitumia.

                             

Ni siku si nyingi zimepita nimekutana na mwanafunzi wa chuo kikuu hajui kabisa kutumia email, inasikitisha.

Ukimwambia mtu akutumie kitu fulani kwenye email ni kana kwamba umemtukana. Sasa katika zama hizi za mapinduzi ya nne ya viwanda na nyakati hizi za zama za taarifa ni muhimu sana kutumia email ili mambo yako yaende sawasawa.

Inawezekana sasa hivi usinielewe na uanze kusema jamaa anaongea upuuzi gani huyu, lakini siku yakikukuta yatakayokukuta utakuja kunikumbuka.

sikutishi ila huo ndio ukweli. Sasa kabla sijaenda mbali hebu nikupe faida 4 za kutumia email (nafikiri ukizijua hizi faida 4 utaanza kutumia email yako mara moja kuanzia sasa);

1. Email hutunza kumbukumbu

Watu wengi wamezoea kutumiana taarifa mbalimbali na wengine mafaili muhimu kupitia mitandao ya kijamii kama vile WhatsApp na Telegram na mingnineyo lakini mitandao hii huweza kufuta mafaili hayo ama si rahisi kuyapata unapopoteza simu yako au simu yako kupoteza mafaili.

                                     

Unapokuwa na email hakuna kinachopotea. Mtu akikutumia ujumbe fulani unaweza kupata hata baada ya miaka kumi. Sasa kwanini bado unaendekeza mambo ya WhatsApp wakati unatuma vitu muhimu kwa marafiki zako na hata mambo mengine ya kikazi na biashara?

2. Email ina faragha zaidi ya mitandao ya kijamii

Kudukuliwa limekuwa jambo la kawaida sana kwa Tanzania na Afrika kiujumla. Chunguzi zinasema hadi sasa Afrika kiujumla ina ukosefu wa wataalamu wa udukuzi zaidi ya 100,000. Taarifa zaidi zinasema dukuzi zaidi ya 96% hufanyika Afrika na haziripotiwi.

                          

Dukuzi nyingi sikuhizi hufanyika katika mitandao ya kijamii. Email ni njia salama ambayo faragha yake ni kubwa sana kuliko ya mitandao ya kijamii.

Kama una mambo yako ya muhimu na ya siri nakushauri utumie zaidi email kuliko kutumia mitandao ya kijamii kuyafanya.

3. Email ni njia salama na nzuri ya kuhifadhi mawasiliano yako

Unakumbuka kipindi umepoteza simu ulipitia changamoto gani? Unakumbuka siku ulipompigia  mtu fulani simu akakwambia alipoteza simu na hivyo hakuwa na namba yako? Haya yote hufanyika kwasababu watu wengi si watumiaji wa email.


Ukiwa na email unaweza kuhifadhi mawasilianao yako yote. Mpaka leo hii email yangu ina mawasiliano zaidi ya 1000 ambayo hata ningekuwa na line ngapi nisingeweza kuyatunza.

Siku nyingine ukipoteza simu na ukakosa kuwa na namba za watu jua tu ni uzembe wako sio uzembe tu bali uzembe uliopindukia.

4. Ni njia rasmi ya mawasiliano ya kikazi

Siku hizi mawasiliano mengi ya kikazi yanafanyika kwa njia ya email. Usishangae siku moja bosi wako anakwambia niandikie email. Ni muhimu pia kujifunza namna nzuri na bora ya kuandika email sasa. Nimeona siku hizi Gmail wameweka hadi sehemu ya kufanyia vikao kwa njia ya video kama ilivyo kwa mtandao wa Zoom mambo yanazidi kuwa makubwa kila uchao.

5. Email Haipunguzi ubora wa kitu

Nafikiri si mara ya kwanza kusikia kwamba ukimtumia mtu picha kupitia Whatsapp ubora (quality) wake huwa unapungua. Unfanyaje kuepuka shida hii? Email ni jibu tosha. Ukitumia email hauwezi kupunguza ubora wa picha au kitu kingine, picha yako inapokelewa kwa ubora ule ule.

 

Imeandaliwa Na

Edius Katamugora (Kijana wa Maarifa)

0764145476

ekatamugora@gmail.com

Friday, 5 February 2021

KOZI ZA AFYA NA VYUO VYAKE TANZANIA

 Catholic University of Health and Allied Sciences (CUHAS), Mwanza (Bugando)

1.      Bachelor of Medical Laboratory Sciences

2.      Bachelor of Pharmacy

3.      Doctor of Medicine

4.      Bachelor of Science in Nursing

5.      Bachelor of Science in Medical Imaging and Radiotherapy

                                                      

 

St. Francis University College of Health and Allied Sciences (SFUCHAS), Ifakara

1.      Doctor of Medicine

                           

St John's University of Tanzania (SJUT), Dodoma

1.      Bachelor of Pharmacy

2.      Bachelor of Science in Nursing

 

Muhimbili University of Health and Allied Sciences (MUHAS), Dar es Salaam

1.      Bachelor of Pharmacy

2.      Bachelor of Medical Laboratory Sciences in Clinical Chemistry

3.      Bachelor of Medical Laboratory Sciences in Hematology and Blood Transfusion

4.      Bachelor of Medical Laboratory Sciences in Histotechnology

5.      Bachelor of Medical Laboratory Science in Microbiology and Immunology

6.      Bachelor of Medical Laboratory Sciences in Parasitology and Medical
Entomology

7.      Bachelor of Science in Environmental Health Sciences

8.      Bachelor of Science in Radiation Therapy Technology

9.      Bachelor of Science in Nursing

10.  Doctor of Dental Surgery

                                        

11.  Doctor of Medicine

12.  Bachelor of Medical Laboratory Sciences General

                       

Hubert Kairuki Memorial University (HKMU), Dar es Salaam

1.      Doctor of Medicine

2.      Bachelor of Science in Nursing

Kampala International University in Tanzania (KIUT), Dar es Salaam

1.      Doctor of Medicine

2.      Bachelor of Pharmacy

                                               

Kozi Nyingine za Afya

1.      Bachelor of Science in Radiation Therapy Technology (BSc RTT)

2.      Bachelor of Science in Prosthetic and Orthotics (BScPO)

3.       Bachelor of Medical Laboratory Sciences in:
(i) Clinical Chemistry
(ii) Hematology and Blood Transfusion
(iii) Histotechnology
(iv) Microbiology and Immunology
(v) Parasitology and Medical Entomology and,
(vi) Bachelor of Medical Laboratory Sciences General

                         

4.      Bachelor of Science in Optometry

5.      Bachelor of Science in Medical Imaging and Radiotherapy

6.      Bachelor of Science in Clinical Nutrition and Dietetics and Bachelor of Science in Food, Nutrition and Dietetics

 

 Imeandaliwa na,

Edius Katamugora (Kijana wa Maarifa)

0764145476

ekatamugora@gmail.com